Licha ya kiungo Mshambuliaji wa Simba SC, Clatous Chama kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu, Uongozi wa Klabu hiyo umeweka bayana kuwa hakuna mpango wowote wa kutaka kumuachia, kutokana na mkataba wake ndani ya timu hiyo.
Kiungo huyo kutoka nchini Zambia na Uongozi wa Simba SC wamekuwa kwenye mvutano ambao umekuwa ukitajwa kama makosa ya utovu wa nidhamu wa mchezaji huyo ambao umepelekea kusimamishwa kwake.
Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC, Ahmed Ally amesema kuwa licha ya kiungo hiyo kusimamishwa lakini hawana mpango wowote wa kumuachia kutokana na kuendelea na progamu za benchi la ufundi.
Ahmed amesema kuwa mbali na kupewa adhabu ya kusimamishwa na kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu lakini kiungo huyo anaendelea na programu za mazoezi aliyopewa na benchi la ufundi pamoja na kulipwa stahiki zake ikiwemo mshahara wake.
“Chama amepata tuhuma za utovu wa nidhamu na amepelekwa katika kamati ya nidhamu, hatuna nia ya kuachana naye, hatuwezi kuachana na mchezaji ambaye bado ana mkataba na hatujapata hitimisho la adhabu yake ya utovu wa nidhamu.
“Kwetu ni mchezaji muhimu kama ilivyo kwa wachezaji wengine na hata ikifikia hatua ya kuamua kuachana naye basi ataondoka Simba SC kwa heshima zote,” amesema Ahmed.
Tunahitaji mabadiliko makubwa ndani ya kikosi cha timu yetu ya simba