Home Habari za michezo GAMONDI BADO AZAM TU….KWINGINE KOOTE ‘KASHALIZWA’ KIBABE….

GAMONDI BADO AZAM TU….KWINGINE KOOTE ‘KASHALIZWA’ KIBABE….

Habari za Yanga SC

HABARI ndio hiyo. Kocha Mkuu wa Yanga amesaliwa na michuano ya Kombe la Shirikisho ya Azam (ASFC) pekee ambayo ndio hajaonja machungu ya kupoteza hadi sasa katika msimu wake wa kwanza akiwa na kikopsi hicho alichojiunga nacho Julai 11 mwaka jana.

Kocha huyo kutoka Argentina amekuwa na bahati mbaya katika muda mfupi tangu ajiunge na Yanga kupoteza mechi katika kila michuano ambayo ameiongoza timu hiyo kuanza kwenye Ngao ya Jamii, Ligi Kuu Bara, Ligi ya Mabingwa Afrika na juzi kati katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Hii ni tofauti na ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Nasreddine Nabi ambaye kwenye msimu wake wa kwanza alikomaa kwenye Kombe la ASFC akicheza bila kupoteza hadi aliptwaa taji kwa Yanga kuifunga Coastal Union kwa penalti baada ya sare ya 3-3 dakika 120, kisha akalitetea taji msimu uliopita ikiichapa Azam kwa bao 1-0. Katika Ngao ya Jamii pia Nabi alianza kwa kuinyoa Simba kwa bao 1-0 kabla ya kutetea msimu uliopita kwa kuifunga tena Simba mabao 2-1.

Kwa Gamondi hali imekuwa sivyo kwa kuanza kwenye Ngao ya Jamii kwa kupoteza taji mbele ya Simba kwa kufungwa kwa penalti 3-1 baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 0-0 na katika Ligi alikumbana na kipigo mapema ilipopoteza kwa Ihefu kwa mabao 2-1 mechi iliyopigwa Oktoba 4 mwaka jana akifuata nyayo za Nabi aliyepoteza mechi ya kwanza ya Ligi Aprili 25, 2021 mbele ya Azam kwa bao pekee la Prince Dube kisha kucheza mechi 49 bila kupoteza hadi ilipokutana na Ihefu na kulala 2-1.

Michuano ambayo Gamondi achekani na Nabi ukiondoa kwenye Ligi ni michuano ya kimataifa kwani makocha wote hao katika msimu wa kwanza wamepoteza mechi pia.

Nabi alianza kwa kupasuka mbele ya Rovers United ya Nigeria katika mechi za raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, ingawa msimu uliopita alijitutumua alipoangukia Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Mabingwa Afrika na Al Hilal ya Sudan na kuifikisha timu fainali ikalikosa taji kwa kanuni ya bao la ugenini lililowabeba USM Alger ya Algeria kwani matokeo yalikuwa sare ya mabao 2-2.

Gamondi licha ya kuandika rekodi ya kuivusha Yanga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupita miaka 25 tangu iliposhiriki mwaka 1998, lakini mechi ya kwanza ya makundi alipasuka kwa kufungwa mabao 3-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria.

Kwa sasa Gamondi amesaliwa na michuano ya ASFC ambayo hajaicheza ili kuonyesha ubabe na kufuata nyayo za Nabi, kwani mchezo wa 64 Bora dhidi ya Hausing FC ya Njombe uliahirishwa kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024 ambayo Yanga ilitolewa hatua ya robo fainali.

Yanga ikiongozwa na Gamondi ilikubali kipigo cha mabao 3-1 kutoka kwa APR ya Rwanda, huku fainali ya michuano hiyo ikipigwa usiku wa jana kwa Simba kuumana na watetezi Mlandege.

Rekodi zinaonyesha msimu wa kwanza wa Nabi hakucheza Mapinduzi, kwani aliikuta timu imetoka kutwaa taji kwa kuifunga Simba kwa penalti baada ya dakika 90 kumaliza kwa suluhu, japo msimu uliopita timu hiyo ikiwa chini ya kocha huyo ilitolewa makundi baada ya kutoka sare ya 1-1 na Singida Big Stars (sasa Fountain Gate) katika mechi iliyowavusha wapinzani wao kwenda nusu fainali.

SOMA NA HII  MANARA :- TFF IMFUKUZE KAZI AMROUCHE....ANAIHUJUMU YANGA MCHANA KWEUPEEE...