Home Azam FC KWA HALI HII ILIVYO AZAM FC KUBEBA UBINGWA NI MIUJIZA TU…

KWA HALI HII ILIVYO AZAM FC KUBEBA UBINGWA NI MIUJIZA TU…

Azam FC

Azam ipo kwenye wakati mgumu wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kundi kubwa la wachezaji wake kukumbwa na majeraha makubwa.

Azam ina wakati mgumu wa kuwania baada ya mastaa wake zaidi ya saba wakiwa nje wanasumbuliwa na majeraha na hivyo wanaweza kuukosa mchezo dhidi ya Prisons.

Gibril Sillah, Feisal Salum Fei Toto, pamoja na Prince Dube wapo nje wakiuguza majeraha madogo, huku Allasane , Malikou Ndoye, Sospeter Bajana na Franklin Navaro wakiwa na majeraha makubwa ambayo yanahitaji upasuaji.

Mbali na hao makipa wao wawili wa kimataifa, Ali Ahmada na Abdulai Idrisu wanaendelea na matibabu baada ya kufanyiwa upasuaji.

Hili linaweza kuwa pigo kubwa kwa Azam kwa ajili ya mbio za ubingwa ambazo kwa sasa inashika nafasi ya pili nyuma ya Yanga.

Youssouph Dabo alisema timu yake ina kikosi kipana lakini kuna wachezaji tayari walikuwa wameingia kwenye mfumo hivyo ni kazi kwake kuhakikisha anarudisha ushindani na kuweza kufikia malengo.

“Tunaenda ugenini kupambana na Tanzania Prisons tukiwa na baadhi ya wachezaji ambao hawawezi kucheza mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na majeraha, hilo haliondoi sisi kutafuta matokeo ambayo yataendelea kutupa nafasi ya kupambania taji msimu huu kama malengo yetu yalivyo;

“Tumetoka kuambulia suluhu dhidi ya Tabora United ugenini sasa tunasafiri kwenda Mbeya tunahitaji ushindi mzuri ambao utatufanya tuendeleze ushindani dhidi ya timu mbili tunazofukuzana nazo nafasi ya juu,” alisema.

Akizungumzia mchezo huo, Dabo alisema ushindani umekuwa mkubwa kutokana na mahitaji ya kila timu hivyo jambo kubwa kwao ni pointi tatu zitakazowaweka katika hali nzuri ya kiushindani.

“Tuna kazi kubwa ya kufanya kwa sababu tuna pengo la pointi na walio juu yetu ingawa tuko kwenye mstari mzuri. Nafurahishwa kwa kiasi kikubwa na aina ya upambanaji unaoonyeshwa na wachezaji kuanzia mwanzo hadi mwisho,” alisema.

Dabo aliongeza, siri kubwa ya kufanya vizuri ni maelewano mazuri aliyonayo kwa wachezaji na viongozi ila amewataka kuendelea kupambana zaidi kwani kasi ya wapinzani wao sio ndogo hivyo jitihada kubwa zinahitajika kila mchezo.

“Suluhu tuliyoipata na Tabora United imebadilisha taswira nzima na hicho ndicho kitu kimetutokea kwa sababu tulikuwa tunaongoza kwa muda mrefu lakini baada ya wenzetu kucheza michezo ya viporo wamesogea juu. Hii ni ishara ya kutobweteka tulipo.”

Mara ya mwisho kwa Azam kutwaa ubingwa wa Bara ilikuwa msimu wa 2013-2014 ilipoivua Yanga kwa kubeba bila kupoteza ikikusanya pointi 62 ikiifikia rekodi iliyowahi kuwekwa na Simba msimu wa 2009-2010.

SOMA NA HII  BAADA YA MO DEWJI KUJIUZULU..BONASI SIMBA SASA ZIPO HIVI...TRY AGAIN AFUNGUKA A-Z