Home Habari za michezo MTIBWA SUGAR WAJA NA MIKAKATI HII KUOKOA JAHAZI

MTIBWA SUGAR WAJA NA MIKAKATI HII KUOKOA JAHAZI

Mkuu wa Benchi la Ufundi la Mtibwa Sugar Zuberi Katwila, amepanga kuja na mikakati miwili tofauti ambayo itakirejesha katika ubora kikosi chake ambacho kwa sasa kinaburuza mkiwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Mkakati wa Kwanza kwa kocha huyo mzawa ni ‘kufufukia’ kwenye mechi mbili za ligi zijazo dhidi ya Namungo, Desemba 7, kisha Young Africans Desemba l6, zote ikiwa ugenini.

Mtibwa inahitaji alama nne kwenye mechi mbili hizo ili iweze kurejesha morali na ari ya upambanaji kikosini.

Mkakati wapili kwa Katwila ni usajili wa Dirisha Dogo unaotarajiwa kufunguliwa Desemba l6, mwaka huu.

Kocha huyo mwenye uzoefu na Ligi Kuu anaamini kupitia Dirisha hilo la usajili ataongeza nyota wapya wasiopungua wanne kikosini, ambao wataungana na waliopo kuhakikisha timu inakaa eneo salama kwenye msimamo.

“Hatuna hali nzuri, kwa sasa tunaangalia namna gani ya kupata alama kwenye mechi mbili zijazo. Tunajua ni mechi ngumu kutokana na wapinzani tutakaokutana nao lakini tuna imani tunaweza kufanya vizuri na tunaendelea kujipanga,” amesema Katwila

“Baada ya hapo nadhani tutageukia usajili. Lazima tuongeze watu kwenye baadhi ya maeneo ambayo tumeona kuna uhitaji wa kufanya hivyo, kisha tutaendelea kujenga timu taratibu kuhakikisha tunamaliza ligi tukiwa sehemu salama.” amesema Katwila

Katwila alitua Mtibwa mwezi Oktoba akichukua nafasi ya Habib Kondo aliyefungashiwa virago na tangu kurejea kwake kwa walima miwa hao ameiongoza timu katika mechi tano, ikishinda moja na kupoteza nne mfululizo.

Mtibwa hadi sasa imecheza mechi 11, ikishinda moja na kutoa sare mbili huku ikipokea vichapo nane na kuwa na alama tano pekee.

SOMA NA HII  UTATA KWISHA, BOSI WA WAAMUZI AVUNJA UKIMYA