TAIFA Stars imeondoshwa kwenye fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2023 zinazoendelea kule Ivory Coast. Imeishia katika hatua ya makundi. Imeshika mkia katika kundi lake. Kuna cha kushangaza? Hakuna. Ilitarajiwa hivyo.
Stars ingefanya vizuri kwenye Afcon ndio ingekuwa habari ya kushangaza. Vinginevyo, mengine ni ya kawaida sana.
Miongoni mwa timu ambazo zilipewa nafasi ndogo ya kufanya vizuri katika fainali hizo ilikuwa Tanzania. Kwanini? Subiri nitakueleza.
Hii ilikuwa ni mara ya tatu kwa Tanzania kushiriki fainali hizo katika historia. Ilikwenda Nigeria mwaka 1980 na Misri mwaka 2019. Kisha ikarejea tena mwaka huu. Tena kwa kufuzu kwa kuungaunga.
Katika fainali hizo mbili za mwanzo haikufanya kitu chochote cha maana. Ilipoteza michezo mitano na kutoka sare mmoja tu kule Lagos, Nigeria na Cairo Misri. Mwaka 1980 ilipoteza mbili na kutoka sare moja, lakini za 2019 ilipoteza zote tatu. Hivyo ilikuwa ni jambo la muda tu kuona watakuwa na kitu gani cha kushtua katika fainali za mwaka huu.
Bahati nzuri ni kwamba katika historia mwaka huu kwa mara ya kwanza Tanzania imeondoka na alama mbili kwenye mashindano hayo makubwa zaidi Afrika. Ni hatua nzuri.
Sababu kubwa ya Tanzania kutofanya vizuri kwenye Afcon iko wazi kabisa. Hatuna wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kushindana na wenzetu. Wachezaji wengi wa Stars ni wa kawaida mno.
Mbwana Samatta ndio kwanza anamalizia maisha yake ya soka. Kasi yake imepungua. Uwezo wake wa kupiga chenga umeshuka. Uwezo wa kufunga umepotea kabisa. Na huyu ndiye staa wa timu yetu.
Saimon Msuva umri naye umeanza kusogea. Kasi yake uwanjani imeshuka sana. Sio Msuva yule ambaye angeweza kukimbia kuliko mabeki wa timu pinzani. Leo anategemea zaidi kukaa katika nafasi na kufunga.
Wachezaji wengine waliobaki ni wa kawaida. Huwezi kuwafananisha kina Mzamiru Yassin, Feisal Salum, Kibu Denis na wengineo na mastaa wa timu za Zambia, DR Congo na Morocco. Hivyo wala hatujafanya vibaya sana, uwezo wetu ndio umeishia hapo.
Kitu pekee ambacho ungetarajia kingeleta maajabu kwenye fainali hizi ni mipango ya benchi la ufundi. Hata hivyo, ni kama vile Kocha Adel Amrouche hakuwa amejiandaa vizuri kwa ukubwa wa mechi hizi. Naye alioondoshwa baada ya mechi ya kwanza tu kisha wakaja makocha wazawa.
Ni hawa kina Hemed Morocco na Juma Mgunda. Ni makocha wakubwa kwa majina yao, lakini wamewahi kufanya nini kikubwa? Hakuna. Wanategemea zaidi uwezo wa kuhamasisha wachezaji uwanjani. Walitegemea zaidi uzalendo. Kiufundi sidhani kama wana maajabu yoyote. Hata hivyo, tunaweza kuwapigia makofi kuvuna alama mbili zinazokuwa rekodi kwa Stars katika fainali hizo za Afcon. Haikuwahi kutokea timu hiyo kuvuna pointi nyingi kama hizo na hata kupta cleansheet. Fainali zote mbili za nyuma iliambulia pointi moja na bila cleansheet.
Licha ya hivyo, lazima ukweli usemwe tu, Tanzania tuna safari ndefu kuwa na wachezaji wa kushindana katika fainali hizi. Hebu fikiria mfano kwenye fainali hizi wangeumia Samatta na Msuva kwenye nafasi zao wangecheza kina nani? Hakuna.
Cyprian Kachwele na Ben Starkie? Ingekuwa kituko. Licha ya kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kawaida wanaoanza, bado kuna tofauti kubwa ya viwango kwa wale wa kikosi cha kwanza na walioko benchi. Inafikirisha sana.
Hata hivyo, sasa tunarejea katika vita ya ngazi ya klabu. Simba na Yanga bado zipo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Bado zina nafasi ya kufuzu robo fainali kama zitacheza vizuri michezo yake ya mwisho.
Simba inatakiwa kwenda kuchukua alama kule Ivory Coast dhidi ya ASEC Mimosas kisha ishinde nyumbani dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana. Ikifanya hivyo itakwenda robo fainali.
Yanga inahitaji kushinda nyumbani dhidi ya CR Belouzdad kisha ikachukue alama mbele ya Al Ahly kule Misri. Itawezekana kama itakuwa na mipango mizuri.
Hata hivyo, sitazamii sana Ligi ya Mabingwa kwa mwaka huu.
Leo nimefikiria juu ya uwekezaji wa Simba na Yanga ni lini zitafikia kiwango cha kubeba ubingwa wa Afrika. Bado tuna safari.
Kuna vikwazo kadhaa lazima ziendelee kuvivuka ili kukaa sawa. Cha kwanza ni kuhakikisha mchakato wa mabadiliko wa timu zao unakamilika na zinakuwa chini ya wawekezaji. Soka la sasa linahitaji fedha na siyo maneno.
Ukitazama Simba ilikuwa imepiga hatua kwenye mashindano haya, lakini sasa imeanza kusuasua kwa sababu uongozi wa timu haujatulia. Ni kama vile Mohamed Dewji amekaa pembeni anatazama. Ushindani wao umeshuka kutokana na kukosa mipango mizuri ya fedha.
Inashangaza kuona hadi leo bado Dewji anachangia Sh 2 bilioni kwenye bajeti ya Simba. Ni fedha nyingi kwa kuzitazama, lakini kwenye uwekezaji wa soka la Afrika ni fedha kidogo.
Leo hii tunazungumzia Mamelodi Sundowns imetoka kusajili mchezaji wa Sh 6.2 bilioni. Ni mchezaji mmoja tu huyo. Je, kikosi chao chote kina thamani kiasi gani? Ni zaidi ya Sh 80 bilioni.
Yanga leo inaona kama iko sawa kwa kuwa GSM anatoa fedha. Itakuwaje siku akisema amechoka? Ni majanga. Mchakato ukamilike na GSM achukue timu kisheria. Awekeze vilivyo na kwenda kushindana Afrika.
Natamani kuona wakati huu Taifa Stars ikiendelea kujitafuta, Simba ama Yanga ichukue ubingwa wa Afrika. Nani atakuwa wa kwanza, ni jambo la kusubiri na kuona. Ila kama hazitakamilisha mfumo wa mabadiliko, naona tu tutaendelea kuiona robo fainali kama ndiyo hatua kubwa zaidi ya mafanikio kwetu.
Jamaa unaongea sana, wewe ungepewa hiyo timu au ungekuwa unacheza mpira ungesaidia kitu gani stars ivuke?
Huwa mna tatizo moja waandishi wa michezo wa nchi hii.Matokeo ya kiwa mabaya mnaongea sana na yakiwa mazuri mtasifia mngeanza kutuchambulia hata vitu vya hovyo. Sasa sifia hiyo Zambia unayoisia ambayo itaenda kucheza fainali.Hovyo kabisa
Jamaa unaongea sana, wewe ungepewa hiyo timu au ungekuwa unacheza mpira ungesaidia kitu gani stars ivuke?
Huwa mna tatizo moja waandishi wa michezo wa nchi hii.Matokeo ya kiwa mabaya mnaongea sana na yakiwa mazuri mtasifia mngeanza kutuchambulia hata vitu vya hovyo. Sasa sifia hiyo Zambia unayoisia ambayo itaenda kucheza fainali.Hovyo kabisa