Home Habari za michezo KUELEKEA MECHI IJAYO….JIKUMBUSHE BACCA NA JOB ‘WALIVYOMFICHA’ STAA HUYU WA MAMELOD…

KUELEKEA MECHI IJAYO….JIKUMBUSHE BACCA NA JOB ‘WALIVYOMFICHA’ STAA HUYU WA MAMELOD…

Habari za Yanga leo

Yanga imelinda heshima ikiwa nyumbani baada ya kulazimishwa suluhu na matajiri wa Sauzi, Mamelodi Sundowns lakini kama kuna kazi ilifanyika basi ni ukuta wa timu hiyo ulivyowapoteza kina Peter Shalulile lakini kumbe Kocha Miguel Gamondi aliwabadilishia mziki jioniii.

Yanga ilipata sare hiyo isiyo na mabao kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa katika mechi ya kwanza ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, huku kocha Gamondi alianza na mabeki wa kati watatu kwenye ukuta, huku mbele yao akiwemo kiungo nguli, Jonas Mkude ila kazi ya maana ilifanywa na Dickson Job ambaye alikuwa kinara wa kutibua.

MABADILIKO YA GAMONDI

Tuanze na hesabu za Gamondi. Jamaa baada ya kuona kikosi kilichoanza cha Mamelodi akiwa tayari ameshaandaa timu kuanza na mfumo wa 3-5-2, fasta akawaita wachezaji na kuwafanyia mabadiliko ya mfumo mwingine ambao alikuwa ameshauandaa.

Gamondi akawaingiza mastaa na mfumo wa 4-4-2 ambao ndio uliwazima Mamelodi maarufu kama Masandawana ambao wakashindwa kuipenya kirahisi ngome ya wenyeji wao.

UKUTA WENYEWE

Ukuta wa Yanga katika mchezo huo, Job ndiye alikuwa kinara wa kutibua mashambulizi ya Mamelodi ambapo alitibua mashambulizi 13 ya wapinzani wao, kipindi cha kwanza akifanya kazi hiyo mara nne kisha kipindi cha pili akatibua mara tisa.

Nyuma ya Job ambaye ni nahodha msaidizi, alikuwa beki mjeshi, Ibrahim Hamad ‘Bacca’ aliyetibua mashambulizi 11 ya Mamelodi, kipindi cha kwanza aliharibu hesabu za wapinzani hao mara sita na kipindi cha pili alifanya hivyo mara tano.

Kazi hiyo bora ambayo iliwafanya washambuliaji wa Mamelodi kuonekana wa kawaida iliendelea akifuata Mkude ambaye alianza mechi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa akitibua hesabu za hatari za Mamelodi mara saba na kipindi cha kwanza alitibua shambulizi moja tu kisha kipindi cha pili akafanya hivyo mara sita na kuwasahaulisha mashabiki wa Yanga pengo la Khalid Aucho.

Nahodha mkuu wa Yanga, Bakari Mwamnyeto naye alikuwa kwenye daraja hilo hilo akitibua mashambulizi sita ya Mamelodi katika eneo la mwisho na kipindi cha kwanza alitibua mara mbili kisha kipindi cha pili akatibua mara nne.

Lomalisa Mutambala ambaye mapema tu alipata kadi ya njano iliyompunguza kasi baada ya kumkwatua Mchile, Marcelo Allende naye akatibua mashambulizi manne ya Mamelodi na kipindi cha kwanza alitibua mara moja kisha kipindi cha pili akafanya hivyo mara tatu.

MSIKIE JOB

Akizungumzia ubora wa safu yao ya ulinzi Job alisema ilikuwa mechi kubwa lakini mpango huo ulikuwa rahisi kwao kutokana na mpango mzuri wa mechi kutoka kwa kocha wao Gamondi huku pia akiwapongeza wenzake kwa kucheza kwa kwango kikubwa.

“Mechi ilikuwa kubwa na ngumu, sio kwamba nilikuwa bora hapana kwanza tuwapongeze makocha wetu kwa kutupa mpango mzuri wa mechi, pili wachezaji wenzangu kila mmoja alijituma kwa nafasi yake kwa kiwango cha kushtua, ilikuwa unamuona kila mmoja yuko makini hata wewe unahamasika kuwa kama wao,” alisema Job.

“Hatukutaka kuwaangusha mashabiki wetu hasa tulipoona uwanja umejaa huku tukisikia mashabiki wengine walizuiwa kuja kuingia tukasema tuwafanyie kazi kubwa kulinda heshima yao nyumbani nisiwasahau viongozi wetu ambao muda wote walikuwa wanatusisitiza kwenda kuitetea klabu na taifa.

MOKWENA HUYU HAPA

Kocha wa Mamelodi, Rhulani Mokwena akizungumzia safu ya ulinzi ya Yanga alisema ukuta huo ulifanya kazi ya viungo wao na hata washambuliaji kuwa ngumu kwa kucheza kwa kuwabana vizuri.

“Hatukuwa wazuri katika kuzalisha pasi za mabao, nirudie kusema tulicheza dhidi ya timu yenye ukuta mzuri, mabeki wa Yanga walicheza kwa kiwango kikubwa kwa ubora kama ule sitashangaa kama mtaona washambuliaji wangu hawakufanya kitu, tunakwenda kujipanga na mchezo wa marudiano.

Kocha huyo alisema naamini mechi ya marudiano itakayopigwa Pretoria, Afrika Kusini itakuwa ngumu kwa kila mmoja kwani mchezo bado upo wazi kwa kila mmoja, licha ya ukweli ipo katika nafasi nzuri kwani sare ya aina yoyote ya mabao inavusha kwenda nusu fainali kwa faida ya bao la ugenini.

Hii ilikuwa ni sare ya pili kwa Mamelodi kuipata mbele ya Yanga ikiwa ugenini kwani zilipokutana katika mechi za raundi ya pili ya michuano hiyo msimu wa 2001 iliisha kwa sare ya 3-3 baada ya awali timu hiyo ya Sauzi kushinda nyumbani mabao 3-2 na kusonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 6-5.

SOMA NA HII  PAMOJA NA KUANZA VYEMA SIMBA...PABLO ASHINDWA KUJIZUIA..AFUNGUKA MSIMAMO WAKE...