Home Habari za michezo HAWA HAPA MAKOCHA WANOSUKUMA NDINGA ZA MAANA LIGI KUU…

HAWA HAPA MAKOCHA WANOSUKUMA NDINGA ZA MAANA LIGI KUU…

Habari za Michezo leo

KUNA maisha ya makocha nje ya mabasi ya timu zao. Hawa jamaa wanasukuma ndinga kali. Swali la mashabiki kwenye mitandao ni je kocha wenu anayo kali kama wetu? Kila mmoja anatambia gari ya mwenzake.

Katika makocha 16 kuna baadhi ya makocha bado wapo chini na wanaendesha magari ya gharama za kawaida pengine hata chini ya wachezaji wao kutokana na uchumi na uhalisia wa klabu zao.

Kwa mujibu wa wachambuzi, suala la kocha wa klabu kuwa na gari binafsi ni muhimu kwani licha ya kumuongezea hadhi pia inampa faragha ya kujadili mambo yake na wasaidizi wake.

Lakini inatoa uhuru pia kwa wachezaji kujadili (ikiwemo kumsema kocha) mambo yao kwa uhuru na kupunguza presha baada ya mazoezi au mechi wakiwa njiani. Tofauti na wakiwa na kocha ambapo baadhi wamekuwa na aibu ya kukosoa au kuwa huru.

Iko hivi. Kila kocha anapoingia mkataba na klabu huwa na majadiliano juu ya mambo binafsi yakiwemo malipo, nyumba na hata usafiri kulingana na uchumi wa timu anayoingia nayo makubaliano.

Kwenye Ligi Kuu Bara maisha nayo yametofautiana, hivyo makocha 16 wamekuwa wanatofautiana aina ya usafiri wanaoutumia nje ya basi la timu ambalo hutumia kwa pamoja wakati wa safari za kwenda uwanjani au hata mazoezini wakati mwingine. Twende sawa:

Benchikha (Mercedes Benz)

Kocha wa Simba, Abdelhak Benchikha anatumia gari iliyokuwa inatumiwa na mtangulizi wake Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aina ya Mercedes Benz Kompressor toleo namba C 200 nyeupe ya mwaka 2010 akiendeshwa na dereva aliyekuwa anamwendesha Mbrazili.

Mercedes ina heshima kubwa kutokana na ukubwa wa jina na umaridadi wake. Kwa sasa sokoni inauzwa Sh24.5 milioni.

Gamondi (Toyota Vanguard)

Kocha wa mabingwa watetezi – Yanga, Miguel Gamondi ni kama Benchikha anatumia gari iliyokuja mara ya kwanza na kutumiwa na mtangulizi wake Nasreddine Nabi. Gamondi anatumia gari aina ya Toyota Vanguard nyeusi.

Gari hiyo toleo la mwaka 2010 bei yake kwa sasa inacheza kati ya Sh29 na milioni 31. Gamondi usipomuona kwenye basi la timu yake utamuona akiwa humo akiendesha mwenyewe. Amekwishavielewa vichochoro vingi vya Jiji la Dar.

Dabo (Rav 4 limited)

Pale Azam FC kocha wa timu hiyo kinara wa ligi, Youssoupha Dabo ‘Ustaadh’ vilevile anatumia gari ambayo awali ilikuwa inatumiwa na George Lwandamina aina ya Rav 4 Limited nyeusi ya mwaka 2015.

Lwandamina hakuitumia sana kwani ilipofika tu kibarua chake kiliota mbawa na makocha wengine waliomfuatia walibadilishiwa ndinga, lakini sasa ipo kwa Dabo ikiwa na thamani ya kati ya Sh27 milioni hadi milioni 32.

Abdihamid Moallin (Kluger)

KMC upande wa kocha wao, Abdihamid Moalin amepewa gari aina ya Toyota Kluger kutembelea kwenye misele yake binafsi pamoja na kwenda nayo mazoezini.

Kluger ni gari nzuri ambapo aliyo nayo ni toleo la mwaka 2001. Kule sokoni inapatikana kuanzia Sh27 milioni na kuendelea.

Goran, Malale (Toyota IST)

Hawa jamaa hawana mambo mengi pengine ni kutokana na bajeti ya klabu zao. Kocha Malale Hamsini wa JKT Tanzania na Goran Kopunovic wa Tabora United ‘wanaishi’ kwenye gari aina ya Toyota IST zote toleo la mwaka 2005 tofauti ni rangi za magari yao.

Tuanze na Malale. Gari yake hiyo nyeupe sio kwamba ni mali ya klabu, bali mali yake baada ya mkataba wake kumhudumia mambo mengine, huku Goran akitumia IST ya rangi ya shaba ambayo ni mali ya mmoja wa mabosi wa juu wa klabu hiyo.

Maxime, Baraza, Baresi (Toyota Harrier)

Wapo makocha watatu ambao wamejificha kwenye gari aina ya Toyota Harrier ambao ni Mecky Maxime wa Ihefu, Francis Baraza wa Dodoma Jiji na Abdallah Mohamed ‘Baresi’ wa Mashujaa FC.

Baresi kwa upande wake gari hiyo ni yake kama ambavyo Malale ilivyo, ingawa amekuwa akiitumia kwenye shughuli za timu hiyo na hivi sasa amekuja nayo jijini Dar es Salaam wakati timu yake ikiendelea na maandalizi ya Ligi Kuu Bara.

Zahera (Alphard)

Papaa wa Namungo, Mwinyi Zahera atapewa gari aliyokuwa akiitumia aliyekuwa kocha wa timu hiyo, Cedrick Kaze aina ya Toyota Alphard toleo la mwaka 2006.

Ingawa bado Zahera hajakabidhiwa gari hiyo akiwa yupo jijini Dar es Salaam na kikosi cha timu hiyo akiendelea na maandalizi, lakini akirejea Lindi huenda wakampatia ambayo thamani yake sokoni ni Sh24 milioni.

Katwila, Hamad, Ouma (hawana magari)

Mtibwa Sugar, kocha wao Zuber Katwila hajapewa gari na kama ana mizunguko yake anatumia usafiri wa kulipia kufanya mambo yake huku akiwa na kikosi hicho hutumia basi la timu.

Naye Kocha wa Prisons, Hamad Ally hana usafiri binafsi anapokuwa kwenye mizunguko binafsi ambapo wakati mwingine hupewa lifti katika magari ya viongozi wa timu au kutumia usafiri wa basi la klabu.

Hali hiyo pia anayo kocha wa Coastal Union ya Tanga, David Ouma ambaye hajapewa gari ingawa mtangulizi wake Mwinyi Zahera alikuwa akitumia Toyota Corolla.

Kitambi (Usafiri wa serikali)

Kocha wa Geita Gold, Denis Kitambi na makocha wengine waliomtangulia hawakuwa na gari au magari maalumu ya kutembelea na endapo kocha huyo anahitaji usafiri, basi anapewa gari ya Halmashauri ya Mji wa Geita kumfikisha anapotaka kwenda na kurudishwa.

Kagera Sugar (Harrier inamsubiri)

Kagera Sugar hawana kocha mpya, lakini kocha waliyeachana naye Maxime na hata Baraza walikuwa wanatumia Harrier kama ambazo wanatumia makocha hao katika klabu waliko.

Kagera bado inasaka kocha mpya ambapo atakapopatikana anaweza kukabidhiwa gari kama hiyo ambayo iliachwa na watangulizi wake.

Credit:- Mwanaspoti

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUONEKANA NA BARBARA...MANULA AIKANA SIMBA SC....ADAI HAJASAINI MKATABA MPYA NA HANA MKATABA NAO...