Home Habari za michezo SIMBA vs WYDAD NI KISASI NA HESHIMA MASTAA WATOA TAMKO

SIMBA vs WYDAD NI KISASI NA HESHIMA MASTAA WATOA TAMKO

Habari za Simba

Mashabiki wa Simba, wanasikilizia chama lao likishuka uwanjani usiku wa leo kwa mara ya pili chini ya kocha mkuu Abdelhak Benchikha ugenini dhidi ya Wydad Casablanca ya Morocco kwenye mechi ya tatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku mastaa wa timu hiyo wakiwatoa hofu kwa kuwaambia ‘msiwaze sana, hawa wetu’.

Simba itashuka kwenye Uwanja wa Marrakech, Morocco katika pambano la Kundi B ikiwa na kumbukumbu ya kupata sare mbili mfululizo za mechi za awali, lakini mastaa wa Simba wameapa kushinda mechi ya leo ili kujiweka pazuri na kuwarudishia furaha mashabiki wa timu hiyo.

Simba imepania kurudia kile kilichofanywa na Jwaneng Galaxy wiki mbili zilizopita kwa kuibuka na ushindi ugenini dhidi ya Wydad wakati wakiwashukia wenyeji wao hao kuanzia saa 4:00 usiku.

Ushindi wa leo ndio unaoweza kuweka hai matumaini ya Simba kutinga robo fainali lakini kinyume na hapo inaweza kujikuta katika nafasi finyu zaidi.

Mchezo huo unakutanisha timu mbili ambazo hadi sasa hazijaonja ladha ya ushindi katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hivyo pengine leo itakuwa mwisho wa nuksi kwa mojawapo au zikaendeleza jinamizi ambalo zimekutana nalo kwenye raundi mbili za mwanzo.

Wydad haijapata pointi yoyote katika mechi mbili za mwanzo ikianza kwa kupoteza kwa bao 1-0 nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy na ikafungwa kwa matokeo kama hayo katika mechi ya pili dhidi ya Asec Mimosas ugenini.

Simba yenyewe katika mechi mbili za mwanzo imevuna pointi mbili, ikitoka sare ya bao 1-1 na Asec Mimosas nyumbani kisha ikalazimisha sare tasa ugenini na Jwaneng Galaxy.

MECHI YA HESHIMA

Timu zote zimekuwa na mwenendo usioridhisha katika mechi za mashindano tofauti ambazo zimecheza siku za hivi karibuni na uthibitisho wa hilo unaweza kujidhihirisha katika mechi tano zilizopita ambazo kila moja imecheza ambapo zimeangusha idadi ya pointi kulinganisha na zile zilizotegemea kupata.

Wydad katika mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, imepata ushindi mara moja tu huku ikipoteza mechi nne, ikifunga mabao manne na yenyewe imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nane.

Simba nayo kwenye mechi tano za mashindano tofauti iliyocheza kabla ya mechi ya leo, imepata ushindi mara moja, imetoka sare tatu na kupoteza mechi moja wakati huo ikifunga mabao matano na imeruhusu mabao manane.

KISASI TU

Simba inaingia uwanjani na kumbukumbu mbili zisizovutia dhidi ya Wydad ambazo zinailazimisha kuibuka na ushindi leo ili imalize kisasi chake dhidi ya miamba hiyo ya Morocco.

Kwanza ni kutolewa katika hatua ya mwisho ya mtoano ya kuwania kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2011 ilipochapwa mabao 3-0 ambapo mechi hiyo ililazimika kuchezwa moja nchini Misri baada ya TP Mazembe kuondolewa mashindanoni kwa kumchezesha mchezaji ambaye hakuwa halali kucheza dhidi ya Simba katika raundi ya kwanza.

Ya pili ni msimu uliopita ambao Simba ilitolewa kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika hatua ya robo fainali baada ya mechi mbili baina ya timu hizo kumalizika kwa sare ya bao 1-1, Simba ikishinda bao 1-0 nyumbani na ikaenda kufungwa 1-0 ugenini, matokeo yaliyolazimisha mikwaju ya penalti kutumika ili kupata mshindi.

UPEPO TOFAUTI

Wakati Simba imekuwa ni timu ya kawaida inapocheza ugenini kwenye mechi za kimataifa, Wydad yenyewe ni moto wa kuotea mbali pale inapocheza nyumbani na ushahidi wa hilo ni mechi 10 zilizopita za mashindano ya klabu Afrika kwa kila timu.

Katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya kimataifa ambazo ilikuwa ugenini, Simba imeibuka na ushindi mara tatu, kutoka sare tatu na kupoteza michezo minne, ikifunga mabao tisa na yenyewe imefungwa mabao 10.

Kwa upande wa Wydad, yenyewe katika mechi 10 zilizopita za mashindano ya Afrika ambazo imecheza nyumbani, imepata ushindi mara saba, kupoteza moja na kutoka sare mbili ambapo imeziona nyavu mara 15 na zake zimetikiswa mara tatu.

CHUNGA HAWA

Simba inapaswa kumnyima uhuru kwa muda mwingi wa mchezo, nahodha wa Wydad, Yahya Jebrane anayecheza nafasi ya kiungo wa ulinzi.

Jebrane ni fundi wa kuilinda safu ya ulinzi kwa kuziba nafasi ambazo wapinzani wanaweza kuzitumia kupeleka kwa washambuliaji wao lakini pia ni hodari wa kuisukuma timu mbele na kupiga pasi za mwisho.

Mwingine ni beki wa kushoto, Yahia Attiyat Allah ambaye ana uwezo mkubwa wa kushambulia kupitia krosi na pia kuzuia pindi inaposhambuliwa.

Kwa upande wa Wydad hapana shaka watapaswa kumchunga zaidi Kibu Denis kwani ndio amekuwa tegemeo la Simba katika kushambulia kutokana na pumzi na nguvu aliyonayo lakini pia ni mchezaji ambaye amekuwa akitumika katika mpango wa kukaba kuanzia mstari wa mbele.

KIKOSI KAZI

Kikosi cha Simba leo kinaweza kuwa na mabadiliko machache kulinganisha na kile kilichoanza katika mchezo uliopita wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galxy ugenini huko Botswana.

Willy Onana anaweza kuanzia benchi kumpisha Clatous Chama lakini nafasi nyingine zinaweza kuwa na wachezaji walewale.

Leo kikosi cha Simba kinaweza kuwa na Ayoub Lakred, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Enock Inonga, Che Malone Fondoh, Sadio Kanoute, Kibu Denis, Fabrice Ngoma, Jean Baleke, Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

MASTAA WALA KIAPO

Baadhi ya nyota wa Simba wamewaapia mashabiki wa wapenzi wa timu hiyo kuwa, leo lazima kieleweke na kwamba wasilale ili wawaangalie wakati wanakipiga, huku wao wakipiga dua njema mambo yawe mepesi.

Kiungo wa Simba, Fabrice Ngoma alisema kuwa wamejipanga na wapo tayari kwa mechi hiyo ya leo.

“Hadi sasa tumejiandaa vizuri, wachezaji wako vizuri na tuko katika hamasa nzuri na nidhamu ya kujiandaa kuhusu mchezo. Ni faraja kwangu kurudi hapa ambako niliacha historia miaka mitatu iliyopita. Sisi kama Simba tumekuja hapa kutafuta alama tatu hivyo kwa upande wangu sioni kama mechi itakuwa ni ngumu au kubwa sana isipokuwa tunatakiwa kumheshimu mpinzani wetu na tumekuja hapa kwa matarajio ya pointi tatu na kwa uwezo wa Mungu tutazipata,” alisema Ngoma, huku nahodha msaidizi, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ akisema wamepania kutoka na ushindi licha ya ugumu wa wenyeji wakiwa nyumbani.

Tshabalala alikuwapo kwenye kikosi kilichotolewa kwa matuta na alisema leo ni kazi moja tu.

“Tumejiandaa vyema na makocha wameshaifanya kazi yao, sasa ni zamu yetu kuwapa raha mashabiki wa Simba, hautakuwa mchezo mwepesi, lakini hii ni vita ambayo lazima tushinde kwa ajili ya kuiweka timu sehemu salama katika safari ya kuvuka makundi kwenye hatua nyingine kwa msimu huu,” alisema Tshabalala beki wa kushoto wa timu hiyo.

Hiyo ni mechi ya nne kwa timu hizo kukutana tangu 2011 ambapo Wydad imeshinda mechi mbili na kupoteza moja katika michezo mitatu ya awali na baada ya pambano hilo zitarudiana wikiendi ijayo jijini Dar es Salaam.

Timu hizo zilikuwa kwenye mechi maalum ya play-off ya kuwania kufuzu makundi 2011 na Simba kulala 3-0 kabla ya mwaka jana kukutana Dar katika robo fainali na Simba kushinda 1-0 na Wydad kulipa kisasi mechi ya marudiano iliyoamuliwa na penalti na Mnyama kung’oka.

SOMA NA HII  KASSIM DEWJI AWEKA HADHARANI WALICHOIFANYA ZAMALEK CAF 2003