Home Habari za michezo SIMBA, YANGA WATULIZA VICHWA KIMATAIFA…… ISHU HII NDIO UMIZA KICHWA

SIMBA, YANGA WATULIZA VICHWA KIMATAIFA…… ISHU HII NDIO UMIZA KICHWA

Mabosi wa klabu kongwe nchini, Simba na Yanga wanaendelea kukuna vichwa juu ya kuchagua viwanja gani vya kutumika kwenye mechi zao za mwisho za nyumbani za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya Serikali kuupiga ‘stop’ Uwanja wa Benjamin Mkapa waliokuwa wakiutumia awali.

Simba na Yanga zimekuwa zikiutumia uwanja huo kwa mechi za nyumbani, lakini juzi serikali ilitangaza kuufunga sambamba na ule wa Uhuru ili kupisha ukarabati hadi Oktoba mwakani na kuzilazimisha timu hizo na nyingine zilizokuwa zikitumia viwanja hivyo kutafuta maeneo mengine ya kujidai.

Kazi kubwa inaonekana ipo kwa Simba kwani katika Ligi Kuu ilikuwa ikiutumia Uhuru sawa na KMC na klabu za Ligi ya Champioship, lakini kwa mechi za CAF iliutumia Benjamin Mkapa kama ilivyo kwa Yanga na Al Hilal ya Sudan.

Kulikuwa na hisia huenda mechi za kimataifa za timu hizo zikahamia Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambao unatarajiwa kuzinduliwa rasmi Desemba 27 baada ya kufanyiwa ukarabati na kampuni kutoka Uturuki, lakini kuwa kwake na nyasi bandia, zinauondolewa sifa ya kutumika kwa mechi za hizo makundi kwa mujibu kanuni za CAF.

Wizara imeamua kuvifunga viwanja hivyo baada ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kuufungia Uwanja wa Uhuru kutotumiwa katika michezo inayoendelea ya Ligi Kuu kutokana na kutokidhi vigezo vya kikanuni vya kutumika katika michezo hiyo.

Mara baada ya kutoka kwa uamuzi huo, inaelezwa viongozi wa klabu hizo, wameanza mchakato wa kutafuta masikani zao mpya ambazo watazitumia kwa michezo ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku upande wa ligi, klabu zilizokuwa zikicheza Uhuru zina chaguo la kwenda Azam Complex inayoutumia Yanga, Azam FC na JKT Tanzania ama uwanja mwingine wa karibu.

Ofisa Habari wa Simba, Ahmed Ally alisema bado wapo na muda wa kufanya machaguo ya uwanja gani ambao watautumia.

“Mbele yetu tuna miezi miwili hivyo tuna muda wa kutosha wa kuangalia uwanjani gani ambao tunaweza kuutumia kwa ajili ya mechi zetu za ligi na hata Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo Wanasimba wanatakiwa kuwa watulivu kila kitu kitaenda sawa sawa na tutawatangazia rasmi mchakato ukikamilika,” alisema Ahmed, huku Ally Kamwe wa Yanga alisema muda mwafaka ukifika watatangaza rasmi lakini alikiri kuwa suala hilo lipo kwa uongozi na wanalitafutia ufumbuzi wake haraka iwezekanavyo.

Hata hivyo, habari ambazo hazijathibitishwa ni kwamba huenda mechi hizo za vigogo na hata Al Hilal zitapigwa Benjamin Mkapa kama ilivyokuwa awali, licha ya tangazo hilo la serikali, ingawa kwa Uwanja wa Uhuru ni ngumu kutumika kwa mechi za Ligi kutokana na sababu mbalimbali licha ya kufungiwa na TFF na serikali.

Juzi mapema, TFF ilitangaza kuufungia Uwanja wa Uhuru kwa kukosa sifa, kisha serikali kupitia Kitendo cha Habari cha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ilitoa tamko la kuvifunga viwanja vyote viwili.

SOMA NA HII  SIMBA WATOA NENO KUHUSU ISHU YA DAVID MOLINGA