Zimepita siku 123 sawa na miezi minne tangu Kocha Roberto Oliveira ‘Robertinho’ alipotimuliwa kazi Simba saa chache tangu timu hiyo ilipofumuliwa mabao 5-1 na Yanga katika pambano la Ligi Kuu Bara la Kariakoo Derby lililochezwa Novemba 5 mwaka jana kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Kocha huyo Mbrazili alisitishiwa mkataba Novemba 7 na kurejea kwao, huku nafasi yake ikizibwa na Abdelhak Benchikha kutoka Algeria anayeinoa kwa sasa Simba ikiwa nafasi ya tatu kwa kukusanya pointi 36 katika mechi 16.
Hata hivyo, licha ya kupitia karibu miezi minne sasa tangu afurushwe Msimbazi, kocha huyo amekiri bado haamini hadi sasa kitu gani kilichowafanya mabosi wa klabu hiyo kumfukuza kazi wakati hadi sasa Simba haijabadilika lolote na wala kukaa vizuri tofauti na alivyoiacha.
Kocha huyo aliyeiongoza timu hiyo katika mechi saba za Ligi Kuu msimu huu, akishinda sita na kupoteza moja tu dhidi ya Yanga, akivuna jumla ya mabao 17 na kufungwa 10 amesema amekuwa akiifuatilia timu hiyo tangu alipoondoka, lakini haoni maajabu yoyote yanayoendelea, licha ya kukiri ingizo la wachezaji wapya limeongeza kitu.
Rekodi zinaonyesha tangu Robertinho alipotimuliwa, Simba imecheza mechi tisa, zikiwamo nane ikiwa chini ya mrithi wa Mbrazili huyo, yaani Benchikha na imeshinda mechi tano, imetoka sare mbili na kupoteza pia moja dhidi ya Tanzania Prisons, ikivuna mabao 14 na kufungwa matano, huku mchezo mmoja ulioisha kwa sare dhidi ya Namungo, timu ilikuwa chini ya kocha msaidizi, Seleman Matola na hilo limemwibua kocha huyo wa zamani.
Akizungumza akiwa Brazili, Robertinho amesema licha ya kuondoka kwake bado Simba haijafanikiwa kukaa sawa, huku akitaja hatua ya kujenga timu hiyo ikionekana bado kuipa wakati mgumu timu hiyo.
Amesema Simba bado inahitaji wachezaji wenye ubora zaidi wa kushindania ubingwa, changamoto ambayo hakuisababisha yeye bali ilihitaji nguvu ya kifedha na akili ya kutafuta walio bora tofauti na mitazamo ya mabosi wa Simba walimpofuta kazi kwa kuamini ameshindwa kufanya kazi ipasavyo.
“Huwa naangalia baadhi ya mechi za Simba nikiwa hapa hapa nyumbani nikiwa na muda, bado sijaanza kazi, muda mrefu nautumia kufanya mambo yangu binafsi na kuwa karibu na familia yangu,” amesema Robertinho na kuongeza;
“Nikiangalia Simba naona bado hakuna mabadiliko makubwa, hapo hapo najiuliza kwa nini maamuzi kama yale ya kunifuta kazi yalifanyika, kuna wakati ukweli lazima utangulie. Nimeona timu imeingia robo fainali ikishinda kwa mabao 6-0, lakini hata mimi nilimfunga Horoya hapo hapo kwa Mkapa mabao 7-0 na kutinga robo fainali, ila sikufungwa na Prisons niliishinda ikiwa kwao kwa mabao 3-1 tena kwenye uwanja mgumu na wachezaji wakiwa na uchovu mkubwa.”
Kocha huyo aliyewahi kuzinoa timu kadhaa barani Afrika ikiwao Rayon Sports ya Rwanda, Vipers ya Uganda kabla ya kuonwa na Simba, ameongeza kwa kusema;
“Nikikumbuka na nikiona hali ya timu nabaki kushangaa na kuwaombea mazuri, Simba ni timu yangu, naheshimu maamuzi ya viongozi na kazi ya makocha waliopo, lakini bado sijajua kwa nini wamenifuta kazi na huku timu ikicheza vile vile?”
Akizungumzia usajili mpya uliofanyika kwenye dirisha dogo baada ya kuondoka, amesema bado hajaona kitu kipya sana lakini akiwataka mashabiki kuwapa muda kina Freddy Michael, Pa Omar Jobe, Ladack Chasambi, Edwin Balua, Saleh Kalabaka na Babacar Sarr.
“Nimewaona washambuliaji wawili na vijana wengine wachache, lakini bado hawajaonyesha kitu tofauti labda wanahitaji muda, naomba niseme Simba inahitaji wachezaji bora zaidi kuweza kushindana na timu mbili za juu.
“Nimesikia Onana (Andre) ameumia, namwombea apone haraka ni mchezaji ambaye nilimleta nikiwa najua ataisaidia Simba kwa ubora wake, kule mbele Simba inahitaji watu bora kuliko hawa walilokuja sasa,” amesema kocha huyo aliyeipa Simba jumla ya pointi 18 katika mechi saba alizoiongoza, zikiwa hazitofautiana sana na zile za Benchikha aliyecheza mechi nyingi zaidi na kuifanya Simba sasa ifikishe pointi 36 baada ya michezo 16.
Kabla ya kipigo cha 5-1, Robertinho ndiye aliyevunja unyonge wa Simba mbele ya Yanga kwa kushinda mabao 2-0 mwishoni mwa msimu uliopita kwa mabao ya beki Henock Inonga na mshambuliaji Kibu Denis, aliyefunga pia katika Kariakoo Derby iliyong’oa likiwa bao pekee la Mnyama.
Kabla ya hapo Simba ilikuwa haijaonja ushindi wowote tangu ilipokuwa imeshinda mara ya mwisho Februari 16, 2019 kwa bao la Meddie Kagere, lakini akiwa na rekodi tamu ya kuitambia Yanga tangu akiwa Rayon Sports na Vipers.
Credit:- Mwanaspoti