Home Habari za michezo A-Z JINSI MAHAKAMA ILIVYOBARIKI BOCCO KULIPWA MIL 200 KUTOKA BILIONI 1 ZA...

A-Z JINSI MAHAKAMA ILIVYOBARIKI BOCCO KULIPWA MIL 200 KUTOKA BILIONI 1 ZA MADAI…

Habari za Simba SC

MAHAKAMA Kuu ya Tanzania, imeiamuru Kampuni ya Michezo ya Kubahatisha ya Princes Leisure (T) Ltd ya jijini Dar es Salaam, kumlipa straika na nahodha wa Simba, John Bocco, Sh200 milioni kwa kutumia picha yake katika tangazo la biashara.

Hukumu hiyo imetolewa na Jaji Irvin Mugeta wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam na kuanza kusambaa katika mitandao ya kijamii juzi jioni na kuibua mijadala, huku baadhi wakisema imeweka msingi wa haki kwa wachezaji.

Awali mchezaji huyo alikuwa ameiomba mahakama iiamuru kampuni hiyo kumlipa Sh1 bilioni kama fidia, kutokana na ilitumia picha yake bila kuwa na mamlaka nayo na kumlipa mrabaha wa asilimia 25 kipindi chote ilichoitumia.

Tangazo hilo likiwa na picha ya nyota huyo lililotolewa katika ukurasa wa Instagram wa kampuni hiyo kati ya Novemba 18, 2021 hadi Desemba Mosi, 2021 na ujumbe huo ulisomeka katika mtandao huo wa kijamii ukisema;

“Uhondo wa Ligi NBC unaendelea leo kwa mechi 3. Kubwa zaidi ni Simba watakuwa wageni wa Ruvu Shooting huko Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kirumba. Siku za Pesa zimerejea.”

Bocco katika kesi hiyo aliyowakilishwa na mawakili Innocent Michael na Gadi Kabele, alisema kutumiwa kwa picha yake kulimaanisha amevunja mkataba na Simba na timu hiyo ilikuwa iko mbioni kumchukulia hatua za kinidhamu.

Kesi hiyo namba 118 ya mwaka 2022 ilisikilizwa upande mmoja (ex parte) kwa vile mdaiwa aliondolewa katika mwenendo wa shauri hilo baada ya kushindwa kuwasilisha utetezi kwa maandishi kwa muda ulio ndani ya sheria.

Kesi hiyo ilisikilizwa na Jaji Mugeta Agosti 25,2023 na hukumu ikatolewa Agosti 31 na nakala ya hukumu hiyo kuwekwa katika mtandao wa mahakama (Tanzill) mahsusi kwa ajili ya kuchapisha maamuzi, sheria na kanuni bure mtandaoni.

Jaji alisema katika kesi hiyo, Bocco alitoa ushahidi kuwa hakuwahi kuipa idhini kampuni hiyo kutumia picha yake na hakuwa na makubaliano ya kibiashara na kampuni hiyo, hivyo inathibitisha ilitumia picha bila idhini yake.

“Kama alivyoeleza mdai (Bocco) kitendo hicho kilihatarisha kibarua chake hasa ikizingatiwa vifungu vya mkataba kuhusiana na matangazo na masuala ya kibiashara,” alisema Jaji Mugeta katika hukumu hiyo na kuongeza;

“Kama wakili wake alivyojenga hoja hapa mahakamani, kampuni hiyo ilikiuka ibara ya 16 ya Katiba ya Tanzania ya 1977.”

Jaji Mugeta wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam alisema kwa kilichofanyika, Bocco anastahili fidia iliyo ndani ya mamlaka ya mahakama na mdai ameomba kulipwa fidia ya Sh1 bilioni lakini ni kiwango kikubwa, hivyo kwa kuzingatia wasifu wa mchezaji huyo aliamuru alipwe fidia ya Sh200 milioni. Jaji alisema ombi la kulipa mrabaha sio ya kweli (unrealistic) kwa kuwa hakuna kielelezo cha ushahidi kilichowasilishwa mahakamani.

SOMA NA HII  MOSES PHIRI AWAAGA WACHEZAJI WENZAKE ZAMBIA...MENEJA WAKE AFUNGUKA TIMU ATAKAYOICHEZEA TZ...