Home Habari za michezo SERIKALI YAPIGA KWENYE MSHONO UWANJA WA UHURU

SERIKALI YAPIGA KWENYE MSHONO UWANJA WA UHURU

Serikali imevifunga viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru, Dar es salaam mpaka hapo ukarabati utakapokamilika Oktoba 2024.

Taarifa ya serikali imekuja baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza kuufungia Uwanja wa Uhuru, kwa michezo ya Ligi Kuu kwa kukosa vigezo.

Katika taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Aron Msigwa wa Wizara ya Utamaduni Sanaa na Michezo imesema kuwa ni muhimu kuzingatia kanuni zinazosimamia Ligi Kuu na michuano ya kimataifa ndio maana viwanja vya Benjamin Mkapa na Uhuru vimefungwa.

“Kwa taarifa hii timu zilizoomba kutumia viwanja vyao vya nyumbani zinajulishwa kutafuta viwanja vingine Wizara inaomba radhi kwa usumbufu wowote ambao wanamichezo wataupata kutokana na kufungwa kwa viwanja hivi,” amesema Msigwa.

Katika taarifa iliyotolewa na TFF ilisema Uwanja wa Uhuru umefungiwa kutokana na miundombinu yake kutokidhi matakwa ya kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya kanuni ya leseni za klabu.

Timu ambazo zilikuwa zikiutumia Uwanja wa Uhuru kama uwanja wa nyumbani ni Simba na KMC FC ambazo sasa zitalazimika kutafuta viwanja vingine.

Hii ni mara ya kwanza Uhuru kufungiwa tangu ulipofanyiwa marekebisho mwaka 2019 kwa ajili ya michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika za Vijana zilizofanyika hapa nchini.

Viwanja vingine ambavyo vimefungiwa msimu huu ni Ali Hassan Mwinyi cha Tabora, CCM Kambarage cha Shinyanga na Liti mkoani Singida.

SOMA NA HII  STARS: TUPO TAYARI KUIMALIZA BURUNDI