Home Habari za michezo KISA SARE YA 0-0….MAAMUZI YA YANGA KUELEKEA MECHI IJAYO HAYA HAPA…

KISA SARE YA 0-0….MAAMUZI YA YANGA KUELEKEA MECHI IJAYO HAYA HAPA…

Habari za Yanga leo

WABABE wa soka nchini, Yanga juzi usiku walikuwa uwanjani kupepetana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini mabosi wa klabu hiyo wameshtuka na kuanza kujipanga mapema kwa mechi ya marudiano ya ugenini huko Sauzi.

Yanga na Mamelodi zitarudiana katika mechi ya pili ya robo fainali itakayopigwa kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld, mjini Pretoria Ijumaa ijayo na mshindi wa jumla atafuzu nusu fainali na kuvaana kati ya Esperance ya Tunisia au Asec Mimomas ya Ivory Coast zilizokuwa zikiumana pia juzi usiku.

Hata hivyo, kwa kujua ugumu wa mechi hiyo ya ugenini, mabosi wa Yanga wakati timu ikijiandaa kwa mechi ya usiku wa juzi, tayari walishaanza maandalizi mapema ya mechi ya ugenini, ikiwamo kuanza kutanguliza watu wa kuweka mambo sawa kabla ya timu kuifuata kuanzia kesho kutwa.

Mmoja wa vigogo wa Yanga, alisema wanajua ugumu wa kuvaana na Mamelodi ikiwa nyumbani, ndio maana wameanza mikakati hiyo mapema bila kujali matokeo ya mchezo wa juzi kwani kiu yao ni kuona wanaendeleza rekodi katika michuano hiyo ya CAF.

“Msimu uliopita tulienda Afrika Kusini kucheza na Marumo Gallants katika mechi ya nusu fainali na tulijipanga mapema na kutoka ushindi ugenini, hata sasa tunaamini tukijiwekea mazingira mazuri kwa mechi ijayo na Mamelodi kule Pretoria tunaweza kuwashangaza kwao,” alisema kigogo huyo.

Katika mechi hiyo ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Yanga ilishinda ugenini 2-1 kwa mabao ya Fiston Mayele na Kennedy Musonda na kusonga kwa jumla ya mabao 4-1 kwani mechi ya kwanza ikiwa nyumbani ilishinda mabao 2-0 na safari hii wanataka kwenda kupata ushindi dhidi ya Mamelodi.

Mamelodi iliwahi kuifunga Yanga mabao 3-2 ikiwa Sauzi katika mecho ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu wa 2001 na kulazimishwa sare ya 3-3 jijini Dar, kitu ambacho mabosi wa Yanga wamesema hawataki kirudie wakienda kuvaana nao Sauzi hata kama imepita miaka mingi tangu timu zilipokutana kwani timu zote zimebadilika kwa sasa.

“Tulikuwa tunamalizana nao Dar, ila akili na nguvu zipo kwa mchezo wa ugenini, bahati nzuri tunajivunia rekodi tamu za ugenini katika michuano tya CAF tangu msimu uliopita,” aliongeza kigogo huyo ambaye hata hivyo hakuweka bayana mipango wanayoifanya wala waliyemtanguliza Sauzi.

Yanga itakuwa mgeni wa Mamelodi inayoshikilia taji la AFL mechi itakayopigwa Ijumaa mjini Pretoria huku ikiwa a kumbukumbu ya kumaliza mechi za makundi kwa kipigo chja bao 1-0 ugenini dhidi ya Al Ahly, kikiwa ni kipigo cha pili kwa Yanga msimu huu katika mechi 10 ilizocheza za CAF tangu Februari 26, mwaka jana, ikishinda mechi sita, droo mbili na vipigo hivyo viwili kikiwamo cha 3-0 kutoka kwa CR Belouizdad ya Algeria.

Kuanzia Februari 26 ilipotoka sare ya Real Bamako katika mechi ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita, Yanga ilishinda ugenini dhidi ya TP Mazembe iliyoinyoa 1-0, ikaipiga Rivers United ya Nigeria katika robo fainali ya michuano hiyo ya Shirikisho kwa mabao 2-0.

Pia iliitwanga Marumo katika nusu fainali kwa mabao 2-1 na kuichapa waliokuwa mabingwa, USM Alger kwa bao 1-0 kwenye fainali ya pili iliyopigwa mjini Algiers na Yanga kulikosa taji kwa faida ya bao la ugenini kwani ilinyukwa mabao 2-1 nyumbani na matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.

Kwa msimu huu wa Ligi ya Mabingwa ilianza na ushindi wa 2-0 dhidi ya Asas ya Djibouti, ikaienda kuinyuka El Merrikh ya Sudan 2-0 jijini Kigali, Rwanda iliyotumiwa kama uwanja wa nyumbani wa Wasudan, kisha ndipo ikanyukwa na CR Belouizdad mechi ya kwanza ya makundi, ikatoka droo na Medeama ya Ghana na kulala tena 1-0 kwa Al Ahly ambayo juzi usiku iliifunga Simba 1-0 katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hata hivyo, Yanga ni lazima ijipange kwelikweli kukabiliana na Mamelodi ikiwa nyumbani kwao, kwani rekodi zinaonyesha katika mechi tisa za michuano ya CAF ilizocheza tangu Aprili 29, 2023 haijapoteza hata moja, isipokuwa imeshinda saba na kutoka sare mbili kuonyesha sio timu ya kuichukulia poa.

Katika mechi hizo tisa za CAF zilizopita, imeruhusu nyavu zao kuguswa mara tatu tu na yenyewe kufunga mabao 13, huku ikiwa na clean sheet katika mechi saba pia na mbili tu ilizoruhusu mabao hayo matatu, kitu kinachompa kazi kocha Miguel Gamondi wa Yanga kuisuka upya safu yake ya ushambuliaji kama inataka kuinyamazisha Mamelodi ikiwa Pretoria hiyo Ijumaa.

Nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Said Maulid ‘SMG’ alisema itakuwa mechi ngumu kwa timu zotee mbili lakini ameweka wazi Yanga inaweza kupata ushindi kama itakuwa na wachezaji wote nyota wakiwa timamu kimwili.

“Pamoja na ukubwa wa Mamelodi lakini Yanga kwa sasa ina kikosi imara. Wachezaji wana ubora mkubwa pia wana kiu ya kufika mbali, utakuwa ni mchezo mzuri, Yanga inaweza kushinda kama itakuwa na mastaa wote na watacheza kwa umoja kama imekuwa ikifanya iwe nyumbani au ugenini,” alisema SMG aliyewahi kucheza soka la kulipwa Angola, huku kocha wa Dodoma Jiji, Francis Baraza alisema Yanga ina wachezaji bora wanaoweza kuidhibiti Mamelodi na kupata ushindi kuanzia hapa nyumbani hadi ugenini kwa soka la sasa halichagui mahali unapocheza kama umejipanga vyema.

“Wanatakiwa kujiamini na kwenda kupambana, kwani hakuna timu isiyofungika na uwezo wa kuwafunga Mamelodi inao,” alisema Baraza.

SOMA NA HII  MUONEKANO WA UKURASA WA NYUMA GAZETI LA SPOTI XTRA JUMANNE