Home Taifa Stars TAIFA STARS IJIPANGE UPYA, LIGI INAREJEA MIPANGO MUHIMU

TAIFA STARS IJIPANGE UPYA, LIGI INAREJEA MIPANGO MUHIMU


TAYARI ratiba ya mechi za Ligi Kuu Bara imewekwa wazi na mzunguko wa 19 unatarajiwa kurejea ndani ya ardhi ya Bongo.

Tayari zipo  mechi za viporo ambavyo vilitokana na timu mbili kuwa kwenye mashindano ya mechi za kimataifa ambazo ni Namungo FC pamoja na Simba.

Kwa jana kila mmoja ameweza kushuhudia namna timu hizo zilivyojuwa zikisaka ushindi ndani ya uwanja na mwisho wa siku kila mmoja akapata kile ambacho alikuwa anahitaji.

Kwa upande wa Namungo FC wao wapo kwenye hatua ya 32 bora Kombe la Shirikisho huku Simba wakiwa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kupenya kwenye hatua za mwanzo walizoanza nazo.

Kwa hatua ambayo wameweza kufika kwa sasa wanastahili pongezi kwani sio kazi rahisi kuwa hapo. Yote kwa yote na wadau pia ikiwa ni pamoja na mashabiki nao pia wanastahili pongezi kwa kutoa sapoti kwenye mechi ambazo zilikuwa zinachezwa uwanjani.

Pia iwe somo kwa wakati ujao kwa wale ambao wanapanga ratiba kupiga hesabu kwamba timu zetu kwa sasa zimeweza kufikia hatua ya mashindano makubwa hivyo wawe wanawapigia hesabu mpaka kwenye hatua ya makundi na sio kwenye hatua za awali.

Licha ya kwamba viporo haviwezi kuepukika ila inaonekana ratiba mara nyingi inaishia kwenye mechi za kimataifa za awali na kusahau kwamba kuna uwezekano timu ikaweza kusonga hatua ya mbele na kuweza kuendelea kuperusha bendera ya Tanzania.

Wakati ujao itapendeza ikiwa ratiba itakuwa rafiki ili kupunguza hivi viporo kwa kuwa vinatibua mipango ya kwenye ligi.

Itakuwa vema ikiwa kila timu ikaaza maandalizi kwa sasa kabla ya ligi kurejea kwa kuwa huu ni mzunguko wa pili ambao unatoa maamuzi nani atakuwa nani ndani ya ligi.

Kwa wale ambao walikuwa kwenye mwendo mbovu kwenye mzunguko wa kwanza kwa sasa ni wakati wao kuweza kujipanga upya ili waweze kufanya vizuri.

Inawezekana ikiwa kila mmoja akaamua kwamba kwa sasa ni wakati wa kuendelea kupambana kwa ajili ya taifa pamoja na timu kiujumla.

Ukiweka kando maandalizi ya Ligi Kuu Bara pia ni muhimu kwa timu yetu ya Taifa ya Tanzania kuanza mipango upya kwa ajili ya wakati ujao.

Tumepoteza nafasi ya kutinga hatua ya robo fainali kwenye michuano ya Chan ambayo imemalizika nchini Cameroon.Hili ni mbaya kwetu kwa kuwa wachezaji walituahidi kwamba wanakwenda kupambana.

SOMA NA HII  STARS KULAMBA BILIONI 17 ZA AFCON....ISHU NZIMA IKO HIVI....

Kutolewa na pointi nne ni mbaya ila kwenye mchezo hakuna cha kubadilisha kwa sasa. Karata yetu tuliichanga vibaya kwenye mchezo wa kwanza. Kufungwa na Zambia tena mabao 2-0 mchezo wa ufunguzi ilikuwa ni hatua mbaya.

Dakika 90 za mwisho ambazo zilikuwa zimeshika funguo ya ushindi nazo zilimeguka huku timu ikishindwa kupata matokeo. Ilikuwa ni huzuni kwa Watanzania kiujumla ila kwa kuwa imetokea hakuna namna.

Wakati ujao ni muhimu kujipanga ili kufanya vizuri kwenye mechi za mwanzo ili kuongeza hali ya kujiamini. Kila mmoja ni muhimu kuwa na mipango makini pamoja na utayari wa kufanya makubwa.

Mambo mengi tumeyakosa kwa sasa ila yanapaswa kuwa funzo kwetu kiujumla na kila mmoja ambaye atakuja kuitwa ndani ya Stars ili kupata matokeo wakati ujao.

Mashabiki furaha yao ipo kwenye kupata ushindi ila kwa kuwa hakukuwa na ushindi basi ni ganzi ndani ya mioyo ya mashabiki na taifa la Tanzania kiujumla.

Kushindwa kutinga hatua ya fainali kumezima ndoto za wachezaji wengi kuweza kusonga mbele kwenye mashindano ya kirafki na yale ya ushindani.

Ile nafasi ya wachezaji kuweza kuingia sokoni imeyeyuka hivyo kwa sasa ni muda wa kuendelea kupambana kwa kuwa ligi inarudi.

Muda mwingine ukifika iwe kazi ni moja kujitoa kuanzia mchezo wa kwanza ambao huwa unakuwa umeshika furaha ya ushindi kwenye mechi zetu.

Kupoteza mbele ya Zambia iwe funzo kwa kuwa mechi mbili tulionekana kuzinduka ila tulikuwa tumechelewa na wachezaji walishindwa kulinda ulinzi kutokana na tatizo la kukosa uzoefu.

Kikosi cha ushindi kianze kuandaliwa wakati huu kwa kuwa ni muhimu kila mchezaji kujipanga na kujiweka vema kwa ajili ya mechi zote za ushindani.

Benchi la ufundi pia linapaswa lianze kutafuta mechi za kirafiki na kikosi chenye ushirikiano zaidi kuliko kwenda na kikosi kipya ambacho kinakuwa na wachezaji wale ambao hawana uzoefu.

Haina maana kwamba wachezaji wapya wasipewe nafasi hapana hapa ninamaanisha kuwa na wachezaji ambao wana uzoefu na mechi za ushindani itaongeza nguvu kwenye ushindani.