Home Habari za michezo HIVI NDIVYO DUBE ANAVYOZIGONGANISHA SIMBA NA YANGA…ISHU YAKE YAPAMBA MOTO…

HIVI NDIVYO DUBE ANAVYOZIGONGANISHA SIMBA NA YANGA…ISHU YAKE YAPAMBA MOTO…

Habari za Michezo

Prince Dube ameendelea kuzivuruga Simba na Yanga. Mashabiki wa klabu hiyo wamegawanyika kwa sasa baada ya kuibuka kwa taarifa nyota huyo aliyeigomea Azam FC, anatamani kuichezea Yanga, huku uongozi ukiweka bayana Simba imetuma ofa ya kumsajili sambamba na Al Hilal.

Ipo hivi. Dube alianza kuhusishwa na Yanga mara baada ya kudaiwa kugoma kuambatana na timu kwa baadhi ya mechi za mikoani na kuonekana Kwa Mkapa wakati vijana wa Jangwani wakimgonga Mwarabu 4-0.

Dube aliibuka uwanjani hapo wakati Yanga ikiifumua CR Belouizdad katika mechi za makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikaelezwa ni mgomo wa kushinikiza kutaka aondoke Azam.

Akadaiwa kurudisha kila kitu cha klabu hiyo na kupeleka mezani Dola 200,000 (zaidi ya Sh500 milioni) ili kuilipa klabu kwa kuvunja mkataba uliosalia.

Hata hivyo, mabosi wa Azam uliibuka na kukanusha Dube amesaliwa na mkataba mfupi. Mabosi hao walisisitiza Azam ina mkataba na Dube hadi mwaka 2025, ila hawana noma kumwachia iwapo tu, jamaa atawalipa Dola 300,000 (zaidi ya Sh700 milioni).

Pia walienda mbali na kusema milango i wazi kwa klabu yoyote inayomhitaji mchezaji huyo, muhimu ni wao kwenda kuzungumza nao na kuwalipa kiasi wanachokihitaji kumwachia Dube.

Siku chache baadaye, Azam ilitoa taarifa imepokea ofa kutoka klabu mbili za Simba na Al Hilal ya Sudan kutaka kumsajili Prince Dube aliyewavuruga hivi karibuni.

Taarifa hizo, zilijibiwa na watu wa upande wa Dube, wakimkariri nyota huyo akisema hana mpango na ofa za klabu hizo, kwani anapotaka kucheza anapajua yeye na hawezi kulazimishwa pa kwenda.

Lakini wakati hali ikiwa hivyo kwa kutokuwepo kwa usahihi wa mahali gani nyota huyo aliyefunga mabao saba katika Ligi Kuu kwa msimu huu ataibukia, tayari ameshawagawa mashabiki wa klabu za Samba na Yanga.

Baadhi ya mashabiki wa klabu hiyo wakipiga chapuo kwa viongozi wao kumalizana mapema na Azam ili jamaa atue kikosini na kuliamsha kama alivyokuwa akifanya alipokuwa Chamazi.

Pia wapo wengine wanaomkataa na kutoa sababu kwa nini klabu hizo zinapaswa kuachana naye hata kama ni bonge la mchezaji.

Haya hapa maoni lukuki ya wasomaji wakitoa msimamo wao juu ya nyota huyo na kuhusishwa na klabu hizo wanazoshabikia na limeamua kuyachapa kuonyesha namna alivyowagawanya mashabiki wa Simba na Yanga wengine wakimtaka na wengine wakimkataa.

Hata hivyo, wale wanaomtaka atue wanaweka bayana, ujio wa Dube kwa Simba utasaidia kuimarisha eneo la mbele la timu hiyo kwani washambuliaji wa sasa Freddy Koublan na Pa Omar Jobe waliosajiliwa dirisha dogo ni kama wamefeli mapema kabla hata hawajamaliza mtihani.

Kwa wale wa Yanga wanasema mwamba huyo akitua ataenda kuvivaa na kuvimudu viatu vilivyoachwa klabuni na Fiston Mayele aliyepo Pyramids, kwani awali Hafiz Konkoni alichemka na hata waliopo sasa, Joseph Guede, Kennedy Musonda na Clement Mzize kiatu kimewapwaya mno.

Kwa aina ya vikosi vya Kocha Miguel Gamondi wa Yanga na Abdelhak Benchikha wa Simba, Dube anafiti vizuri tu, kwa rekodi alizonazo ndani ya misimu minne aliyoichezea Azam iliyomsajili kutoka Highlangers ya Zimbabwe inayohusishwa pia kumtaka kumrejesha kikosini.

Licha ya kumudu kucheza kama mshambuliaji namba mbili na wakati mwingine akitokea pembeni, lakini Dube ni mshambuliaji wa mwisho, hivyo kwa vikosi vyote vya Simba akipangwa na kuanza analiamsha kama kawaida na kuwapa raha mashabiki wa timu hizo kongwe nchini.

Kama Dube akitua Simba inawezekana Benchikha akaanza langoni na Ayoub Lakred, Shomary Kapombe, Mohammed Hussein, Che Malone, Henock Inonga, Babacar Sarr, Fabrice Ngoma, Sadio Kanoute, kisha akamtupa Dube asimame mbele na Clatous Chama na Saido Ntibazonkiza.

Kwa upande wa Yanga kama itafanikiwa kumvuta kikosini, basi Gamondi anaweza kulipanga jeshi upya kwa langoni kusimama, Diarra Djigui, Yao Kouassi, Joyce Lomalisa, Ibrahim Bacca, Dickson Job, Khalid Aucho, Maxi Nzengeli, Mudathir Yahya, Prince Dube, Pacome Zouzoua na Stephane Aziz KI.

SOMA NA HII  MAN UNITED WAFUNGA RASMI JALADA LA POGBA OLD TRAFORD....JUVENTUSI YAJIWEKA SAWA KUMPOKEA...