Home Habari za michezo WAKATI UPANDE WA PILI NI VICHEKO TUPU…BENCHIKHA KATAZAMA WEE..KISHA AKASEMA HILI…

WAKATI UPANDE WA PILI NI VICHEKO TUPU…BENCHIKHA KATAZAMA WEE..KISHA AKASEMA HILI…

Habari za Simba

Kitendo cha Simba kulazimishwa suluhu ugenini kwenye mechi ya Kundi B ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Asec Mimosas ya Ivory Coast, kisha Yanga kushinda mabao 4-0 mbele ya CR Belouizdad ya Algeria na kutinga robo fainali kupitia Kundi D kumewachanganya mashabiki wa Msimbazi.

Wanaamini chama lao, lilistahili kuwa la kwanza kutinga hatua hiyo kama ilivyowahi kufanya katika misimu mitatu kati ya mitano iliyopita, lakini kocha wa timu hiyo, Abdelhak Benchikha amewatuliza mashabiki hao na kuwaambia wamwachie yeye kwani anajua anachokifanya na muda si mrefu watafurahi na roho zao.

Simba inatarajiwa kuikaribisha Jwaneng Galaxy ya Botswana katika mechi ya mwisho ya kundi hilo itakayopigwa Kwa Mkapa wikiendi hii ambapo ushindi wa aina yoyote utaivusha Simba na kuiingiza robo fainali kwa mara ya tano ya michuano ya CAF ndani ya misimu sita ikiwamo moja ya Kombe la Shirikisho na nne za Ligi ya Mabingwa.

Kocha huyo aliyetwaa Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na CAF Super Cup msimu huu, akiwa na USM Alger ya Algeria, alisema mechi na Jwaneng itakuwa ni zaidi ya fainali kwa Simba, kwani wanahitaji ushindi ili kusonga mbele na tayari amejua namna gani atawamaliza wapinzani hao.

Benchikha alisema anautazama mchezo huo kwa jicho jingine na anatarajia kufanya baadhi ya mabadiliko katika kikosi chake ili kutengeneza zaidi mashambulizi tofauti na michezo iliyopita na kwamba mashabiki wasiwe na presha kabisa.

“Mechi ijayo ni zaidi ya fainali kwetu, tunahitaji ushindi na tayari tumeanza kuandaa namna ya kushinda. Mambo ya ufundi niachiwe mimi na benchi zima tunajua nini tutafanya, lakini nawaomba mashabiki na wanachama wa klabu yetu kujitokeza kwa wingi zaidi katika mechi hiyo,” alisema Benchikha aliyeiongoza timu hiyo kwenye mechi nne za makundi ya msimu huu na kuvuna pointi tano, ikishinda mara moja na kutoka sare mbili na kupoteza mara moja.

“Ni mechi ya historia kwa kila mmoja wetu. Tunaamini itawezekana na pia tutawashangaza wengi namna tutakavyoanza na kumaliza mechi hiyo,” aliongeza kocha huyo.

Simba, Jwaneng na wanafainali wa msimu uliopita wa michuano hiyo, Wydad CA ya Morocco kila moja ina nafasi ya kuifuata Asec iliyotangulia robo fainali kutoka Kundi B, hivyo kufanya mechi za mwisho zitakazopigwa siku na muda mmoja kuwa na utamu wake, kwani wakati Simba ikimalizana na Jwaneng, Wydad itakuwa nyumbani kuikaribisha Asec iliyofuzu tayari kwa kukusanya pointi 11 katika mechi tano za awali ilizocheza hadi sasa.

Simba na Wydad kila moja ina pointi sita, lakini matokeo baina yao yanaibeba Simba kama zitamaliza zikilingana kwa alama, kwa vile matokeo ya jumla timu hizo zilipokutana Simba ilishinda 2-1.

Katika kundi B, imebaki nafasi moja tu ya kufuzu robo fainali baada ya Asec Mimosas yenye alama 11 kujihakikishia kusonga mbele ikiwa kileleni wakati Jwaneng ipo mkiani kwa sasa na pointi nne tu.

Hata hivyo, rekodi zinaibeba Simba inapocheza Uwanja wa Mkapa kwenye mechi za CAF kwani tangu msimu wa 2018/2019 katika mashindano yote imecheza jumla ya mechi 24 na kupoteza mbili tu ambazo ni ile iliyochapwa 3-1 na hao hao Jwaneng na kuondoshwa katika duru ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa mwaka 2021 kwa bao la ugenini baada ya mechi ya kwanza kushinda 2-0 ugenini na matokeo ya jumla kuwa (3-3), na ile ya msimu uliopita dhidi ya Raja Casablanca ilipofungwa 3-0.

Wachezaji wa Simba Shomari Kapombe, Henoc Inonga, Mohamed Hussein, Aishi Manula, Israel Mwenda, Sadio Kanoute, John Bocco, Mzamiru Yassin, na Kenedy Juma ni wachezaji wa Simba waliokuwa kwenye kikosi kamili dhidi ya Jwaneng wakati wanapoteza mechi hiyo, hivyo hii itakuwa ni mechi ya kisasi.

SOMA NA HII  KWA SIMBA HUUU...ATAPIGWA MTU NYINGI...CHAMA AFUNGUKA KILA KITU...AWATAJA WATOTO, MAGORI....