Home Habari za michezo TFF WAKUBALI YAISHE KWA MASTAA WA SIMBA NA YANGA WALIOKO TAIFA STARS….’SOO’...

TFF WAKUBALI YAISHE KWA MASTAA WA SIMBA NA YANGA WALIOKO TAIFA STARS….’SOO’ LOTE LIKO HIVI…

Habari za Michezo

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limezikubalia klabu Simba na Yanga kuwaruhusu nyota wa klabu hizo baada ya mechi ya kwanza ya Fifa Series 2024 dhidi ya Bulgaria utakaocheza Machi 22, mwaka huu kujiunga na timu zao kujiandaa na michezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Ofisa habari wa TFF, Clifford Ndimbo amesema wamepokea barua ya kuridhia maombi ya klabu hiyo mbili kutaka wachezaji wao kurejea kwenye vikosi vyao mapema kabla ya Machi 24, mwaka huu ili kupata nafasi ya kujiandaa kuelekea katika michezo ya robo fainali

Simba ina wachezaji wanne katika kikosi cha Taifa Stars ambao ni Aishi Manula, Kennedy Juma, Mohammed Hussein (Zimbwe Jr) na Kibu Denis na Yanga ni Aboutwaleeb Mshery, Bakari Mwamnyeto, Ibrahim Bacca na Mudathir Yahya.

Ndimbo amesema katika utaratibu wa tiketi za kurudi tarehe tofauti na wengine, Simba na Yanga wamekubaliwa wachezaji wao kuruhusiwa mapema baada ya mechi ya dhidi ya Bulgaria watarejea nchini na kujiunga na klabu zao.

“Ni kweli Simba na Yanga ilituandikia barua ya kuomba wachezaji wao ambao wako katika kikosi cha kwanza waliopo kwenye majukumu ya Taifa kujiunga harak kabla ya Machi 25, mwaka huu ili kuwahi program ya ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Al Ahly na Mamelodi Sundowns.

Kwa maslahi mapana ya pande zote mbili tumewakubaliana nyota hao lakini watakuwepo nchini Azerbaijan na kucheza mechi moja dhidi ya Bulgaria baada ya hapo watarejea kuendelea na majukumu ya klabu yao,” amesema Msemaji huyo.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally juu ya suala hilo amekiri kupeleka barua TFF ya kuomba wachezaji wao kurejea nchini mapema kuungana na wenzao waliopo Visiwani Zanzibar.

Amesema wachezaji wao waliopo kikosi cha Taifa Stars wataungana na wenzao Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kambi ya wiki mbili na kucheza mechi moja ya kirafiki kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly.

“Tunatarajia wachezaji wetu waliopo Taifa Stars kurejea mapama kama tulivyoomba pamoja na nyota wetu wa kimataifa ambao wameitwa kwenye timu za Taifa akiwemo Clatous Chama, Saidi Ntibazonkiza, Henock Inonga. nyota hao wakimaliza majukumu ya timu za Taifa watarejea haraka kuungana na wenzao kuendelea na maandalizi makubwa kwa ajili ya mambo mawili katika mchezo wetu dhidi ya Al Ahly.

Jambo la kwanza kuwatoa Al Ahly katika hatua hii suala la kuwafunga hilo tumefanya sana kwa sababu ndani ya miaka mitano tunekutana nao mara tatu katika michezo sita tumeshinda mara mbili. Kufungwa mara mbili na sare pia, hivyo hivyo kwa Al Ahly, “ amesema Ahmed.

Ameeleza kuwa wanataka kutengeneza mipango mizuri na maandalizi ‘bab kubwa’, kwa ajili ya kumuondoa Al Ahly katika hatua ya robo fainali msimu huu wamedhamilia kuingia nusu fainali.

Katika mchezo huo Simba wataanzia nyumbani Machi 29, mwaka huu, wakiwakaribisha Al Ahly ya Misri uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, saa 3:00 Usiku.

SOMA NA HII  SIMBA KAZI INAENDELEA ARUSHA