Droo ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika imepangwa juzi jioni na miamba ya soka nchini, Yanga na Simba zikifahamu wapinzani watakaokutana nao kwenye hatua hiyo.
Yanga imepangwa kukutana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku Simba ikipangwa na Al Ahly ya Misri, lakini Kocha wa wanajangwani, Miguel Gamondi amesema wapinzani wao hao wana ubora sana na wamewekeza lakini hawawaogopi.
Gamondi aliwahi kuifundisha Mamelodi kuanzia Julai, 2005 hadi Oktoba 02, 2006 na akaiwezesha kuchukuwa taji la kwanza la Ligi Kuu Afrika Kusini baada ya miaka sita, akishirikiana na kocha mzawa Neil Tovey.
Kwenye mahojiano yake baada ya droo hiyo, Gamondi amesema anawaheshimu Mamelodi kwa mafanikio waliyopata lakini mwisho wa yote mpira unachezwa na watu 11 kila upande.
“Ukiangalia hata bajeti ya Yanga na Mamelodi ni vitu viwili tofauti, ni timu yenye uwekezaji sana, mfano mwaka jana walichukua mchezaji Argentina kwa pesa nyingi wakati sisi tumesajili Augustine Okrah tena bure, lakini mwishowe wote tuna wachezaji 11 tutaenda kupambana.”
“Tuna malengo ya kuwa moja kati ya timu tano bora barani Afrika na ili kufika huko lazima uzifunge timu kubwa, ni ngumu sana kucheza nao, lakini kila kitu kinawezekana. Naamini tuna wachezaji ambao wana uzoefu wa kucheza mechi za aina hii, ambao wengi walicheza kwenye michuano ya Afcon,” amesema Gamondi ambaye ameiongoza Yanga kwa mafanikio hadi sasa ya kufuzu robo fainali baada ya miaka 25.
Msimu uliopita Yanga ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ikimaliza nafasi ya pili mbele ya USM Algers na kuwa moja ya timu tishio kimataifa na Gamondi anaamini kikosi chake kitapambana kwani uzoefu wa kucheza hatua kubwa tayari wanayo hivyo hawaihofii Mamelodi.
Yanga ambayo ndio vinara wa Ligi Kuu Bara na mabingwa watetezi, ilimaliza nafasi ya pili ya hatua ya makundi nyuma ya Al Ahly na hivyo itaanzia nyumbani mchezo wa robo fainali dhidi ya Mamelodi.
Mchezo wa mkondo wa kwanza unatarajiwa kupigwa kati ya Machi 29 na 30 kisha ule wa marudiano utapigwa kati ya April 05 na 06.