Home Habari za michezo KISA TABIA ZA CHAMA….MABOSI SIMBA WAKIMBILIA KWA BENCHIKHA….KIBANO KIPYA HIKI HAPA…

KISA TABIA ZA CHAMA….MABOSI SIMBA WAKIMBILIA KWA BENCHIKHA….KIBANO KIPYA HIKI HAPA…

Habari za Simba leo

VIONGOZI wa Simba wameamua kukubaliana na kocha Abdelhak Benchikha kwa kuweka vipengele vigumu kwenye mikataba ya wachezaji, ikiwemo suala la nidhamu ndani na nje ya uwanja hasa kwa wachezaji wapya waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo lililofungwa wiki iliyopita na msimu ujao.

Mtendaji Mkuu wa Simba, Imani Kajula amesema kwa sasa hawatakuwa wapole kwa mchezaji yoyote ndani ya klabu hiyo atakayeonyesha nidhamu mbovu ikiwemo kwenda tofauti na kile kilichowekwa na kocha wao Benchikha, na watakapenda tofauti na vipengele vya mkataba .

“Viongozi hatutakuwa tayari kuona mchezaji anaenda kinyume na vipengele vya makubaliano, tunaungana na benchi la ufundi linaloongozwa na Benchikha kutovumilia mtu ambaye anajiona yeye ni mkubwa kuliko timu, hata ukiwa kipenzi cha mashabiki asipokuwa na nidhamu hatuwezi kumvumilia,” amesema Mtendaji huyo.

Inasemekana kuwa kocha Benchika ndiye aliyewashauri viongozi wa Simba kuweka baadhi ya vipengele hivyo kwenye mikataba ya wachezaji baada ya kukuta nidhamu mbovu kwa baadhi ya wachezaji wa timu hiyo, na viongozi wakaridhia.

Ikumbukwe kiungo wao, Clatous Chama kusimamishwa na kupelekwa kwenye kamati ya nidhamu lakini pia Mosses Phiri kabla ya kutemwa aliondolewa dakika za mwisho kwenye kikosi katika mechi ya Wydad Casablanca waliocheza hapa nchini baada ya kuchelewa muda wa chakula.

Habari zinasema kuwa Benchikha alipofika nchini aliweka mikakati yake kwa wachezaji wanapokuwa kambini ikiwemo suala la kuvaa sare (Uniform), kutochelewa muda wa kula na mazoezi, hata wachezaji wapya waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo wamekutana na kitu hiki huku wakiambiwa hakuna mchezaji bora ndani ya timu hiyo.

Miongoni mwa wachezaji wapya waliotambulishwa ndani ya Simba ni Babacar Sarr, Pa Omar Jobe , Fredy Michael, Saleh Karabaka, Ladack Chasambi na Edwin Balua.

Katika hatua nyingine Kocha Benchikha anatarajia kutua nchini muda wowote akitokea kwenye mapumziko ya muda mrefu na kurejea katika majukumu ya kazi yake ya kuimarisha timu yake kwa ajili ya mzunguko wa pili wa ligi kuu Tanzania Bara.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally amesema kuna baadhi ya nyota wa kigeni hasa wachezaji wapya waliosajiliwa dirisha dogo kuanza kuwasili na tayari kuanza rasmi mazoezi Alhamisi hii uwanja wa Mo Simba Arena, Bunju.

Amesema Mtaalamu wao Benchikha anarejea kwa ari mpya kwa ajili ya kukinoa kikosi cha timu yao kwa wachezaji wote kasoro wale ambao wako kwenye majukumu ya timu za Taifa zinazoshiriki fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON).

“Hadi jumatano ya wiki hii wachezaji wote wa kigeni ambao hawako kwenye timu ya Taifa watawakuwa wameshawasili nchini na Alhamisi kuanza rasmi mazoezi kwa ajili ya duru la pili la ligi kuu na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo wanatarajia kucheza dhidi ya Asec Mimosas,” amesema Ahmed.

Ameeleza kuwa ujio wa Benchikha utakuwa wa aina yake kwa sababu anahitaji kukisuka kikosi chake kinakuwa imara na kuanza safari yao ya kutafuta mafanikio katika mechi zilizopo mbele yao ikiwemo ligi kuu, FA na ligi ya Mabingwa Afrika.

SOMA NA HII  KUMBE ULIMWENGU ALIZICHOMOLEA SIMBA, YANGA ISHU IKO HIVI