Home Habari za michezo WAKATI AZAM FC WAKIWA JUU MAWINGUNI….VIGONGO VYA SIMBA NA YANGA HIVI HAPA…

WAKATI AZAM FC WAKIWA JUU MAWINGUNI….VIGONGO VYA SIMBA NA YANGA HIVI HAPA…

Habari za Michezo

Wakati Azam FC ikiongoza Ligi Kuu Bara kwa tofauti ya pointi nne dhidi ya mabingwa watetezi Yanga, vigogo Simba na Yanga wamerudi kuchanga karata baada ya Ligi ya Mabingwa Afrika mambo kuwaendea kombo kwenye mechi tatu za mwanzo za hatua ya makundi sasa ni vita ya mechi sita mwezi Desemba.

Azam FC inaongoza ligi baada ya kucheza mechi 11 na kukusanya pointi 25 ikiiacha Yanga kwa pointi nne ambayo imecheza mechi tisa ikikusanya pointi 24, huku Simba ikiwa nafasi ya tatu na pointi 19 baada ya kucheza mechi nane.

Vigogo hao licha ya kuwa nyuma kwa mechi hizo bado wanaendelea kuwa katika tatu bora kwenye msimamo mwezi huu, lakini wana kazi kubwa ya kufanya kutokana na ratiba kuwa na mechi nyingi Disemba.

Hizi hapa mechi 10 za mwezi huu kwa vigogo Simba na Yanga ambazo kati ya hizo mbili tu ndizo za Ligi ya Mabingwa huku nne kwa kila timu zikiwa za Ligi Kuu Bara.

MECHI TANO SIMBA

Simba ndio timu iliyocheza mechi chache zaidi hadi sasa ikicheza mechi tisa na kufanikiwa kukusanya pointi 19 zilizoiweka katika nafasi ya tatu kwenye msimamo, Ijumaa inarudi ikianza na Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi utakaopigwa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Baada ya mchezo huo ambao utaamua namna itakavyosajili dirisha dogo ambalo linafunguliwa pia Ijumaa, Simba itarudi kimataifa kuwakabili Wydad ambao wametoka kuifunga bao 1-0 ugenini, lakini sasa wanakaribishwa Dar.

Mechi nyingine za ligi upande wa Simba mwezi huu ni dhidi ya KMC mchezo ambao itakuwa ugenini kisha itaifuata Mashujaa na kumaliza na Tabora United Desemba 29.

MECHI ZA YANGA
Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga watakuwa na kibarua kigumu cha kuhakikisha wanaiteremsha Azam FC kileleni kutokana na kuimarika na kushinda mechi zake mfululizo. Yanga wapo nyuma mechi mbili wakizidiwa pointi nne.

Wao watawaalika Mtibwa Sugar mchezo utakaopigwa Jumamosi (Desemba 16) Chamazi nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam. Baada ya hapo watageukia Ligi ya Mabigwa Afrika Jumatano kwa kuikaribisha Medeama ya Ghana ambayo mchezo wa kwanza ilitoka nayo sare ya bao 1-1 ugenini.

Mechi nyingine tatu za ligi ambazo zimepangwa kupigwa Desemba ni dhidi ya Tabora United ugenini (Desemba 22), Kagera Sugar ugenini (Desemba 22) na itafunga na Mashujaa nyumbani Desemba 29.

WASIKIE MAKOCHA
Akizungumzia michezo inayowahusu, kocha wa Yanga, Miguel Gamondi anasema ni ratiba ngumu, lakini watapambana kuhakikisha wanafikia lengo la kutetea taji huku akikiri kuwa haitakuwa rahisi kutokana na ushindani. “Tuna mechi nne za ligi mwezi Desemba mbili nyumbani, mbili ugenini ratiba sio rafiki, lakini tayari imepangwa. Tunatakiwa kuifanyia kazi. Wachezaji wangu wanatambua umuhimu wa michezo hiyo nawaamini. Lengo ni moja tu kurudi kwenye ushindani kwa kupata matokeo ya ushindi.

“Kila timu imekuwa ikisaka pointi tatu muhimu hasa kipindi hiki ambacho ni muhimu kutengeneza mazingira ya kujiweka kwenye nafasi nzuri kabla ya mzunguko wa lala salama hivyo tunatarajia ushindani na tunatakiwa kujipanga ili kuweza kufikia malengo,” anasema Gamondi.

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anasema ratiba inampa mwanga wa kikosi huku akilia na washambuliaji kuwa hafurahishwi na uchezaji wao. “Ratiba imepangwa ili ifanyiwe kazi na wachezaji wangu wanatambua umuhimu wa michezo iliyo mbele yetu kwa upande wangu naendelea kuwasoma wachezaji kubaini shida ilipo na ubora wao.

“Hadi sasa sifurahishi na eneo la ushambuliaji nina kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha eneo hilo linakuwa bora na linanipa matokeo kwenye michezo hiyo ambayo inahitaji pointi ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutwaa taji,” anasema.

SOMA NA HII  NI KWELI BABACAR SARR KATATUA SHIDA YA KIUNGO SIMBA?....UKWELI WA KUJUA HUU HAPA...