Baada ya kuishuhudia Timu yake ikifuzu kwa mbinde kwa changamoto ya ,mikwaju ya penati 3-2 dhidi ya Yanga mchezo wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa.
Kocha wa Mamelodi Sundowns, Rulani Mokwena kwenye mkutano na Waandishi wa Habari amesema;
“Kwa kifupi sina cha kusema kuhusu Yanga wamenizidi karibia kila eneo kwenye michezo yote miwili hilo napaswa kulikubali, lakini pia siwezi kuzungumzia kuhusu goli lao kama ni halali au sio halali kwakuwa naelewa hata ingekuwa mimi ni Yanga nisingesema tofauti”
Mabingwa hao wa Tanzania, Yanga SC wametupwa nje ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika na Mamelodi Sundowns kwa penalti 3-2 kufuatia sare ya 0-0 ndani ya dakika 90 usiku wa jana Ijumaa Uwanja wa Loftus Versfeld Jijini Pretoria, Afrika Kusini.
Katika mchezo huo wa marudiano wa Robó Fainali, Refa Dahane Beida wa Mauritania alilazimika kutumia Teknolojia ya VAR dakika ya 58 kuamua juu ya shuti la kiungo mshambuliaji wa Yanga, Mburkinabe, Stephane Aziz Ki lililoonekana kudundia ndani ya mstari wa lango si bao.
Katika mikwaju ya penalti waliofunga za Mamelodi Sundowns ni viungo Mchile, Marcelo Allende, Mbrazil Lucas Ribeiro Costa na mzawa, Neo Maema wakati ya nyota kutoka Uruguay, Leandro Sirino iliokolewa na kipa Mmali, Djigui Diarra wa Yanga.
Waliofunga penalti za Yanga ni winga Mghana, Augustine Okrah na mshambuliaji wa Ivory Coast, Joseph Guédé Gnadou huku Aziz Ki na mabeki Dickson Job na Ibrahim Hamad ‘Bacca’ wakikosa.
Ikumbukwe mechi ya kwanza ya Robó Fainali Jumamosi iliyopita timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana pia Uwanja wa Benjamín Mkapa Jijini Dar es Salaam. Sasa Mamelodi Sundowns itakutana na mshindi wa jumla katí ya Esperance ya Tunisia na ASEC Mimosas ya Ivory Coast zinazorudiana leo baada ya sare ya 0-0 pia kwenye mechi ya kwanza.