Home Habari za michezo KUHUSU AL HILAL KUSHIRIKI LIGI YA BONGO…UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA…WATALIPA MIL...

KUHUSU AL HILAL KUSHIRIKI LIGI YA BONGO…UKWELI UNAOPASWA KUJUA HUU HAPA…WATALIPA MIL 230 KUPATA KIBALI…

Habari za Michezo leo

Mabosi wa Al Hilal ya Sudan itawabidi kuingia mfukoni na kulipa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kikosi cha wachezaji 38 pamoja na benchi la ufundi ili kupata idhini ya kucheza michezo ya Ligi Kuu Bara msimu ujao wa 2024-2025.

Pamoja na kwamba bado Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) linaendelea na vikao vyake juu ya namna nzuri ambayo wababe hao wa Sudan watashiriki Ligi Kuu Bara kwa kipindi kifupi kutokana na maombi waliyowasilisha mapema kutokana na mzozo mkali wa kisiasa za kijeshi unaondelea nchini kwao.

Kwa sasa timu hiyo ipo kambini Cairo Misri, ikipigwa tafu na Al Ahly itakayokuja kucheza na Simba katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayopigwa Ijumaa Uwanja wa Benjamin Mkapa, kuanzia saa 3:00 usiku kabla ya kurudiana wiki ijayo kusaka ya kwenda nusu fainali.

Hivi ndivyo namna ambavyo mabosi wa Al Hilal itawabidi kuingia mfukoni na kulipa mamilioni hayo kwa ajili ya wachezaji na benchi la ufundi, ili kupata vibali kutoka kwenye mamlaka tatu tofauti ambazo ni Idara ya uhamiaji inayotoa kibali cha makazi, Wizara ya Kazi na Ajira inayotoa vibali vya kazi na Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) ambalo hutoa leseni kwa wachezaji isipokuwa makocha na waajiriwa wengine kama vile maofisa ambao sio wachezaji.

Al Hilal yenye jumla ya wachezaji 38 kati ya hayo 27 ni wazawa (Sudan), huku 11 wakiwa wa kigeni kutoka mataifa ya Ivory Coast (2), Senegal (3), Mauritania (1), DR Congo (3), Burundi (1) na Zambia (1), inatakiwa kulipa jumla ya Dola 15,500 (zaidi ya Sh39.3milioni) kwa wachezaji 31 ambao wanatoka kwenye mataifa ya ukanda wa Afrika Mashariki.

Habari za MichezoMchezaji mmoja kutoka mataifa ya ukanda huu kibali chake kutoka idara ya uhamiaji ni Dola 500, lakini kwa wachezaji wa mataifa mengine na Ulaya ni Dola 2000, hivyo watatakiwa kulipa tena dola 14,000 (Sh35.5milioni) kwa nyota saba ambao wanatoka kwenye mataifa ya Senegal, Mauritania na Ivory Coast.

Jumla kwa upande wa vibali vya makazi tu, mabosi wa Al Hilal watatakiwa kutoa zaidi ya Sh74.8milioni hapo bado Dola 1000 kwa wachezaji wote (Sh2.5 milioni) kupata vibali vya kazi huku kwa upande wa TFF wenyewe wakikamua Sh4 milioni kwa mchezaji wa kigeni hivyo kwa idadi ya wachezaji waliyonao hapo ni Sh152 milioni.

Kwa kuzingatia taratibu zote kama ambavyo Simba na Yanga zimekuwa zikifanya kwa wachezaji wake wa kigeni, basi mabosi wa Al Hilal watatakiwa kulipa Sh229.3 milioni na hapo bado watakuwa wanakabiliwa na gharama za usafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine bado kulipa mishahara ya wachezaji na malazi, vichwa vinaweza kuwauma.

WASIKIE UHAMIAJI

Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji Tanzania na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano Mrakibu wa Uhamiaji, Paul John Mselle alisema; “Bado hatujapata taarifa rasmi za ujio wa timu hiyi kutoka Sudan na kama wapo basi tutafuatilia kuanzia Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo ili kujua wamewapa masharti gani maana tunafahamu nchini kwao hakuko salama.”

“Na baada ya hapo tujue hiyo timu ina wachezaji wangapi kutoka Sudan na wangapi sio raia wa Sudan ndipo vibali vya makazi vitolewe maana kuna utaratibu na gharama tofauti za kulipua vibali vya makazi,” alisema Msele na kuongeza;

“Pia tuwasiliane na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ili kufahamu watacheza hiyo ligi kwa misimu mingapi na kanuni zao zinasemaje, suala la kanuni nadhani sio gumu sana maana ni kukaa na kujadiliana na kukubaliana kuona ni namna gani wataziboresha ili hiyo timu ishiriki, hivyo yote kwao huenda yakawezekana.

“Hivyo nadhani kiundani zaidi nitakuwa nimelijua hadi wiki ijayo baada ya kufuatilia maeneo yote hayo maana sina uhakika kama wapo nchini ama bado hawajaja huenda hizi ni hatua za awali kabla hawajafika.”

BODI YA LIGI

Mkurugenzi Mtendaji wa TPLB, Almas Kasongo ameonyesha matumaini ya kufanyiwa kazi kwa haraka jambo hilo kutokana na vikao vinavyoendelea huku akihudhuria kama mjumbe. “Sekretarieti ya TFF ikiongozwa na katibu wanawajibu wa kukaa na kuchakata wakijiridhisha wanapeleka katika kamati ya utendaji,” alisema na kuongeza;

“Wanapokea, wanajadili na kufanya maamuzi, kwa hiyo nisingependa kuwa msemaji katika hilo kama mtendaji mkuu, nahudhuria kwenye kikao hicho lakini kama Sekretarieti na sio kama mjumbe pale kunapokuwa na jambo la ligi kwa ajili ya ufafanuzi.”

ITAKUWAJE?

Habari za Michezo leoHaya ni maswali matano kuhusu ushiriki wa Al Hilal msimu ujao katika Ligi ya Bara ambayo pia yamekuwa vichwani mwa wadau mbalimbali wa soka nchini wamekuwa wakijiuliza wakati huu ambao bado TFF haijaeleza kwa kina juu ya namna itakavyokuwa kutokana na vikao vinavyoendelea.

Wanachezaje bila ya kuwa kwenye msimamo? Kwa mujibu wa taarifa zilizopo ni Al Hilal haitakuwa sehemu ya msimamo lakini michezo yao itakuwa kwenye ratiba kama ilivyo michezo mingine.

Mechi zao zitapewa uzito? Ikiwa hawatakuwa sehemu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara kama inavyoelezwa, wanaweza wasipate kile ambacho wamelenga kukipata kwenye ligi maana klabu mbalimbali zinaweza zisiupe uzito mchezo huo na miongoni mwa sababu ambazo zimeisukuma timu hiyo kushiriki ligi kuu ni ushindani uliopo.

Mfumo wa mechi zao? Je! watakuwa wakicheza nyumbani na ugenini kama ilivyo kwa timu nyingine kwenye ligi, maskani yatakuwa Dar kama ilivyo kwa Simba, Yanga, Azam FC na KMC au la.

WATAPATA MGAWO WA UDHAMINI?

Fungu la udhamini katika Ligi Kuu Bara ambalo limekuwa likitolewa kwa mafungu kwenye kila msimu, husaidia katika uendeshaji wa klabu, watashiriki huku wakijigharimikia wenyewe au nao watakuwa sehemu ya mgawo kama ilivyo kwa timu nyingine.

Gharama itakuwaje? Kitendo cha timu kuongezwa kwenye ratiba ya msimu ina maana klabu husika zitaingia ghamara zaidi ya bejeti zao ambazo wamekuwa wakiziweka kwa msimu mzima je itakuwaje kwenye hilo au kutakuwa fungu maalumu ambalo TFF na wadhamini watalitoa kwa ajili ya kufanikisha hilo.

KWA WENZETU

Yapo mataifa mengi huko Ulaya ambayo yalizikaribisha timu kutoka nchi nyingine na zikashiriki Ligi Kuu kutokana na sababu mbalimbali, mfano mzuri ni Union Esportiva de Bossost ya Hispania ilienda Ufaransa.

Timu hii iko katika Bonde la Aran huko Catalonia, Uhispania Kaskazini, na inashindana Ufaransa kutokana na hali ya hewa. Theluji ya majira ya baridi imekuwa kikwazo kwao kusafiri kwa kwenda katika maeneo mengi ya nchi hiyo hivyo ni rahisi kwao kwenda Ufaransa.

Mfano mwingine mzuri ni kwa FC Busingen ya Ujerumani iligonga hodi Uswisi, hii ndio timu pekee kutoka Ujerumani kucheza nchi nyingine.

Kulingana na maelezo ya Busingen, hicho ni kipande cha ardhi ambacho ni sehemu ya Ujerumani, lakini kipo Uswisi, klabu hiyo inashindana katika mfumo wa Ligi ya Uswisi hata England zipo timu kutoka Wales na Scotland ambazo zinashiriki katika ngazi tofauti ya ligi nchini humo na wanachukuliwa kama zilivyo timu nyingine kwenye ligi hizo.

WAJE TU

Mkurugenzi wa Bodi ya Ihefu, Muhibu Kanu alisema; “Kwangu naona ni jambo zuri, tunapata changamoto mpya, mpira ni kazi kama kazi nyingine, unahitaji kupata mawazo mapya na uzoefu kutoka kwa watu wengine walioendelea kwa hiyo, tunawakaribisha.”

Kwa upande wa Katibu wa Prisons, Ajabu Kifukwe alisema; “Kwa upande wangu sina shida na hilo nimepokea kwa mikono miwili maana kwanza lazima ujue sababu ya wao kuomba kuja kwetu ni nini? Shida ni amani kukosekana kwao sasa kama jibu ni hilo tunaangalia katika nyanja mbili moja ya upande wa michezo pili la upande wa usalama,”

“Ikumbukwe Tanzania ni moja nchi wanachama wa UN na kuna mikataba mbalimbali wamesaini ikiwa ni pamoja na shida na raha sasa hapa tutaongelea kwenye shida, angalia kwa mfano sisi timu inatoka Mbeya mpaka Kagera au Lindi mpaka Tanga bila kusindikizwa na msafara wowote kwa kuwa nchi yetu ina amani, lakini kwa upande wao hiki kitu hakipo kabisa.”

CREDIT;- MWANASPOTI

SOMA NA HII  FEISAL SALUM ATEMBEZA BONGE MOJA YA MKWARA