Heshima aliyojijengea nahodha wa Simba, John Bocco tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara mwaka 2008 hadi 2024, inawafanya
mashabiki kuyafuatilia maisha yake na kutaka kujua ukimya wake unasababishwa na kitu gani.
Kwa wachezaji wa sasa, Bocco ndiye anaongoza kwa kufunga mabao 154 katika misimu 16 aliyocheza, ukiachana na mastaa wa zamani kama Mohamed Hussein ‘Mmachinga’ aliyeacha rekodi ya mabao 153 katika misimu 13.
Tangu msimu huu uanze Bocco, hakuwa na nafasi kubwa kikosini, mechi yake ya mwisho kufunga bao ilikuwa Desemba 15 kwenye Uwanja wa Uhuru dhidi ya Kagera Sugar, timu yake ikishinda 3-0, mabao mengine yakifungwa na Said Ntibanzokiza ‘Saido’ kwa penalti na Sadio Kanoute.
Bocco hajaonekana kwa muda mrefu uwanjani, zipo baadhi ya mechi, mashabiki na wachezaji wanaona zilifaa uwepo wake, mfano Simba dhidi ya Al Ahly.
Nahodha wa Prisons, Benjamin Asukile aliwahi kusema: “Mechi ya Al Ahly na Simba kuna nafasi ambazo washambuliaji walizikosa angekuwa Bocco angefunga, shida iliyopo kwenye soka letu wapo watu wanaoshindwa kuheshimu mchango wa wachezaji.”
MAMBO YA KUJIULIZA KWA BOCCO KASTAAFU KIMYAKIMYA?
Kwa heshima aliyojiwekea kwenye soka la Tanzania, kama Bocco angestaafu soka, ingekuwa vyema kuagwa kama ilivyokuwa kwa wengine waliowahi kupewa heshima hiyo ndani ya Simba, pia ingepunguza maswali mengi kwa mashabiki wake. Kitendo cha Bocco kutoonekana, wengi wanajiuliza huenda ni majeraha ama sintofahamu baina yake na uongozi.
KUONEKANA NA KIKOSI B
Kuna baadhi ya picha zilimuonyesha Bocco akiwa na timu ya vijana ya Simba, jambo linalozua maswali mengi kwamba ndio majukumu yake mapya na hataonekana tena uwanjani, jibu la swali hilo lipo kwa viongozi wa klabu na Bocco mwenyewe.
HESHIMA YAKE INAISHIAJE
Bocco hakuzifanyia makubwa Azam FC na Simba pekee, bali alikuwa na mchango kwenye kikosi cha Taifa Stars, jambo lililofanya wachezaji wengi vijana wanatamani kufikia mafanikio yake.
Baadhi yao waliowahi kukiri hilo ni Anwar Jabir (Dodoma Jiji), wengine japokuwa wanacheza nafasi tofauti na yeye ni beki Oscar Masai (Mtibwa), winga Edwin Balua (Simba) hao ni baadhi.
Kulikuwa na uvumi wa chinichini kwamba Bocco alitakiwa kurejea kikosini wakati Simba ikijiandaa kuikabili Yanga Aprili 20, lakini staa huyo alikataa akiona hapewi heshima yake, hivyo ukimya uliopo baina yake na viongozi unafanya tetesi hizo kuwa na nguvu.
JE, KAPATA MRITHI?
Kocha Meja Mstaafu, Abdul Mingange amewahi kusema akimtazama Clement Mzize wa Yanga akitengenezwa vizuri kwenye ufungaji wake, anamtarajia awe Bocco ajaye, huku akisisitiza Bocco anastahili kuagwa kwa heshima endapo kama anastaafu soka. Je, Simba imepata mshambuliaji mzawa mbadala wake atakayemkabidhi jezi yake 22?
Miaka mitano iliyopita aliyekuwa nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wakati anatundika daruga, jezi aliyokuwa anaivaa namba 23 aliikabidhi kwa beki Abdallah Shaibu ‘Ninja’, wakati anaagana na mashabiki wake Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.
Je, Bocco amepewa nafasi hiyo ya kuagana na mashabiki wake na wale ambao walimuona kama kioo katika kazi zake? Hilo limewahi kumfikirisha, meneja wa zamani wa Azam FC, Phillip Alando kwamba Bocco na Erasto Nyoni wataagwa na timu gani.
“Ni wachezaji ambao hawajacheza timu nyingi hapa nchini, Bocco kacheza kwa muda mrefu Azam na Simba, Erasto ni Azam, Simba na sasa yupo Namungo, wanastahili kuagwa kwa heshima siku wakitundika daruga ila sijui ni timu gani itachukua jukumu hilo,” amesema.
REKODI ZA BOCCO LIGI KUU
AZAM FC
2008/2009(1),2009/2010 (14), 2010/2011 (12),2011/2012 (19), 2012/2013 (7), 2013/2014 (7), 2014/2015 (2), 2015/2016 (12), 2016/2017 (10), alifunga jumla ya mabao 84.
SIMBA
2017/2018 (14), 2018/2019 (16), 2019/2020 (9), 2020/2021 (16), 2021/2022 (3), 2022/2023 (10), 2023/2024 (2), amefunga jumla ya mabao 70.
Bocco tangu aanze kucheza Ligi Kuu Bara 2008-2024 ana jumla ya mabao 154.