Home Habari za michezo KITAMBI FULL UBABE GEITA GOLD

KITAMBI FULL UBABE GEITA GOLD

KOCHA TANZANIA PRISONS...

Kocha Mpya wa Geita Gold, Denis Kitambi na msaidizi wake, Lucas Mlingwa wameanza vyema kibarua chao ndani ya timu hiyo baada ya kuiongoza leo kupata ushindi kwenye mchezo wake wa Ligi Kuu dhidi ya Singida Fountain Gate.

Timu hiyo ilimtangaza Kitambi juzi kuwa kocha mkuu wa klabu hiyo saa chache baada ya kutangaza kuistisha mkataba na aliyekuwa kocha mkuu, Hemed Suleman ‘Morocco’ kwa madai ya kutingwa na majukumu ya timu ya taifa akiwa ameiongoza kwa miezi sita kuanzia Julai 21 hadi Desemba 20, mwaka huu akishinda mechi tatu, sare nne na kupoteza tano.

Mchezo huo umepigwa jana Desemba 21, 2023 kuanzia saa 10:00 jioni katika Uwanja wa Nyankumbu, mkoani Geita huku Geita Gold ikiibuka na ushindi wa bao 1-0, ukiwa ni ushindi wa nne msimu huu kwenye ligi na ushindi wa tatu mfululizo katika Uwanja wa Nyankumbu.

Ushindi huo ni wa kwanza kwa Geita Gold kuifunga Singida Fountain Gate katika mechi tatu timu hizo zilipokutana kwenye Ligi Kuu ambapo mchezo mmoja umemalizika kwa sare huku Singida ikishinda mchezo mmoja.

Kichapo hicho ni cha kwanza kwa Singida Fountain Gate tangu ilipopoteza kwa mabao 2-0 ugenini mbele ya Yanga katika Uwanja wa Benjamin, Mkapa jijini Dar es Salaam Oktoba 27, mwaka huu.

Bao la Geita Gold limefungwa na mshambuliaji, Valentino Mashaka kwa kichwa dakika ya 78 zikiwa ni dakika 26 tu tangu ameingia mchezoni dakika ya 52 akichukua nafasi ya winga, Yusuph Mhilu.

Bao hilo ni la nne kwa mshambuliaji huyo katika Ligi Kuu tangu amejiunga na Geita Gold mwanzoni mwa msimu huu akitokea Ruvu Shooting, hivyo kuwa kinara wa mabao kikosini hapo.

Kiungo wa Singida, Mbrazil, Bruno Gomes, ameshindwa kuifungia timu yake bao la kuongoza dakika ya 55 baada ya kukosa mkwaju wa penalti ambao umedakwa na kipa wa Geita Gold, Costantine Malimi. Penalti hiyo imepatikana baada ya nahodha wa Geita, Samwel Onditi kunawa mpira waakati akijaribu kuokoa hatari kwenye eneo lao.

Timu zote mbili zimefanya mabadiliko ya wachezaji kuleta uhai kwenye vikosi vyao, ambapo Geita Gold imewatoa Yusuph Mhilu, Raymond Masota na Edmund John na kuwaingiza Offen Chikola, Valentino Mashaka na Yusuph Dunia dakika ya 46, 52 na 82.

Kwa upande wao, Singida wamewapumzisha Marouf Tchakei, Habib Kyombo, Mukrim Issa, Duke Abuya na Bruno Gomes huku nafasi zao zikichukuliwa na Yahya Mbegu, Dickson Ambundo, Elvis Rupia, Deus Kaseke na Meddie Kagere mnamo dakika ya 46, 68 na 71.

Baada ya ushindi huo, Geita Gold imefikisha pointi 16 na kupanda hadi nafasi ya 10 kutoka ile ya 13, huku Singida Fountain Gate ikibaki na alama zao 20 katika nafasi ya nne.

SOMA NA HII  AZIZ KI AFICHUA SIRI HII YA KUIFUNGA AZAM