Home Habari za michezo MAMBO YAZIDI KUWA MAGUMU KWA KELVIN JOHN NDANI YA KRC GENK…

MAMBO YAZIDI KUWA MAGUMU KWA KELVIN JOHN NDANI YA KRC GENK…

Habari za Michezo leo

CHATI ya maendeleo ya mshambuliaji wa Kitanzania, Kelvin John anayecheza soka la kulipwa KRC Genk ya Ubelgiji kwa sasa inaonekana kushuka chini badala ya kupanda kama ilivyotarajiwa na wengi jambo ambalo linaonekana kuwa hatari kwa kipaji chake.

Nini tatizo? Kwani kama unakumbuka kuna kipindi alipandishwa kwenye kikosi cha kwanza cha KRC Genk, msimu wa 2021/22 na akapata nafasi ya kucheza mchezo wake wa kwanza kwenye ligi ya Ubelgiji dhidi ya KAS Eupen na huu ni msimu wa tatu sasa hakuna hatua yoyote aliyopiga mshambuliaji huyo.

Mbaya zaidi, hata upande wa timu ya taifa la Tanzania ‘Taifa Stars’ amefungiwa vioo na Kocha Adel Amrouche na alieleza kabla ya kufungiwa kule Ivory Coast kwenye fainali za Afcon kuwa kinda huyo ni mtovu wa nidhamu.

Turudi Ubelgiji, wakati aliposajiliwa rasmi na KRC Genk alitajwa kama miongoni mwa wachezaji ambao wanaweza kuvaa viatu vya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta kwa miaka michache ijayo kwenye kikosi hicho.

Samatta ambaye kwa sasa yupo zake Ugiriki alikaa na Kelvin kwa kipindi kirefu Ubelgiji na ndiye anayetajwa kuwa sehemu ya uhamisho wa kinda huyo kwenye klabu hiyo kutokana na ushawishi alionao, ni miongoni mwa wachezaji wenye heshima kubwa kwenye klabu hiyo kutokana na yale ambayo ameyafanya.

Tofauti na wachezaji wengine ambao hupandishwa na kupigania nafasi kwenye kikosi cha kwanza hadi kutoboa, Kelvin alipandishwa na mambo yalipokuwa magumu na imebidi atumike kwenye ligi ya wachezaji wa akiba kwa lengo la kuboresha kiwango chake kwenye ligi hiyo na msimu huu amefunga mabao mawili na kutoa asisti tano.

Kikosi cha pili cha KRC Genk ‘Jong Genk’ kinashiriki ligi daraja la kwanza ‘Challenger Pro League’, na amekuwa akicheza ligi hiyo kwa msimu wa tatu.

MKATABA UNAISHA
Mimi na wewe hatujui mabosi wa KRC Genk watakuwa wanawaza nini kuhusu Kelvin maana mkataba wake unamalizika Juni mwaka huu, je! wataendelea kuwa na imani naye au watamfungulia mlango wa kutokea ili akatafuta changamoto mpya ya soka sehemu nyingine kama ilivyo kwa makinda wengine ambao hushindwa kuonyesha makali yao?

Hilo ni suala la muda tu lakini kwa hali ilivyo, Kelvin anatakiwa kupambania ugali wake vinginevyo anaweza kujikuta katika mazingira magumu zaidi.

Kwa mujibu wa kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael ambaye kwa sasa yupo nyumbani kwao Ubelgiji, anaamini kinda huyo ana nafasi ya kubadili upepo wa mambo na kufanya vizuri kama ilivyokuwa kwa Samatta.

“Amebahatika kupata nafasi mapema ya kuingia Ulaya, anatakiwa kupambana kwa sababu klabu huzalisha wachezaji wengi wenye vipaji, hivyo ukisinzia ni rahisi mchezaji mwingine kukuzidi kete na kupewa nafasi ndivyo ilivyo,” anasema.

WENZAKE WAMEPENYA
Wakati mambo yakiwa sio shwari kwa Kelvin, Bilal El Khannouss ambaye ni mchezaji wa kimataifa wa Morocco mwenye umri wa miaka 19, amepenya kwenye kikosi cha kwanza cha KRC Genk na msimu huu amepata nafasi kwenye michezo 25 kwenye ligi.

Bilal ambaye ni kiungo mshambuliaji ameifungia Genk mabao mawili na kutoa asisti tano, ni kati ya wachezaji vijana zaidi ambao wanafanya vizuri kwenye kikosi hicho cha kwanza huku Kelvin akisota kwenye orodha ya wachezaji wa akiba.

Jina la Kelvin halipo kwenye usajili wa wachezaji wa KRC Genk ambao wanatumika kwa ajili ya msimu huu, wachezaji wengine vijana wa umri wake ambao wanapambania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo ni pamoja na Mike Penders (18), Josue Kongolo (17), Anouar Ait El Hadj (21), Konstantinos Karetsas (16), Luca Oyen (20), Noah Adedeji-Sternberg (18) na Christopher Bonsu Baah (19).

Tangu msimu uliopita Kelvin na wachezaji wengine vijana wamekuwa wakipata nafasi ya kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza cha KRC Genk kwa ajili ya maandalizi ya msimu husika na wale ambao humshawishi kocha hupewa nafasi.

WADAU UBELGIJI
Arthur Emmanuel ni miongoni mwa wadau wa soka la Tanzania ambaye anaishi Waregem yalipokuwa maskani ya zamani ya Novatus Dismas, amemshauri Kelvin hata kama KRC Genk itataka kumpa mkataba mpya aombe kutolewa kwa mkopo.
Mdau huyo anaamini kinda huyo anaweza kupata changamoto mpya ambazo zitamjenga na kuwa bora kama ilivyokuwa kwa Joseph Paintsil.

“Nakumbuka vile ambavyo Joseph (Paintsil) alikuwa na wakati mgumu Genk lakini alipotolewa kwa mkopo na kurejea akawa mmoja wa wachezaji muhimu kwenye kikosi hadi Genk ilipoamua kumuuza na kwenda Marekani, bado Kelvin ni mchezaji mdogo na mwenye kipaji kikubwa,” anasema.

Kwa upande wake, Jeff Megan ambaye ni rafiki wa Samatta huko Ubelgiji, anasema, “Ninachoamini wakati wake bado, ukifika hakuna mtu ambaye anaweza kuzuia hilo, itakuwa kama chemchem ya maji, kikubwa ni kuendelea kupambana.”

WASIFU WAKE
Kuzaliwa: Jun 10, 2003 (20)
Mahali: Morogoro, Tanzania
Uraia: Mtanzania
Urefu: 1,75 m
Nafasi: Mshambuliaji
Ajenti: CAA Stellar

Credit:- MwanaSpoti

SOMA NA HII  YANGA KUBEBA WINGA WA MAZEMBE...NI MKALI ZAIDI YA KISINDA...PABLO KUFYEKA WATATU SIMBA..CHAMA NDANI...