Home Habari za michezo ROBERTINHO:- PACOME ALINIFUKUZISHA KAZI SIMBA….KUHUSU UBORA WA CHAMA MHHH…..

ROBERTINHO:- PACOME ALINIFUKUZISHA KAZI SIMBA….KUHUSU UBORA WA CHAMA MHHH…..

Habari za Michezo leo

KOCHA wa zamani Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’, aliyetimuliwa Msimbazi Novemba mwaka jana, baada ya kichapo cha mabao 5-1 ilichoopewa na Yanga, amevunja ukimya na kuzungumzia kilichomponza hata kutemeshwa kibarua akimtaja kiungo mshambuliaji wa Yanga, Pacome Zouzoua.

Mbrazili huyo alisema kuwa kiwango kikubwa cha nyota huyo kilichowavuruga kwenye mechi ya watani, ndicho kilichomponza na kuwafanya mabosi wa Msimbazi kuamua kumfuta kazi.

Pacome aliyesajiliwa msimu huu akitokea ASEC Mimosas akiwa mchezaji bora wa msimu uliopita, ndiye aliyetengeneza nafasi nyingi za mabao katika mechi hiyo ya watani iliyopigwa Novemba 5 na akifunga bao la tano lililowanyong’onyesha mashabiki wa Simba ambao hawakuwahi kuiona timu hiyo ikifungwa mabao mengi katika ligi.

Kiungo huyo aliyefunga mabao tisa, yakiwamo matatu ya Ligi ya Mabingwa Afrika na sita ya Ligi Kuu kupitia mechi 15 walizocheza kati ya 16 akitumika kwa dakika 1134 huku akiasisti mara nne ikiwamo moja ya mcihauno ya CAF.

Akizungumza kutoka Brazili, Robertinho alieleza kama alitimuliwa kutokana na matokeo ya mechi yake ya mwisho dhidi ya Yanga basi ubora wa Pacome ulichangia kwa asilimia kubwa kuondoka katika klabu hiyo.

Alisema Pacome ni kiungo ambaye anacheza soka la kisasa sana akiwa na kasi, ya kwenda lango la wapinzani pia anacheza kwa ajili ya timu sio kutafuta ustaa.

“Sitaki kuingia kwenye siasa za nani bora kati ya Chama na Pacome, kwani nawaheshimu wote ni wachezaji wenye akili kubwa, lakini Pacome bado atabaki katika kumbukumbu isiyofutika kwangu kwa namna alivyotupa shida kwenye mechi ya mwisho,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Naona moto ule ameendelea na kama ataendelea hivi ataendelea kusumbua kwenye ligi ya Tanzania na Afrika, napenda sana uchezaji wa Pacome kwa kuwa ni kiungo. Uwepo wa Pacome Yanga umemrahisishia kazi Aziz KI kwa kuwa timu nyingi zitamwangalia zaidi yeye na wakati Yanga ina wachezaji wengine hatari kama Aziz.”

Mastaa hao wa Yanga wanaofahamika kwa ubora wao,wote wakitokea timu moja ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast, licha ya kuzungumziwa na kocha huyo lakini wamekuwa na wakishikilia rekodi ya mabao.

Aziz KI mpaka sasa ndie anaongoza kwa ufungaji Ligi Kuu akiwa na mabao 10 na kutokana na ubora wao kuna uwezekano mkubwa wa viungo hawa kufunga zaidi mpaka mwisho wa msimu. Yanga itakuwa ugenini Ijumaa, Tarehe 8 Machi kusaka alama tatu dhidi ya Namungo, ikiwa ni mechi ya 17 ya ligi wakiwa na jumla ya pointi 43 katika michezo 16 waliyokwisha kucheza.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI NA LIVERPOOL KESHO....ROONEY APIGA DEBE RONALDO ASIPANGWE....KISA NI....