Home Habari za michezo YANGA YENYE OKRAHA YAANZA KUOGOPWA HUKO…11 YA GAMONDI HUENDA IKAWA HIVI SASA…

YANGA YENYE OKRAHA YAANZA KUOGOPWA HUKO…11 YA GAMONDI HUENDA IKAWA HIVI SASA…

Habari za Yanga leo

USAJILI wa mshambuliaji Joseph Guede na Augustine Okrah utamfanya kocha Miguel Gamondi kuwa na machaguo mengi na kuzidi kuifanya timu hiyo iwe tishio na kama timu pinzani hazitakuwa makini huenda zikapata aibu kama zilizowakuta KMC, JKT Tanzania na Simba zilizopigwa tano tano katika Ligi Kuu.

Yanga ilizifunga JKT na KMC kwa mabao 5-0 kila moja, kisha kuicharaza Simba 5-1 katika Kariakoo Derby mbali na kugawa dozi kama hizo katika mechi za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asas ya Djibouti na Jamhuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024, iliyomalizika Jumatatu ya wiki hii.

Hata hivyo, kocha mkuu wa timu hiyo, Miguel Gamondi alikuwa akilalamika kila mara akidai bado timu yake haitumii nafasi inazozitengeneza na kuutaka uongozi umletee mshambuliaji mmoja wa kumaliza tatizo la mabao na ndipo akashushwa Joseph Guede kutoka Ivory Coast na Mghana Okrah mbali na Shekhan Ibrahim kutoka JKU ya Zanzibar ambaye ni kiungo mshambuliaji anayetumika pia katika nafasi nyingine tofauti.

Ingizo la wachezaji hao wapya waliochukua nafasi ya Jesus Moloko, Hafiz Konkoni na Crispin Ngushi, linamfanya Gamondi kuwa na jeuri ya kuwa na vikosi viwili vya moto, iwapo wachezaji hao watafanya mambo makubwa kuliko waliondoka.

Ipo hivi. Yanga imeachana na Moloko, huku ikiwatoa kwa mkopo Hafiz Konkoni kwenda Turk Birligi ya Cyprus na Crispin Ngushi akipelekwa Coastal Union ya Tanga na kuwaingiza Okrah, Shekhan na Guede.

Ujio wa mastaa hao wapya endapo kocha ataamua kuwatumia wote basi kuna wachezaji watatupwa nje ya kikosi kupisha hao waingie moja kwa moja, lakini wanampa kocha nafasi ya kutengeneza vikosi viwili tofauti vyenye nguvu ya kuwakimbiza wapinzani.

Tayari eneo la pembeni mbele, Moloko ameondolewa kabisa baada ya kuachwa, hivyo Okrah amejihakikishia nafasi endapo atafanya vizuri huku Guede akimtoa kati ya Clement Mzize au Kennedy Musonda ambao wote walikuwa na uhakika wa kucheza licha ya kugawana dakika, huku Shekhan akiwa na nafasi ya kuwapokea nyota hao au Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI au pale kwa Khalid Aucho na Mazi Nzengeli.

Hiki hapa kikosi ambacho kipo kwa sasa Yanga kikiwa na zaidi ya mchezaji mmoja na kuonyesha wazi, wapinzani watakuwa na kazi kama wanataka kutoka salama mbele ya vijana wa Gamondi.

Ukianzia kwenye eneo la kipa, anayeanza ni Djigui Diarra , lakini nyuma yake kuna Abutwalib Mshery na Metacha Mnata ambao hata wakianza bado huwezi kuona tofauti kubwa baina yao hata pale kipa namba moja aliyepo Afcon 2023 atakapokosekana.

Kwenye namba mbili kuna Yao Kouassi ambaye ndiye chaguo la kwanza, lakini akiwa na majembe kama Kibwana Shomary na pengine Dickson Job ambaye hutumika pia kwenye nafasi hizo, huku upande wa kushoto kuna Joyce Lomalisa mwenye namba yake, wakati Nickson Kibabage na hata Farid Mussa naye anaweza kuliamsha na usione tofauti kubwa.

Kwenye beki ya kati kuna nahodha Bakar Mwamnyeto na Ibrahim Bacca wenye uhakika wa namba, sambamba na Job anayetumika pia kwenye eneo hilo akiwamo Gift Fred ambaye ameuwasha moto katika michuano ya Kombe la Mapinduzi 2024.

Eneo la namba sita kuna Khalid Aucho huku Zawadi Mauya, Jonas Mkude na Shekhan Ibrahim wakiwa wana uwezo wa kufunika kama dokta akikosekana, huku kwenye wingi ya kulia kuna Maxi Nzengeli mwenye uhakika wa namba, lakini akiwa na watu wa kumsaidia akiwamo Skudu Makudubela, Denis Nkane na Shekhan pia hapo anaingia. Katika namba nane kuna Pacome Zouzoua akipigwa tafu na Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Shekhan anayeingia eneo hilo pia.

Mshambuliaji wa kati ni Guede ambaye kama ataingia na moto atawapiku Musonda na Clement ambao walikuwa wakipokezana baada ya Konkoni kuchemka, wakati mshambuliaji wa pili anaweza kuanza Stephane Aziz KI ama Pacome na bado akawa na msaada wa Shekhan na kushoto Okrah ana uhakika, japo anaweza pia kutumika kama mshambuliaji namba mbili au winga wa kulia akipokezana pia na Aziz Ki au Shekhan anayemudu kucheza pia nafasi hizo. Kiufupi kama ulikula 5 na kikosi kile cha mwanzo wa msimu, usipojipanga katika kikosi hiki cha kumalizia msimu 2023-24 unaweza kupasuka nyingi zaidi. Sisi yetu macho tu.

WASIKIE MAKOCHA

Kocha wa zamani wa Yanga, Boniface Mkwasa ‘Master’ akizungumzia juu ya maingizo hayo mapya yanayoenda kuiimarisha zaidi Yanga inayoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na ya pili kwa kufunga mabao mengi nyuma ya vinara Azam FC, alisema ni maingizo muhimu.

Mkwasa alisema usajili uliofanywa ni muhimu kwa eneo la ushambuliaji akiamini ni sahihi kama kocha ndiye aliyependekeza kutokana na kilio cha muda mrefu cha kukosa mchezaji wa eneo hilo.

“Simfahamu (Guede) hivyo siwezi kumzungumzia sana lakini naamini kama ni pendekezo la kocha anaweza kuongeza kitu na kuisaidia timu ukiangalia aina ya wachezaji watakaokuwa wanamlisha mipira waliopo Yanga anahitaji kufanya kilichomleta naamini atafanikiwa kumaliza tatizo lililokuwepo,” alisema Mkwasa.

Kocha wa zamani wa Tanzania Prisons, Mohamed ‘Adolf’ Rishard, ambaye amekuwa kwenye ligi kwa muda mrefu alisema kwenye usajili kuna kubahatisha, kupatia au kukosea. .

Alisema Guede ataisaidia timu hiyo kutokana na kutoka nchi ambayo ina mashindano mengi na ushindani mkubwa wa ligi yao huku akiweka wazi kuwa atakuja Yanga kama mwenyeji kutokana na kukutana na wachezaji wanaozungumza lugha moja.

“Guede huenda ikawa kuna wachezaji wanaocheza Yanga wamechangia aje kutokana na kuzungumza lugha moja na kutoka nchi moja mfano Pacome Zouzoua, Yao na Stephane Aziz Ki ambao wanazungumza Kifaransa watampokea na kumuelewesha aina ya soka analotakiwa kucheza,” alisema Adolf, nyota wa zamani wa Yanga, Pan African na timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, iliyoshiriki fainali za kwanza za Mataifa ya Afrika (Afcon) 1980 zilizofanyika Nigeria.

“Pia wanacheza nyuma yake Aziz Ki, Pacome hivyo kutakuwa na maelewano mazuri eneo hilo na ni wachezaji sahihi wa kumlisha mshambuliaji natarajia manufaa makubwa zaidi kwake,” aliongeza Adolf.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI YA LEO SIMBA WATENGA MAMILIONI KUIMALIZA USGN ...TRY AGAIN AFUNGUKA MKAKATI ULIVYO...