KIUNGO mpya wa Simba, Babacar Sarr aliyesajiliwa hivi karibuni ameibua vita mpya ya namba kikosini, huku akiulazimisha uongozi wa klabu hiyo kumchomoa mtu mmoja kati ya nyota wa kigeni ili kumpa nafasi ya kufanya kazi kwa ufanisi.
Sarr, nyota wa zamani wa US Monastir ya Tunisia amesajiliwa kwa dili la miaka miwili akiwa mchezaji huru na kuifanya Simba kufikisha wachezaji wa kigeni 13 wakiwamo Kramo Aubin, Clatous Chama, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, Saido Ntibazonkiza, Moses Phiri, Ayoub Lakred, Willy Onana, Fondoh Che Malone, Jean Baleke, Henock Inonga na Luis Miquissone.
Japo jina la Kramo, Phiri na Chama aliye katika mzozo na klabu hiyo kabla ya kwenda timu ya taifa ya Zambia itakayoshiriki fainali za Afcon 2003, mmojawapo anatajwa kukatwa ili kumpisha Sarr.
Kramo aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu tangu asajiliwe anangaliwa kwa sasa, huku Chama ni kutokuwa chaguo la kocha Abdelhak Benchikha, mbali na utovu wa nidhamu uliomponza kusimamishwa kwa muda usiojulikana ilhali Phiri ni vile alishaandika barua ya kutaka kuondoka klabuni.
Hivyo ujio wake unaulazimisha uongozi kupitisha panga kwa nyota mmoja wa kigeni ili kuingiza jina lake tayati kwa mechi za Ligi Kuu Bara, Kombe la ASFC na hata Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini akiibua vita mpya ya mastaa wanaocheza nafasi ya kiungo mkabaji anayocheza Msenegali huyo.
Sarr anaifanya safu ya kiungo ya Simba kuwa na watu wanne watakaokuwa na kazi ya kugombea namba ya kuanza kikosi cha kwanza akiwamo Mzamiru Yassin, Ngoma na Kanoute, huku Simba ikiwa imemsajili pia kiungo mwingine Saleh Masoud Karabaka anayemudu kucheza kiungo cha juu.
Karabaka anaweza kucheza kiungo mshambuliaji au winga wa kulia na kushoto na kwa mujibu wa kocha aliyekuwa anamnoa amethibitisha mchezaji huyo anafiti zaidi namba 11, mbali na Ladack Chasambi anayeweza kutokea pembeni winga ambaye pia amesainiwa na klabu hiyo akitokea Mtibwa Sugar hivyo Simba wameziungatia zaidi maeneo mawili – kiungo na winga.
Ukiachana na wawili hao wanaomudu kucheza nafasi nyingi uwanjani mtihani mkubwa ni eneo la kiungo mkabaji ambalo lina wachezaji hao watatu na wapo tayari kwa vita ya kugombea nafasi tatu za kuanza katika kiungo.
Kusajiliwa kwa Sarr kumeongeza idadi ya nyota wa n kiungo katika kikosi hicho na ni wazi kwamba kocha Abdelhak Benchikha atapasuka kichwa kuamua nani aanze na gumu zaidi ya yote itakuwa ni kuhakikisha kila mmoja ana furaha.
Hawa hapa ni wachezaji wanne watakaopasuana kichwa kuwania nafasi za kuanza katika kikosi cha kwanza msimu huu ambao tayari umeanza Simba wakiwa nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 10 na kukusanya pointi 23 katika msimamo.
MZAMIRU YASSIN
Kati ya wachezaji hao wanne, mzawa ni mmoja tu – yaani Mzamiru Yassin ambaye licha ya kuletewa nyota kutoka nje amekuwa akipenya kupata nafasi ya kucheza ukiwa ni msimu wa nne sasa upande wake.
Mzamiru bado ni mmoja wa wachezaji wanaoijua staili ya timu hiyo nje ndani, na ndiye mtu anayechukuliwa mzawa ambaye atakuwa msaada kwa wageni wanaotua kikosini.
SADIO KANOUTE
Huyu alikuwa mchezaji tegemeo ndani ya kikosi cha Simba misimu miwili ya mwanzo tangu atue Simba licha ya sasa kiwango chake kushuka na kuingia na kutoka kikosini.
Licha ya kuwa na kasoro za kuongoza kwa kuonyeshwa kadi kutokana na kucheza rafu nyingi, Kanoute ni miongoni mwa wachezaji walio na msaada mkubwa wa ulinzi.
FABRICE NGOMA
Ni kiungo ambaye amesajiliwa msimu huu na tayari ameonyesha mchango mkubwa ndani ya kikosi hicho licha ya kutajwa kuwa ni mzuri akicheza juu kama kiungo mshambuliaji.
Huenda akasogezwa acheze mbele kiungo namba 10 sehemu ambayo imekuwa bora zaidi chini ya Clatous Chama ambaye ameingia kwenye mgogoro na timu yake kwa madai ya utovu wa nidhamu.
WADAU WANASEMAJE?
Nyota wa zamani wa Tanzania Prisons, Yona Ndabila amesema ujio wa Babacar ndani ya Simba utaongeza chachu ya uimara eneo la ulinzi kwa sababu timu hiyo ilikuwa inakosa mchezaji wa aina hiyo.
“Ni kweli wana Kanoute, Ngoma na Mzamiru, lakini hawakuwa na kiungo ambaye anakabia chini kama ilivyo kwa Khalid Aucho wa Yanga ambaye huoni akipanda juu kama ilivyo kwa hao wengine,” alisema.
“Ni usajili sahihi kilichobaki kwake ni kuona namna gani atafanya kazi yake kwa ubora kama anavyotarajiwa na wengi. Endapo atafanya hivyo atapunguza makosa mengi eneo hilo.”
Akiwaelezea Ngoma na Kanoute, alisema mmoja ni mzuri katika kusambaza mipira na mwingine ni bora kwenye ukabaji, lakini sio mtulivu kwenye eneo lake na amekuwa muumini wa kupanda na kuchelewa kurudi kusaidia safu ya ulinzi.
Alisema Simba ilikuwa na shida eneo hilo na endapo Babacar ni kiungo mkabaji asilia, basi imetibu tatizo licha ya kuwa itakuwa na sehemu nyingine ya kufanyia marekebisho kama eneo la ushambuliaji.
Kocha wa zamani wa Yanga, Geita na Tanzania Prisons ambaye sasa hana timu, Fredy Felix ‘Minziro’ alisema usajili unafanyika kulingana na mahitaji ya kocha, hivyo kama Simba imekamilisha usajili basi kocha ndiye kahitaji mchezaji huyo kutokana na kushindwa kuridhishwa na waliopo.
“Sio rahisi kuzungumzia sajili za timu pinzani ambazo zina makocha ambao wanazifundisha usajili mara nyingi ni mapendekezo ya mwalimu hata kukiwa na wachezaji 10 kila mmoja anakuwa na umuhimu wake na inawezekana wote wakashindwa kufanya kile mwalimu anakitaka haimzuii kusajili,” alisema.