Winga wa Yanga, Augustine Okrah amesema baada ya kupona majeraha aliyoyapata kwenye mechi ya Kombe la Mapinduzi 2024 sasa amerejea kwenye utimamu wake na kadri siku zinavyoenda anazidi kuimarika na kwamba ule utamu uliokuwa unasubiriwa na mashabiki utaanza kupatikana muda si mrefu.
Okrah aliyeichezea Simba msimu uliopita, alitua Yanga katika dirisha dogo la usajili lililofungwa Januari 15 mwaka huu na tayari ameanza kuonyesha makeke yake kikosini hapo akitoa asisti mbili kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC), ambao chama lake lilishinda 5-0 dhidi ya Polisi Tanzania na juzi kuonyesha kiwango bora alipoingia kipindi cha pili wakati Yanga ikiichakaza CR Belouizdad kwa kichapa mabao 4-0 na kutinga robo fainali.
Okrah alisema anazidi kuimarika kila siku na sasa anatumaini atapata muda wa kutosha kuwatumikia Wananchi.
βAwali nilikuwa na majeraha, hivyo sikupata muda wa kucheza. Ukitoka kwenye majeraha hauwezi kuingia moja kwa moja kikosini, namshukuru Mungu napata nafasi na kucheza na naamini kadri siku zinavyozidi kwenda naimarika zaidi na nitapata muda zaidi wa kucheza na kuonyesha ubora wangu,β alisema Okrah anayevaa kinyago usoni kutokana na jeraha la mishipa ya uso alilolipata.
Kabla ya kutua Yanga, Okrah alikuwa akicheza klabu ya Bechem United ya kwao Ghana ambapo katika mechi 16 alizocheza alicheka na nyavu mara tisa.
Wachezaji wengine waliosajiliwa kipindi cha dirisha dogo ndani ya Yanga ni pamoja na Mshambuliaji Joseph Guede aliyefunga bao la nne lililoipeleka Yanga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika juzi.