Home Habari za michezo NABI:- HUYU MZIZE HUYU…IPO SIKU NAWAAMBIA

NABI:- HUYU MZIZE HUYU…IPO SIKU NAWAAMBIA

Habari za Yanga leo

“Msimchukulie poa.” Ndicho alichosema kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi juu ya straika wa timu hiyo, Clement Mzize ambaye anaamini anaweza kuwa mmoja wa washambuliaji hatari wa Kitanzania miaka michache ijayo.

Hata hivyo, alichosema kocha huyo wa sasa wa FAR Rabat ya Morocco ni kwamba, mchezaji huyo atafika tu huko anapofikiria iwapo ataendelea kuaminiwa na kupewa nafasi na kocha wa sasa, Miguel Gamondi kutokana na umri wake.

Kocha huyo ambaye kwa sasa anaiona AS FAR ya Morocco, amesema hayo kufuatia msala alionao Mzize hasa baada ya kuondoka kwa Fiston Mayele. Mshambuliaji huyo na wenzake waliopo kwa sasa, akiwemo Joseph Guede wameonekana kuwa na wakati mgumu kuongoza safu ya ushambuliaji ya timu hiyo, badala yake, Yanga kwa sasa inabebwa na viungo washambuliaji Stephane Aziz KI mwenye mabao 13, Maxi Nzengeli (9), Mudathir Yahya (8) na Pacome Zouzoua (7), hakuna mshambuliaji wa kati hata mmoja aliyepo kwenye vita ya kuwania kiatu cha ufungaji bora katika ligi.

Nabi ambaye alimtambulisha kijana huyo katika soka la ushindani na kumpa nafasi licha ya kuwa na mshambuliaji hatari kwa wakati huo, Fiston Mayele aliyekuwa akitetema kila kukicha, amesema Mzize ni kijana mwenye kipaji kikubwa, hivyo anatakiwa kuendelea kujengwa.

“Hatukumpa presha kubwa, niliamini kuwa ni mchezaji mzuri ambaye anahitaji muda, hatua kwa hatua ili kupata kile kilicho bora kutoka kwake, na alikuwa msaada katika timu pale ambapo alikuwa akihitajika, nilikuwa nikikaa naye mara kwa mara kumjenga, kiukweli anatakiwa kuendelea kupewa nafasi ili kubwa bora zaidi,” alisema kocha huyo.

Mzize mwenye mabao manne katika ligi na asisti tatu, alifunga bao muhimu, Jumatano usiku wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya kombe la Shirikisho (FA) na kufikisha mabao matano katika ma-shi-ndano hayo, akiwa kinara wa ufungaji.

Miongoni mwa mambo ambayo yamekuwa yakimuangusha Mzize licha ya kujua kukaa katika nafasi na kuwa na mikimbio mizuri, ni namna ya kutumia nafasi hizo, mfano mzuri ni katika michezo yote miwili ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika alipoteza nafasi mbili za wazi dhidi ya Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini, huku akitizamana na kipa, Ronwen Williams.

Mzize mwenye umri wa miaka 20, akizungumzia hilo baada ya kuifunga Dodoma Jiji, juzi, alisema: “Japo muda mwingine nimekuwa nikikosa nafasi, kama mshambuliaji nimekuwa nikiendelea kupambana kwa kufanyia kazi upungufu wangu kwa kutaka kuwa bora zaidi. Wakati nikiingia kocha aliniambia nisipaniki maana katika mchezo uliopita sikufanya vizuri (alipoteza nafasi za wazi).”

MSIKIE NGASSA

Akimzungumzia Mzize ambaye msimu uliopita alifunga mabao matano na kutoa asisti moja katika ligi chini ya Nabi, nyota wa zamani wa Yanga, Mrisho Ngassa alisema mshambuliaji huyo ana kitu ndani yake, hivyo anatakiwa kuendelea kuvumiliwa kwani anaweza kuwa mmoja wa washambuliaji hatari nchini.

“Yanga hii ni bora sana katika miaka hii miwili. Toka naijua Yanga kwa sasa mashabiki wana injoi sana, wanaenda uwanjani wakijua watashinda,” alisema Ngaza huku akiongeza kwa kusema:

“Niwape ushauri mashabiki wa Yanga, wampe sapoti Mzize, ni mtu hatari sana kushinda wote wanaowapenda au ambao waliwahi kuwapenda, ni suala la muda tu kwake kuonyesha nini alichonacho.”

SOMA NA HII  KIKOSI CHA WACHEZAJI 25 WA AZAM FC CHAIFUATA PYRAMIDS YA MISRI KIBABE