Home Azam FC HIVI NDIVYO DUBE ALIVYOIPIGISHA SHOTI AZAM FC….KOCHA MSENEGAL NAYE AMKATAA MAZIMA…

HIVI NDIVYO DUBE ALIVYOIPIGISHA SHOTI AZAM FC….KOCHA MSENEGAL NAYE AMKATAA MAZIMA…

Habari za Michezo

WAKATI mabosi wa Azam FC wakiendelea kumkomalia mshambuliaji, Prince Dube anayelazimisha kuondoka klabuni hapo, benchi la ufundi na timu hiyo nalo limepata shoti kwa kukosa huduma za Mzimbabwe huyo aliyekuwa amesalia kama straika pekee kikosini baada ya Allasane Diao na Franklin Navarro kuwa majeruhi wa muda mrefu.

Dube aliyeifungua Azam mabao saba hadi sasa ameshaaga klabuni na yupo kwenye harakati za kuvunja mkataba na matajiri hao wa Chamazi, ili msimu ujao awe mchezaji huru, japo mabosi wa klabu hiyo wamemkomalia wakisema bado wana mkataba naye na akitaka kusepa awape tu Dola 300,000 (zaidi ya Sh700 milioni) ili wamuachie.

Maisha lazima yaendelee kwa Azam kucheza sasa bila mshambuliaji huyo akiongeza msala kikosini kwa kukosa huduma za washambuliaji halisi baada ya wenzake wawili kuumia na kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu sasa.

Dube ndiye mshambuliaji kiongozi katika kikosi cha Azam (namba tisa) akiifungia timu hiyo mabao saba na kutoa asisti mbili katika msimu huu, hivyo kuondoka kwake kutaiacha timu ikitegemea zaidi viungo washambuliaji kusaka mabao japo kwa soka la kisasa wala sio ishu sana licha ya ukweli kuwa na mshambuliaji asilia huongeza udambwidambwi uwanjani.

Diao aliumia kwenye mechi ya michuano ya kirafiki wakati akifunga bao kwa kichwa na kuangukia goti, wakati Mcolombia Navarro alipata jeraha la kifundo cha mguu (enka) katika mchezo dhidi ya Simba uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza Februari 9, 2024, baada ya kufanyiwa madhambi na beki Kennedy Juma.

Wachezaji wote hao walipelekwa Afrika Kusini kwa matibabu na inaelezwa watakuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu usiopungua miezi sita, ikiwa na maana hawatakuwepo katika michezo iliyosalia ya Ligi Kuu na Kombe la ASFC, hivyo kujiengua kwa Dube aliyetoa ‘Thank You’ mtandaoni kuishukuru Azam ni wazi kumeongeza mzigo kwa benchi la ufundi.

Awali, ilionekana kama Dube alisharejesha majeshi nyuma kwa kuamua kwenda mazoezini mapema wiki hii na kuzungumza na kocha mkuu, Youssouf Dabo kabla ya siku iliyofuata kuelezwa alienda kumpa matumaini tu kocha huyo kwa kumheshimu na kumueleza sababu zinazomuondoa kisha kukomaa na msimamo wake wa kuikacha timu.

WATATU WAULA

Kutokana na kukosekana kwa mastraika hao watatu, hususani Dube aliyekuwa amebeba matumaini ya timu hiyo kwenye eneo la ushambuliaji katika kutimiza ndoto za kupata ubingwa wa pili wa Ligi Kuu Bara baada ya ule wa msimu wa 2013-2014, kocha Dabo kaamua kuwapa kazi viungo washambuliaji watatu kuziba mapengo yaliyopo.

Kocha huyo kutoka Senegal ameamua kuwatumia wachezaji hao watatu tofauti katika eneo hilo kwa nyakati tofauti na tayari wameanza kazi hiyo katika mechi nne zilizopita.

Mawinga Ayoub Lyanga na Abdul Sopu na kiungo mshambuliaji Djibril Sillah ndio wamepewa kazi ya kuziba pengo la Dube wakati huu ambapo Navarro na Diao hawapo. Pia amekuwa akimuingiza Kipre Junior kuchukua nafasi ya mmoja kati ya watatu ambao ambao anaanza nao katika kikosi cha kwanza.

Ikumbukwe kwa mara ya mwisho Dube kuichezea Azam ilikuwa Februari 19, mwaka huu alipoingia uwanjani katika dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Sillah kwenye mechi ya ligi dhidi ya Tabora United iliyomalizika kwa suluhu.

Hivyo, Sillah, Lyanga na Sopu walianza kuvaa viatu vya Dube rasmi kwenye mechi dhidi ya Tanzania Prisons (1-1), kisha wakafuata na Singida Fountain Gate (1-0), Dodoma Jiji (4-1) na Coastal Union (1-1). Kiufupi ni mechi nne zilizopita.

Katika mechi na Prisons iliyomalizika kwa sare ya mabao 1-1, Azam ilimuanzisha Sopu kama mshambuliaji kinara lakini dakika ya 63 alitolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Cheikh Sidibe. Baada ya Sopu Kutoka, Sillah aliyekuwa akicheza eneo la kiungo alisogea juu na kucheza kama mshabuliaji kinara.

Mchezo uliofuata dhidi ya Singida ambao Azam ilishinda 1-0 kwa bao la Kipre Junior, Azam ilimuanzisha Lyanga kama mshambuliaji kinara, lakini dakika ya 84 alitoka na kuingia beki Nathanael Chilambo, lakini kabla ya hapo Sopu alikuwa ameingia dakika ya 75 akichukua nafasi ya Iddi Selemani ‘Nado’, hivyo baada ya Lyanga kutoka Sopu alisimama namba tisa.

Mechi iliyofuata dhidi ya Dodoma, Azam ikishinda 4-1 kwa mabao ya Lyanga, Kipre, na Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mara mbili, Azam ilianza na Lyanga kama namba tisa na alicheza kwa dakika zote 90 akafunga na kutoa asisti moja, pia sopu aliingia katika dakika ya 77 kuchukua nafasi ya Fei hivyo akawa anacheza kwa kuswichi nafasi kati yake na Lyanga.

Mchezo wa mwisho kwa Azam dhidi ya Coastal uliomalizika kwa sare ya mabao 1-1, Fei akiifungia Azam na Charles Semfuko kuifungia Coastal, Lyanga ndiye alianza kama mshambuliaji kinara lakini katika dakika ya 73 alimpisha Sopu.

Hadi sasa Azam imefunga jumla ya mabao 45 kwenye ligi, lakini mengi yamefungwa na mawinga na viungo hali inayoonyesha timu hiyo haimtegemei zaidi mchezaji mmoja.

Kiungo Fei Toto ndiye kinara wa upachikaji mabao kwenye ligi kwa sasa akiwa amecheka na nyavu mara 12, huku anayefuata ndani ya Azam kwa mabao akiwa Dube aliyeondoka akiwa amefunga saba.

Winga Kipre Junior amefunga sita na kuasisti manane akiwa mchezaji wa pili kuhusika kwenye mabao mengi katika Ligi baada ya Fei Toto, huku kiungo Sillah amepachika mabao manne sawa na winga Idd Seleman ‘Nado’, kiungo Sospeter Bajana aliye majeruhi amefunga matatu huku Lyanga akiwa nayo mawili na wengine wachache wakmefunga moja moja.

Azam kwa sasa ipo kileleni mwa msimamo wa ligi na alama 44 ilizovuna kwenye mechi 20, na mechi ijayo itakuwa nyumbani Machi 17, mwaka huu kuikaribisha Yanga.

MSIKIE DABO

Kocha Dabo amesema kuwa anatambua umuhimu wa Prince Dube kikosini kwake lakini kukosekana kwake haliwezi kuwa pengo kwani tayari ana wachezaji wengine wanaofanya vizuri.

“Tumemkosa kwenye mechi nne dhidi ya Tanzania Prisons tukamaliza mchezo kwa sare ya bao 1-1, tumeshinda 1-0 dhidi ya Singida Fountain Gate, tukashinda 4-1 dhidi ya Dodoma Jiji na tumetoka sare ya 1-1 dhidi ya Coastal Union. Wachezaji waliopo wamefanya vizuri,” amesema kocha huyo na kuongeza;

“Azam ina wachezaji wengi na kila mmoja anatamani kupata nafasi ya kucheza hivyo naamini waliopo watafanya vizuri eneo hilo bila kujali kutokuwepo kwa Dube.”

Dube alisajiliwa na Azam mwaka 2020 kutoka Highlanders ya Zimbabwe na kumaliza msimu wa kwanza akiwa na mabao 14 akicheza katika mechi 11 tu kabla ya kupata majeraha na msimu uliopita aliorudi kwa kasi alifunga mabao 11 katika mechi 11 na msimu huu ameanzisha mgomo baridi akiwa na mabao saba katika mechi 9.

SOMA NA HII  FT: YANGA 2-0 NAMUNGO FC.....AZIZ KI AMJIBU CHAMA KIBABE...MUSONDA NI 'PAPATUPAPATU' TU...