Kuelekea sherehe za kuadhimisha miaka 89 ya mabingwa wa historia Yanga, Februari 11 uongozi wa klabu hiyo umeandaa suprize kwa mashabiki wake ikiwa ni sambamba na uzinduzi wa ofisi za klabu hiyo Jumatano.
Februari 11, Yanga inatimiza miaka 89 tangu kuanzishwa kwake na sherehe za kuadhimisha miaka hiyo zinaanza leo kwa timu hiyo kuingia mkataba na mojawapo wa hospitali kubwa kwa ajili ya wanachama wake.
Akizungumza na wanahabari, Ofisa Habari wa klabu hiyo, Ally Kamwe amesema watakuwa na suprize nyingi kwa wanachama wa klabu hiyo hadi siku ya kilele kubwa wanaanza na kuingia mkataba na moja ya hospital kubwa Afrika kwa ajili ya wanachama wao.
“Kesho tunaingia mkataba na moja ya hospitali kubwa barani Afrika kwa ajili ya wanachama wetu kwa lengo la kuwanufaisha kwenye masuala yanayohusu afya zao na Jumatano tutakuwa na uzinduzi wa ofisi zetu za Jangwani,” amesema Kabwe.
“Tumejenga ofisi za kisasa nzuri ambazo zina hadhi ya klabu yetu kongwe, hivyo siku hii kutakuwa na viongozi wetu wote watakuwa na kitu cha kuzungumza zaidi, lakini ieleweke kuwa tutakuwa na ofisi za viwango.”
Ofisa huyo ameongeza kuwa, “uongozi umefanya ukarabati wa kihistoria na umeifanya Yanga kuwa na ofisi bora zaidi Afrika Mashariki na Kati.”
Pia amesema hawezi kuzungumza kila kitu walichokiandaa, lakini wana mambo mengi zaidi kuelekea siku hiyo ya kumbukumbu ya kuanzishwa kwa klabu hiyo.
“Sherehe za miaka 89 ya Yanga zitafanyika jijini Mbeya ambapo tutakuwa na mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Tanzania Prisons siku ambayo timu yetu ndio inatimiza miaka hiyo,” amesema.
Amesema ratiba inaonyesha kutakuwa na mchezo huo wa ligi, hivyo Mkoa wa Mbeya umepata bahati ya kusherehekea siku ya ‘birthday’ ya klabu hiyo.
“Siku hiyo tunakwenda kuzindua nyimbo mbili kubwa kwa lengo la kusheherekea kilele cha miaka 89 ya timu yetu na kuelekea siku hiyo ni jiwe juu ya jiwe, hatutapoa.”