Home Habari za michezo KAZE MAMBO MENGINE YANUKIA IHEFU

KAZE MAMBO MENGINE YANUKIA IHEFU

Habari za Michezo Bongo

Baada ya kuachana na Kocha kutoka nchini Uganda Moses Basena, uongozi wa Klabu ya Ihefu FC huenda ukamtwaa aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Young Africans na Namungo FC, Mrundi, Cedric Kaze.

Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zimeeleza kuwa Kaze anaonekana kuwa chaguo la pili baada ya ugumu wa kumpata Juma Mgunda ambaye ndiye alikuwa chaguo la kwanza la klabu hiyo.

Chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo kimeeleza kuwa ugumu wa kumpata Mgunda unatokana na kwamba ana mkataba na Klabu ya Simba SC na kwa sasa ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Simba, akihusika zaidi na timu za vijana chini ya miaka 17, miaka 20 na Simba Queens.

Juzi kocha huyo alionekana kwenye benchi la Simba Queens iliyokuwa ikicheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga Princess akisaidiana na Mussa Hassan Mgosi.

“Kulikuwa na mazungumzo na Klabu ya Simba SC, lakini kuna ugumu, hivyo ili tusikae muda mrefu bila ya kocha, tumeamua kugeukia upande wa pili na tunaona kocha mwenye hadhi ambaye anaweza kuitoa Ihefu FC hapa ilipo na kuipeleka mbele, lakini kama nilivyosema huu bado ni mchakato wa ndani, haujawekwa nje mpaka sasa, ila kila kitu kikishakuwa tayari tutawajuza ni nani kocha mpya wa klabu yetu.” Kimeeleza chanzo cha habari hizi

Basena aliyeichukua timu hiyo kutoka kwa Zuberi Katwila, alioneshwa mlango wa kutokea baada ya suluhu dhidi ya Prisons, mechi iliyochezwa Desemba 4, mwaka huu, katika Uwanja wa Highland Estates, Mbarali, akiiongoza timu hiyo kwenye michezo saba bila kushinda hata mmoja, akipoteza mitatu na sare nne.

Hata hivyo, kabla hata haijapata kocha, Ihefu ilishinda mechi yake ya Ligi Kuu nyumbani, ljumaa iliyopita kwa kuifunga Tabora United mabao 2-1.

Ulikuwa ni ushindi wa kwanza kwa timu hiyo tangu ilipoifunga Young Africans mabao 2-1, Oktoba 4, mwaka huu kwenye uwanja huo, na mpaka sasa ina pointi 13 kwa michezo 13 iliyocheza.

SOMA NA HII  KWA MARA YA KWANZA FEI TOTO AFUNGUKA KUHUSU ISHU YA KULA UGALI NA SUKARI AKIWA YANGA