Home Habari za michezo MIAKA 89 YA YANGA ILIVYOSHEREKEWA KIBABE MBEYA LEO HII…MZIZE, PACOME NI BALAAH…

MIAKA 89 YA YANGA ILIVYOSHEREKEWA KIBABE MBEYA LEO HII…MZIZE, PACOME NI BALAAH…

Habari za Yanga leo

Yanga wameidhimisha miaka 89 ya Kumbukizi ya siku ya kuzaliwa kwao kwa Ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania Prisons kwenye mchezo uliokuwa na rapsha za hapa na pale uliopigwa kwenye dimba la CCM Sokoine, jijini Mbeya.

Yanga walipata bao la Mapema kabisa dakika ya 8 tu kupitia kwa mshambuliaji wake Clement Mzize aliyemalizia kishujaa krosi iliyoonekana kama haina madhara kutoka kwa Pacome Zouzoua upande wa kulia.

Mchezo ulilazimika kusimama kwa zaidi ya dakika 2 kupisha matibabu ya Mlinzi wa Prisons Salum Kimenya aligongwa kichwani na goti la Lomalisa Mutambala wakati wakigombea mpira dakika ya 17.

Kauli ya “Prison Confidence” ilionekana kufanya kazi kwani licha ya kuwa nyuma kwa bao 1-0 Prisons walionekana kuwa watulivu huku na wao wakisogea karibu kabisa kwenye lango la Yanga lakini ukisefu wa utulivu na mawasiliano hasa kwenye eneo la mwisho liliwaangusha.

Yanga walitengeneza baadhi ya nafasi lakini ya wazi zaidi ni aliyoipoteza Maxi Nzengeli aliyeshindwa Kumalizia vizuri mpira ulioshindwa kuunganishwa na Farid Mussa dakika ya 43 na yeye kupiga mpira uliogonga mwamba pakiwa hakuna golikipa golini.

Dakika ya 45+3, Pacome Zouzoua katika utulivu wa hali ya juu akipokea pasi murua kutoka kwa MuIvorian mwenzake Yao Kouassi akausereresha mpira katikati ya miguu ya Yona Amos na kuiandikia Yanga bao la 2.

Mapumziko Yanga walitoka wakiwa kifua mbele kwa mabao 2-0.

Ally Msengi aliingia kipindi cha pili upande wa Prisons mwanzoni kabisa likiwa ndio badiliko pekee kwa timu zote mbili kuanza kipindi cha pili.

Mechi iliendelea kuwa yenye ushindani huku Prisons wakionyesha kuongeza kasi ya mashambulizi.

Kuanzia Dakika ya 58, iliwalazimu Yanga kucheza wakiwa pungufu baada ya golikipa Metacha Mnata kumzuia isivyo halali akiwa ndiye mtu wa mwisho Samson Mbangula ambaye alikuwa akililielekea lango la Yanga.

Dakika ya 63, Jeremiah Juma alitumia mpira huo wa adhabu kuwarejesha Prisons mchezoni baada ya kufunga kiumarudadi kabisa mpira uliomshinda golikipa Abutwalib Mshery aliyeingia baada ya Metacha Mnata kutoka huku akipishana na Farid Mussa. 2-1 bado ilikuwa faida kwa Yanga.

Licha ya kuwa Pungufu bado Yanga walionekana kuwa hatari huku Prisons wakiwa taratibu sana kwenye kuanzisha au kufanya mashambulizi ya kasi hivyo kuwaruhusu Yanga kupumua na wao kuweza kujenga mashambulizi pia. Akitambulishwa mchezoni Joseph Guede nafasi ya Clement Mzize.

Joseph Guede alipata nafasi nzuri eneo la 18 lakini shuti lake liliokolewa vizuri na Yona Amos. Wakati huo Stephane Aziz Ki alitambulishwa mchezoni nafasi ya Pacome Zouzoua huku Gift Fred akichukua nafasi ya Maxi Nzengeli yakiwa mabadiliko ya kiufundi.

Dakika ya 87, Prisons nao walijikuta pungufu baada ya Zabona Mayombya kutolewa nje kwa kadi ya pili ya njano kwa kile kilichotafsiriwa na muamuzi kuwa alijidondosha kwenye eneo la 18 na kudai penati.

Stephane Aziz Ki alipata nafasi ya kupiga mpira wa faulo lakini Amos Yona tena alifanikiwa kuliweka salama lango la Prisons.

Dakika zote 90 zikatamatika zikishuhudia Yanga wakibuka na ushindi wa mabao 2-1.

Kwa matokeo hayo, Yanga wanazidi kujikita kileleni mwa Msimamo wa Ligi kuu wakifikisha alama 40.

SOMA NA HII  KIUNGO WA SIMBA SAKHO CHINI YA UANGALIZI