KIKOSI cha Simba leo kinashuka dimbani kwa lengo moja ya kusaka ushindi mnono katika mchezo wao wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly ya Misri.
Mchezo huo utakaochezwa uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam saa 3:00 usiku, dhamila yao ni kusaka ushindi mnono na kumaliza dakika 90 katika dimba lao nyumbani Tanzania kabla ya marudiano nchini Misri.
Katika siku za hivi karibuni timu hizo zimekutana mara sita kila mmoja ameshinda mbili na sare mbili na jumla mabao ya kufunga 14, Simba akifunga tano na Al Ahly tisa.
Timu zote zinahistoria ya kutumia vizuri uwanja wake wa nyumbani Simba inaingia kwenye kumbukumbu za Tangu Mwaka 1993 ilipofuzu hatua ya Robo fainali kwa kumtoa Mpinzani wa muda mrefu wa Al Ahly Klabu ya Zamaleck ya Misri ikiutumia vyema uwanja wake wa Nyumbani Enzi hizo ukiitwa Shamba la Bibi na kuwaacha mdomo wazi Mabingwa hao wa zamani wa Mafarao wa Misri.
Katika hatua Nyengine ni Simba wakizishangaza timu kadhaa kwa kuutumia vyema uwanja wake wa nyumbani kwenye hatua mbalimbali za Michuano ya kimataifa mpaka kufikia kuuita uwanja wao wa nyumbani Machinjioni na kuzaa kaulimbiu maarufu ya kwa mkapa hatoki Mtu.Kutokana na Kukua na kuendelea kwa Mpira wa Tanzania klabu ya Simba imezidi kujizolea Mashabiki lukuki Nchini hasa wachezapo Michuano ya Kimataifa, Nguvu ya upambanaji wao huwaongezea Wapenzi wao hari na hamasa ya kujitokeza kwa wingi uwanjani.
Hii ni Michuano inayobeba kwa hari na hamasa kwa Taifa zima na huwafanya Mashabiki wa soka kupata mguso wa aina yake kuvutika kwenda uwanjani kushuhudia kwa macho yao kile kinachotokea, Al Ahly wao si wageni na hatua hizi kwa yamkini wao wameshiriki Michuano hii mara nyingi zaidi kuliko timu yoyote na wametwaa Makombe mengi zaidi kuzidi klabu zote Afrika wakitwaa mara 11 Ubingwa ligi ya Mabingwa Afrika.
Si wepesi hata kidogo hasa wawapo katika hatua hizi huwa wanabadilika kabisaa mwenendo wao wa kupambania nafasi, wamejaaliwa ubora pia wawapo Nyumbani kwao haijawahi kuwa rahisi hata kidogo wao kupoteza Mchezo katika Dimba la kimataifa la Cairo.
Uwanja wa Benjamin Mkapa wamekutana mara tatu Simba walishinda mechi mbili na kutoka sare mara moja, wakiwa ugenini kwenye dimba la Al Salaam, wamekutana mara tatu Al Ahly kashinda mbili, sare moja.
Katika michezo ya CAF wamekutana mara mbili na zote kutoka sare na Ligi ya Mabingwa Afrika wamecheza mara nne, Simba kashinda mbili na Al Ahly mbili.leo ni mara ya saba wanakutana katika hatua ya robo fainali kila mmoja anahitaji ushindi. Kitu pekee Simba wanachokifikiria ni kuhitaji nusu fainali kufikia mipango hiyo wanalazimika kusaka ushindi na kutaka kumaliza mchezo nyumbani kwa kuwaondoa Al Ahl kabla ya kurudiana.
Kuelekea mchezo huo, Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amesema mechi kubwa kwa timu zote mbili anategemea mazuri kwao kwa sababu wachezaji wanachukuwa tahadhari kubwa kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
Amesema kuna tofauti kubwa waliocheza na Al Ahly akiwa na USM Alger na anakutana na wapinzani huyo akiwa na Simba wakiwa wamejiandaa vizuri kwa ajili ya kusaka ushindi.
“Matokeo ya nyuma ni mengine, timu iliyopo sasa tofauti ya awali, Matokeo ya kesho (leo) ndio yataamua, kila mmoja anatambua ukubwa wa Al Ahly, siwezi kutabiri lakini tumejipanga kwa ajili kwa ajili ya kusaka ushindi.
Nilitamani kuwepo kwa wachezaji wote kuwepo Zanzibar lakini hakuweza kupata kwa sababu ya kalenda ya Fifa Series, hali hiyo nimewaandaa vijana wangu kwa ajili ya kutafuta ushindi mbele ya Al Ahly,” amesema Benchikha.
Ameongeza kuwa Simba imekuwa ikipata mabao mengi nyumbani lakini kwa mchezo wa leo tunahitaji idadi kubwa ya nyumbani ili mechi ya marudiano iwe nyepesi wanapokuwa ugenini.
“Matokeo ya michezo na Al Ahly ambayo aliyoyapata akiwa USM Alger itamsaidia kwa timu aliopo sasa, kuiondoa Al Ahly katika hatua ya robo fainali na kusonga mbele, kuchukuwa mara 11 haituzui kumuondoa Al Ahly katika mashindano kwa sababu nimeongea na wachezaji wangu na wanahitaji hii mechi.
Haiwezekani Simba kukosa matokeo hapa nyumbani, jambo ambalo ni gumu. Dhamana tulioipata kwa mashabiki wa Simba ni deni kubwa kwa benchi la ufundi na wachezaji, naomba wajitokeze uwanjani kwa wingi kwa sababu wanaenda kupigana hadi sekunde ya mwisho kutafuta matokeo ikiwa nyumbani na ugenini,” amesema Benchikha.
Nahodha wa Simba, Shomari Kapombe amesema wamejiandaa vizuri kutokana na maandalizi waliyoyapata wako tayari na wanaimani ya kufanya vizuri katika mchezo wa leo hasa kutumi vizuri katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
“Tumepata muda mzuri wa kujiandaa na kukaa pamoja kama wachezaji, tunaimani kubwa ya kufanya vizuri kikubwa wanasimba wajitokeze kwa wingi uwanjani kuona timu yao inavyofanikiwa katika malengo yetu,” amesema Kapombe.
Ameongeza kuwa anaenda kucheza robo fainali ya tano na malengo yao ni kwenda nusu fainali na kufika huko lazima wapambane leo kusaka ushindi, wanawapa heshima Al Ahly dhamila yao kubwa ni kutumia vema uwanja wa nyumbani.
Amesema katika soka kuna matokeo matatu, lakini kwao ni ushindi kuhakikisha wanapata matokeo mazuri nyumbani na ushindi wa leo utakuwa maalum kwa mashabiki wa Simba.
Kapombe amesema mechi ya leo ni muhimu kumaliza mchezo huo katika Benjamin Mkapa kwa kutafuta ushindi mnono na kutoruhusu bao kikubwa wameandalia zawadi nzuri kwa mashabiki wa Simba na Tanzania.
Kocha Al Ahly, Marcel Koller amesema haitakuwa mechi rahisi kwa sababu wanakutana na timu waliyokutana katika robo fainali ya African Football League (AFL) mara mbili na zote kutoka sare katika michezo yote.
Amesema wanatambua ubora wa Simba na kutokana na kipindi cha hivi karibuni na kuonyeshana ushindani wanatakiwa kuwa makini kuhakikisha wanafanya vizuri katika mchezo wa leo.
“Nimecheza nao mechi mbili na zote nimetoka nao sare, iliwaona na naweza kusema kuwa wapo kwenye level kama yetu na wala sio timu ndogo. Tunawaheshimu na kucheza kwa umakini mkubwa.
Ni kweli tutakosa wachezaji muhimu lakini hatuna presha juu ya kutokuwepo kwao kwa sababu kuna wabadala wao,” amesema Marcel.
Kuhusu kocha Benchikha amesema anamfahamu uwezo wa mwalimu huyo aliwahi kufanya vizuri na makubwa kwenye timu alizofundisha kabla ya kufundisha Simba.