Mchezaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ pamoja na vilabu vya Yanga na Simba, Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’ ametoa maoni yake kuhusu mchezo wa marejeano wa Ligi ya mabingwa Afrika hatua ya makundi, Yanga SC dhidi ya Medeama FC ya nchini Ghana huku akiwataka mashabiki wa klabu hiyo kumpa muda zaidi kocha Miguel Gamondi kwaajili ya kuiandaa timu na siyo kutoa presha kuelekea mchezo huo.
Jembe Ulaya amesema kuwa, Yanga mpaka sasa wameshafikia malengo yao Kimataifa msimu huu, hivyo wanapaswa waongeze wachezaji wenye ubora zaidi ili kwenda mbele ya hapo walipofikia.
“Kwa sasa hivi ukiiangalia Yanga wamesha-prove, malengo yao ya kwanza yalikuwa kuingia group stage na wamefanikiwa. Lakini kuhusu kwenda robo fainali kwa Yanga inatakiwa tumpe mwalimu muda wa kuitengeneza timu ya kwenda robo fainali au nusu fainali.
“Yanga wana wachezaji wazuri lakini lazima waongeze wachezaji wenye quality kubwa zaidi, ili kwenda kwenye ufalme wa Afrika. Naona baadhi ya wachezaji wakibaki Afrika na quality nyingine zikaongezwa, kwa hii misimu inayokuja, Yanga kwenda robo fainali au nusu fainali itakuwa sio issue,” amesema Jembe Ulaya.