Kinachoendelea Simba leo ni matokeo mchakato wa uchaguzi Mkuu uliopita.
Uchaguzi ambao ulikuwa na makundi makuu mawili, kundi la waliokuwa wanamuunga mkono Wakili Karua na kundi la waliokuwa wanamuunga mkono Mangungu [wote walikuwa wanagombea uenyekiti upande wa wanachama].
Sio jambo baya kwa maana ya demokrasia kuchukua nafasi yake na kila mtu kuamini katika upande anaoona unafaa.
Baada ya mchakato wa uchaguzi, Mangungu alifanikiwa kushinda nafasi ya mwenyekiti upande wa wanachama.
Lile kundi la wanaomuunga mkono Wakili Karua ni kama
hawakukubali matokeo, na kwa bahati mbaya kundi hilo ni kama mwekezaji alikuwa analiunga mkono kimyakimya bila kuonekana na watu wa nje.
Baada ya uchaguzi ndio mwekezaji akaanza kujiweka mbali na timu, wakati yeye ndio alitakiwa arudi na kuwaita wote wakakaa pamoja ili kufuta makundi na tofauti zilizojitokeza wakati wa uchaguzi.
Watu waungane na kuwa kitu kimoja kama ikivyokuwa kabla ya uchaguzi.
Kwa hiyo hadi sasa hivi yale makundi bado yapo na yanakubaliana kutokukubaliana! TeamMangungu wanaendelea na timu lakini wale TeamKarua hawapo kwenye mfumo na kama hawautambui uongozi uliopo madarakani.
Huko kutoelewana kati yao ndio kunapekelea haya tunayoyaona sasa hivi ndani ya Simba.
Suluhisho pekee ya hili ni kurudi tena pamoja na mtu wa kufanikisha hilo ni mwekezaji mwenyewe Mo Dewji.
Kuna kipindi alijaribu kuiunganisha Simba kwa kuunda Kamati iliyokuwa na watu wengi, hizo zilikuwa ni jitihada za kutaka kusawazisha mambo lakini bado hakufanikiwa.
Kinachoigharimu Simba ni kukosa umoja miongoni mwao lakini siku wakikaa pamoja wakavunja makundi na kurudisha umoja wao, watazungumza lugha moja na kupiga hatua.