Home Habari za michezo SIMBA WASHINDWE WENYEWE MWAMBA KAVUNJA MKATABA HUKO

SIMBA WASHINDWE WENYEWE MWAMBA KAVUNJA MKATABA HUKO

Kiungo wa klabu ya Union Touarga ya Morocco, Eric Mbangossoum mwenye umri wa miaka 23, amevunja mkataba na klabu hiyo hivyo ni dodo kwa Simba ambao wanatajwa kunyatia saini yake.

Licha ya Simba kuwa na uhitaji wa mchezaji huyo, itaingia vitani na Wydad Casablanca na RS Berkane ambao pia wameonyesha nia ya kuwania saini ya kiungo huyo mkabaji.

Awali gazeti hili liliripoti kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha kuthibitisha kumhitaji kiungo huyo ‘mkata umeme’ wa kusaidia kuifanya timu kuwa na muunganiko mzuri eneo la kati hadi mbele.

Kwa mujibu wa meneja wake ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini alilithibitishia gazeti hili kiungo huyo amevunja mkataba na klabu yake tayari yupo sokoni dirisha hili la usajili. “Ofa ni nyingi na Simba ni miongoni mwa timu zinazomtaka pamoja na Wydad na RS Berkane zote zimeonyesha nia ya kumhitaji kiungo huyo ambaye anaitumikia timu ya taifa ya Chad;

“Siwezi kuzungumza ni ofa gani ambayo ni kubwa kwetu kwani huu ni muda wa usajili, timu yoyote ambayo itafanya ushawishi mzuri na kumhakikishia mchezaji wetu kupata nafasi ya kucheza itakuwa na faida kubwa ya kumpata.” alisema meneja huyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.

Habari kutoka ndani ya klabu ya Simba zinasema kwa sasa mabosi wa timu hiyo wameanza mazungumzo na Eric baada ya Benchikha kuwaeleza anamhitaji mtu huyo kikosini.

Kwa muda mrefu, Simba imekuwa na uhitaji wa kiungo mkabaji atakayeweza kuwaongezea nguvu mabeki wa kati licha ya kuwasajili na kuwatumia viungo kadhaa wa nafasi hiyo akiwamo Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute na Mzamiru Yassin kwa nyakati tofauti, lakini wameonekana hawampi kocha kile ambacho anakitaka.

Pia inaelezwa kitendo cha kumkosa Kanoute katika mchezo ujao wa makundi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba itakaporudiana na Wydad ya Morocco kutokana na kutumia adhabu ya kupewa kadi tatu za njano, imemvuruga Benchikha na kuwasisitiza mabosi wa klabu hiyo kufanya usajili huo haraka iwezekanavyo.

Kukosekana kwa Kanoute kunaifanya Simba kusaliwa na viungo wakabaji wawili pekee Mzamiru na Ngoma ambao wamekuwa wakitumika mara kwa mara.

Amezaliwa Mei 26, 2000 katika jiji la N’Djamena kuanza kucheza soka la ushindani mwaka 2017 aliposajiliwa Racing Bafoussam ya Cameroon kwa msimu mmoja kabla ya kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Chad akiwa na Elec-Sport mwaka 2018 na kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa msimu huo.

Pia amecheza soka la kulipwa katika klabu ya Futuro Kings ya Guinea ya Ikweta na mwaka 2020 alitua rasmi Union Touarga ya Morocco aliyonayo hadi leo akisaidia kuipandisha daraja na kwenye soka la kimataifa kwa timu ya taifa alianza kuichezea tangu mwaka 2019 alipoitwa kwa mara ya kwanza 2019 na kucheza mechi ya kuwania Fainali za Kombe la Dunia chini ya Kocha Emmanuel Tregoat dhidi ya Sudan na timu hiyo kulala 3-1.

Kiungo huyo anasifika kwa kutumia miguu yote miwili, kukaba kwa kutumia akili mbali na umahiri wa kutoa pasi kiufundi na kuituliza timu pale inaposhambuliwa akisaidia ukuta wa timu ndani ya timu ya taifa na hata klabu anayoichezea kwa sasa.

SOMA NA HII  KAMA UTANI KIPA MRUNDI AIBUKIA KAMBINI KWA YANGA