Home Habari za michezo HIZI HAPA DONDOO MUHIMU KUELEKEA FAINAL YA AFCON LEO….NI KIVUMBI CHA HAJA…

HIZI HAPA DONDOO MUHIMU KUELEKEA FAINAL YA AFCON LEO….NI KIVUMBI CHA HAJA…

Habari za Michezo leo

Itakuchukua saa mbilli na nusu au tatu ukisafiri kwa ndege kutoka Lagos nchini Nigeria hadi kufika Abdijan, Ivory Coast yanapofanyika mashindano ya Afcon mwaka huu. Umbali wa kutoka Jijini Lagos hadi Abdijan ni kilomita 815, ambazo ndio zitakuwa kilomita walizosafiri mashabiki mbali mbali wa Nigeria kwenda nchini Ivory Coast kwa ajili ya kuitazama timu yao ikicheza fainali dhidi ya wenyeji Ivory Coast kwenye Afcon 2023.

Wababe hao wanakutana ikiwa ni baada ya kufanya vibaya kwenye hatua ya makundi hadi wakapewa nafasi ndogo ya kuingia kwenye hatua ya 16 bora.

Timu hizo zimekutana mara saba kwenye mashindano hayo, Nigeria ikishinda mara tatu, Ivory Coast mara mbili na mechi mbili zilimalizika kwa sare. Hapa tunakuwekea baadhi ya vitu muhimu vinavyohusu mechi hiyo itakayopigwa kuanzia saa 5:00 usiku.

DONDOO MUHIMU

Baada ya kuifunga Ivory Coast bao 1-0 kwenye hatua ya makundi, Nigeria itakuwa inahitaji kurudia rekodi ya kuifunga timu moja mara mbili kwenye fainali za Afcon baada ya kufanya hivyo mwaka 2006 ambapo iliifunga Senegal kwenye hatua ya makundi na mchezo wa kuwania mshindi wa tatu.

Ivory Coast itakuwa inapambana kuwa timu ya sita mwenyeji wa Afcon kushinda kwenye fainali ambapo mara ya mwisho ilikuwa ni Misri 2006 iliyoshinda kwa penalti baada ya kumaliza dakika 120 kwa suluhu.

Timu mwenyeji tano kati ya sita zilizofika fainali zilifanikiwa kushinda kombe isipokuwa Nigeria iliyopoteza mbele ya Cameroon kwa penalti 2000.

Nigeria itakuwa inacheza fainali ya nane kwenye mashindano hayo ikiwa imezidiwa na Misri na Ghana ambazo zimecheza mara tisa. Katika fainali mbili za mwisho Nigeria imefanikiwa kushinda zote ambazo ni 1994 na 2013.

Fainali nne za mwisho ambazo Ivory Coast imecheza zilimalizika bila bao lolote na zikaamuliwa kwa penalti ambapo Ivory Coast ilishinda mara mbili nazo ni 1992 na 2015, zote dhidi ya Ghana na ilipoteza 2006 dhidi ya Misri na 2012 mbele ya Zambia. Ivory Coast imeshinda mechi 17 kati ya 18 za Afcon baada ya kuanza kufunga bao. Mara ya mwisho kuanza kufunga bao kwenye mechi na kupoteza ilikuwa ni dhidi ya Algeria mwaka 2010 ambapo ilifungwa mabao 3-2.

Pia Tembo hao hawajapoteza mechi 22 ambazo walianza kufunga bao tangu 2010 walipopoteza mbele ya Misri ikiwa imeshinda mechi 19 na kutoa sare tatu.

Katika kipindi cha miaka zaidi ya 10, mechi za fainali za mashindano hayo zilimalizika kwa matokeo ya ba 1-0 (mara nane), 0-0 (mara saba), tangu 2002 fainali zote zimemalizika kwa matokeo ya aina hiyo isipokuwa 2004 ambapo Tunisia ilishinda mabao 2-1 na mwaka 2017 ambapo Cameroon ilishinda 2-1.

Tangu ilipopoteza kwa mabao 3-1 mbele ya Misri 2010, Nigeria imeruhusu mabao 16 kwenye mechi 28 za Afcon na mabao manane kati ya hayo ndio ambayo wamefungwa kupitia mipira isiyokuwa ya kutengwa.

William Troost-Ekong kutoka Nigeria amefunga mabao manne katika mashuti matano aliyopiga kwenye lango la wapinzai na mwaka huu amefunga mabao mawili kupitia penalti akiwa ndio mchezaji wa kwanza wa Nigeria kufunga penalti mbili baada ya Samuel Ojebode (1976), Jay-Jay Okocha (2004) na Victor Moses (2013), ukiondoa zile penalti baada ya dakika 120.

Mabao sita ambayo Ivory Coast imefunga kwenye mashindano ya mwaka huu yote yamefungwa na wachezaji tofauti ambao ni Seko Fofana, Jean-Philippe Krasso, Franck Kess, Simon Adingra, Oumar Diakit na Sebastien Haller. Mara yamwisho kuwa na wafungaji wengi kwenye Afcon ilikuwa ni 2008 ambapo walikuwa wanane.

Straika wa Nigeria, Victor Osimhen amepiga mashuti 24 kwenye mashindano ya mwaka huu na kufunga bao moja tu, hiyo ni sawa na asilimia nne tu ubadilishaji wa mashuti kuwa mabao ikiwa inaonekana kuwa wastani mdogo.

Wachezaji pekee waliowahi kupiga mashuti mengi kwenye shindano moja la Afcon kumzidi tangu mwaka 2010 ni Asamoah Gyan wa Ghana ambaye alipiga mashuti 25 na kufunga bao moja mwaka 2013 na Vincent Aboubakar kutoka Cameroon ambaye alipiga mashuti 31 mwaka 2021 na kufunga mabao nane.

WAAMUZI

Mwamuzi wakati atakayesimamia mechi hii kwa dakika zote ni Dahane Beida ambaye ndio alichezesha mchezo wa ufunguzi wa Super League kati ya Simba na Ahly uliopigwa katika dimba la Mkapa, Jijini hapa.

Pia aliwahi kuchezesha mashindano ya Kombe la Dunia kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17, yaliyofanyika nchini Indonesia 2023.kwenye fainali za Afcon mwaka huu alichezesha mchezo wa 16 bora kati ya Angola na Namibia ambapo Angola ilishinda mabao 3-0, pia alichezesha mechi ya Misri na Msumbiji ambao ulimalizika kwa sare ya mabao 2-2.

Kwa upande wa washika vibendera watakuwepo Emiliano Dos Santos (Angola) na Diana Chicotesha (Zambia), mwamuzi wa mezani ni Bouchra Karboubi (Morocco). VAR itasimamiwa na Mohamed Ashour (Egypt) na Maria Rivet (Mauritius)

UWANJA Fainali hii inatarajiwa kupigwa katika dimba la Alassane Ouattara Stadium saa 5:00 usiku ambayo ni sawa na 2:00 usiku kwa saa za pale nchini Ivory Coast. Uwanja huo una uwezo wa kuingiza mashabiki 60,012 na ulijengwa mwaka 2016 kabla ya kuvunjwa na kufanyiwa marekebisho mwaka 2020 ambapo taarifa zinadai zilitumika Dola 257 milioni kuukarabati.

VIKOSI Nigeria: Olorunleke Ojo, Stanley Nwabali, Francis Uzoho, Kenneth Omeruo, William Troost-Ekong, Semi Ajayi, Chidozie Awaziem, Calvin Bassey, Bruno Onyemaechi, Bright Osayi-Samuel, Ola Aina, Zaidu Sanusi, Alhassan Yusuf, Raphael Onyedika, Joe Aribo, Frank Onyeka, Moses Simon, Paul Onuachu, Ahmed Musa, Alex Iwobi, Victor Osimhen, Kelechi Iheanacho, Samuel Chukwueze, Terem Moffi, Ademola Lookman. KOCHA: Jose Peseiro

Ivory Coast: Charles Folly, Yahia Fofana, Badra Ali Sangaré, Evan Ndicka, Wilfried Singo, Ousmane Diomande, Ismaël Diallo, Sèrge Aurier, Odilon Kossounou, Ghislain Konan, Willy-Arnaud Boly, Seko Fofana, Jean Seri, Franck Kessié, Idrissa Doumbia, Ibrahim Sangaré, Lazare Amani, Max Gradel, Jérémie Boga, Simon Adingra, Oumar Diakité, Jean-Philippe Krasso, Sébastien Haller, Jonathan Bamba, Christian Kouamé, Nicolas Pépé, Karim Konaté. KOCHA: Emerse Fae

SOMA NA HII  MBUNGI YA AZAM vs YANGA KUPIGWA SIKU HII WIKI IJAYO