Home Habari za michezo KUMBE SIMBA WAMEWEKA KAMBI ZANZIBAR KWA SABABU HII…KIBADENI AFUNGUKA A-Z

KUMBE SIMBA WAMEWEKA KAMBI ZANZIBAR KWA SABABU HII…KIBADENI AFUNGUKA A-Z

Habari za Michezo

Simba imeenda tena kuchukua maujanja Zanzibar kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Yanga utakaochezwa Jumamosi ya wiki hii kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kuanzia saa 11:00 jioni.

Ni Kariakoo Dabi ambayo kila mmoja anaizungumzia kwa namna yake, lakini ndani ya uwanja, dakika tisini ndizo zitaamua matokeo ya mwisho nani atacheka na nani atalia au kama mzani utakuwa sawa.

Baadhi ya mashabiki wa Simba na wadau wa soka kwa jumla, wanajiuliza Simba inafuata nini zaidi Zanzibar ambacho kama wakiamua kubaki Dar es Salaam watakikosa katika maandalizi yao hayo.

Maswali hayo yanajibiwa na Mwanaspoti kupitia rekodi za Simba miaka ya nyuma ilipoamua kuweka kambi Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi matokeo yalikuwaje.

Lakini mbali na kuangalia rekodi, wachezaji na makocha waliowahi kupita ndani ya Simba nao wamefichua kilichopo kambini huko, sehemu ambayo Simba imeiona kama ni mkombozi wao mkubwa.

Ikumbukwe kwamba, mbali na Simba kukimbilia Zanzibar kujiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi dhidi ya Yanga, lakini pia imewahi kwenda visiwani humo kujiandaa na mechi za michuano tofauti ikiwemo ile ya Machi 29, mwaka huu dhidi ya Al Ahly.

Simba iliweka kambi Zanzibar kujiandaa na mchezo wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo walipoteza kwa bao 1-0 nyumbani, kabla ya kwenda ugenini na kufungwa mabao 2-0, ikatolewa na Al Ahly kwa jumla ya mabao 3-0.

SIRI ILIYOJIFICHA SIMBA ZANZIBAR
Si mara zote Simba imekuwa ikienda Zanzibar inapokuwa inajiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi, lakini kwa mujibu wa rekodi zilizopo miaka ya karibuni ilipoweka kambi visiwani humo ilipokuwa ikijiandaa kuikabili Yanga, ilishinda mechi tatu na moja sare.

Katika mchezo wa Ligi Kuu uliochezwa Mwachi 8, 2015, wakati Simba ikiwa inanolewa na Kocha Mkuu, Dylan Kerr, walishinda bao 1-0, mfungaji akiwa ni Emmanuel Okwi. Kabla ya mchezo huo, Simba iliweka kambi ya muda mfupi Zanzibar.

Baada ya hapo, mchezo wa Februari 25, 2017, wakashinda tena mabao 2-1 dhidi ya Yanga kwa mabao ya Laudit Mavugo na Shiza Kichuya, huku lile la Yanga mfungaji akiwa Simon Msuva.

Hapa Simba waliweka kambi Zanzibar, timu ikiwa chini ya Kocha Joseph Omog.
Mwanzoni mwa msimu wa 2017/18 ambapo timu hizo zilikutana katika Ngao ya Jamii iliyochezwa Agosti 23, 2017.

Dakika tisini za mchezo huo matokeo yalikuwa 0-0. Simba iliyokuwa ikinolewa na Joseph Omog, ikashinda kwa penalti 5-4.

Mara ya mwisho kwenda Zanzibar wakati wakijiandaa na mchezo wa Kariakoo Dabi, ilikuwa katika mechi ya Septemba 30, 2018, ikamalizika kwa matokeo 0-0.

KWA NINI ZANZIBAR TENA?
Ukiangalia Simba na Yanga miaka ya nyuma inapokaribia Kariakoo Dabi zilikuwa zikihamisha kambi kutoka Dar es Salaam na kuwenda kujificha nje ya mkoa huo ikiwemo Zanzibar na mikoa mingine, lakini utamaduni huo wakaja kuachana nao hapa katikati.

Yanga wakaweka makazi yao rasmi Avic Town pale Kigamboni walipo hadi sasa, Simba kwao ni Bunju ambapo kuna uwanja wake wa mazoezi ambao ndiyo inautumia katika maandalizi ya mechi mbalimbali ikiwemo zile za kimataifa.

Safari hii Simba wameamua kubadili upepeo, wamerudi kwenye sehemu wanayoamini kwamba ni salama kwao katika kuweka mikakati mizuri ya ushindi.

Walianza hivyo walipojiandaa kucheza dhidi ya Al Ahly, licha ya kwamba hawakwenda na wachezaji wote kutokana na wengine kuwa na majukumu ya timu za taifa kipindi cha Kalenda ya FIFA, lakini Kocha Abdelhak Benchikha alisisitiza kwamba ameamua kuipeleka timu huko kutokana na kuhitaji utulivu zaidi.

Kwa sasa ukiangalia Simba inapitia wakati mgumu, mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakitoa vitisho kwamba kama timu ikiendelea kutopata matokeo mazuri, watalazimika kufanya jambo tofauti ikitafsiriwa ni kufanya vurugu.

Ili kipindi kama hiki kuwafanya wachezaji kuwa watulivu na kuondoa huo wasiwasi, huku akili na mawazo yao yakiwa zaidi kuelekea mchezo ulio mbele yao, wameamua kwenda kujificha Zanzibar tofauti na wangebaki Bunju, wanapofanyia mazoezi Mo Simba Arena.

Kitu cha kwanza kilichowafanya wakimbilie Zanzibar na siyo sehemu nyingine mikoani, ni ukaribu wa Dar na Zanzibar, lakini pia, huko wametoka hivi karibuni na wameona kuna kitu cha tofauti walikipata mara ya mwisho walipoenda.

HALI YA HEWA
Kwa sasa hali ya hewa ya Zanzibar na ilivyo Dar es Salaam, hazitofautiani sana, kote kuna mvua za hapa na pale kitu ambacho hakiwezi kuwafanya kuharibu ratiba zao za mazoezi.

Pengine wangeamua kusaka sehemu nyingine yenye utulivu mbali na Zanzibar, hali ya hewa ingeweza kuwasaliti kwani sehemu nyingi za nchi hii tofauti na maeneo yaliyotajwa hapo, mvua zake ni nyingi na zimeleta maafa.

MUDA
Kuanzia leo Jumanne mpaka Ijumaa ambapo Simba inatarajiwa kurejea Dar es Salaam kwa ajili ya mchezo utakaopigwa Jumamosi, ni takribani siku nne. Hivyo Kocha Benchikha ana muda wa siku nne kuiweka sawa timu yake na kuirudisha kwenye hali ya ushindani kama ambavyo mashabiki na viongozi wa timu hiyo wanahitaji kuona kikifanyika.

Kwa sasa Simba imepoteza hali ya ushindani kutokana na aina ya matokeo inayoyapata katika mechi zake za michuano yake.

Rekodi zinaonesha kwamba, katika mechi nne zilizopita, Simba imeambulia sare moja dhidi ya Ihefu (1-1), imepoteza mechi tatu, mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly (1-0 nyumbani na 2-0 ugenini), lakini ikapoteza katika Kombe la FA ilipofungwa kwa penalti 5-4 dhidi ya Mashujaa baada ya dakika tisini matokeo kuwa 1-1.

KOCHA, MCHEZAJI WAFICHUA JAMBO
Kocha wa zamani wa Simba, Abdallah Kibadeni ambaye wakati akicheza soka enzi zake aliweka rekodi ya kufunga mabao matatu ‘hat-trick’ katika dabi, anaamini utulivu ndiyo kitu ambacho kimekuwa kikiwafanya Simba na Yanga kutoka nje ya Dar es Salaam kwa ajili maandalizi.

“Dabi huwa ni zaidi ya mechi ya kawaida, hivyo hata maandalizi yake huwa makubwa, Zanzibar ni sehemu tulivu kwa hiyo kocha na viongozi wameona ni sehemu sahihi kwao kwenda huko na kufanya maandalizi,” anasema Kibadeni.

“Kitu kingine ambacho huwa kinatazamwa ni usiri ambao utawasaidia maandalizi yao kuwa ya ndani tu bila kufuatiwa na wapinzani.”

Kibadeni aliweka rekodi yake katika dabi iliyochezwa Julai 19, 1977 akifunga mabao matatu wakati Simba wakiibuka na ushindi wa mabao 6-0. Alifanya balaa hilo katika dakika ya 10, 42 na 89, huku mengine yakifungwa na Jumanne Hassan ‘Masimenti aliyefunga mawili dakika ya 60 na 73 na beki wa Yanga, Selemani Sanga alijifunga dakika ya 20.
Kwa upande wake, Uhuru Seleman Mwambungu ambaye aliwahi kuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, alisema:

“Dabi haijawahi kuwa rahisi kama wengi wanavyodhani, nimecheza na najua namna ilivyo na haiwezi kuzoeleka.

“Kutokana na hilo, viongozi huhitaji timu ifanye maandalizi katika eneo tulivu ambalo kutakuwa na usiri na wala hakuna kitu kingine cha ziada.”

SOMA NA HII  KISA SARE NA AL AHLY JUZI....KIGOGO YANGA 'KANG'ATA ULIMI' KISHA AKASEMA HAYA MAPYA...