Home Habari za michezo ROBERTINHO:- JOBE NA FREDY NI HASARA TUPU WALE…. WANATAKIWA WAFUKUZWE SIMBA…

ROBERTINHO:- JOBE NA FREDY NI HASARA TUPU WALE…. WANATAKIWA WAFUKUZWE SIMBA…

Habari za Simba leo

Kwa sasa Simba inakuna kichwa ikitafuta mbinu za kushuka nazo jijini Cairo, Misri katika mechi ya marudiano ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly baada ya kunyukwa bao 1-0 Kwa Mkapa, lakini kocha wa zamani wa timu hiyo amewang’oa mastraika wawili wapya klabuni hapo.

Simba ilifungwa na Al Ahly wikiendi iliyopita katika mechi ya mkondo wa kwanza wa robo fainali ikiwa ni mara ya kwanza kupoteza nyumbani dhidi ya Al Ahly na sasa italazimika kushinda angalau kuanzia mabao mawili ili irejee rekodi iliyowekwa mwaka 1974 kwa kucheza hatua ya nusu fainali.

Katika mwaka huo, Simba ilikumbana na Mehalla El Kubra ya Misri na kufungwa kwa mikwaju ya penalti 3-0 baada ya kila timu kushinda mechi ya nyumbani, lakini ikiirejesha Simba katika kumbukumbu ya mwaka 2003 ilipowavua taji Zamalek kwa penalti jijini humo na kutinga makundi.

Achana na hilo. Kocha wa zamani wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ aliufuatilia mchezo huo wa juzi na kutamka wazi kipigo kilichangiwa zaidi na kukosekana kwa mshambuliaji wa kuimaliza Al Ahly, kisha akasema washambuliaji wapya walioanzishwa benchi, Pa Omar Jobe na Freddy Michael wanatakiwa kupigwa chini na klabu hiyo, kwani ni usajili wa hasara kwa Mnyama.

Akizungumza akiwa jijini Rio de Jeneiro, Brazil Robertinho alisema Simba ilicheza vizuri mechi hiyo, lakini eneo la mwisho la umaliziaji likawaangusha kwa kukosa watu muafaka wa kuimaliza mechi.

Robertinho alisema hana shida na mrithi wake Kocha Abdelhack Benchikha kwani mbinu zake zilitiki mbele ya Waarabu, lakini akasema Simba lazima imeze dawa chungu kwa kuwatema kina Pa Jobe na Freddy walioingizwa kupitia dirisha dogo la usajili iwapo timu hiyo itatolewa katika michuano hiyo ya CAF.

Kocha huyo aliyewagomea Ahly mara mbili katika mechi za African Football League, alisema Simba iliwasajili washambuliaji hao wakubwa kwa kazi hii ambayo hata hivyo wote wamejikuta wakikosa ushawishi wa kuanza wakati kikosi hicho kikiangamia.

“Niliangalia mechi, kwangu niliona Simba ilicheza vizuri, mpango wa mechi kutoka kwa makocha ulikuwa sahihi hata wachezaji walijituma vizuri, lakini shida ilishindwa kuamua matokeo yenyewe kwa kukosa watu sahihi katika eneo la ushambuliaji,” alisema Robertinho na kuongeza;

“Ukiwa na mtu kama Jean Baleke timu isingepoteza nafasi zote zile hata kama alikuwa sio mshambuliaji mwenye ubora mkubwa, unaweza kujiuliza wale washambuliaji wapya walikuja kufanya nini wakati mechi kubwa kama ile wanakosa nafasi ya kutumika kikosi cha kwanza?

“Ushauri wangu wanatakiwa kuachana nao kama Simba itatolewa hapa kwani, hawana maana ya uwepo wao, Simba ilikuwa na malengo ya kucheza nusu fainali na mpaka sasa unaona njia ni ngumu ya kufika huko kwa kuwa tayari nafasi ya kukamilisha hilo imeshapotea kwa kutoshinda nyumbani.”

Pia Robertinho alisema Simba bado ina nafasi yakufanya kitu tofauti itakapokwenda Cairo endapo wachezaji watajisahihisha kwa kutengeneza nafasi na kuzitumia.

“Makocha wanaweza kuongea na Kibu (Denis) na wengine, wanatakiwa kutulia, lolote linaweza kutokea, wakati tunatoka nao sare hapo Dar es Salaam ya 2-2 wengi waliona kama tunakwenda kupoteza vibaya ugenini, lakini haikuwa hivyo tukakaa chini na kuwapa kazi ngumu na kufunga njia zao na sisi ndio tulitangulia kuwafunga bahati mbaya wakarudisha baadaye na kuisha kwa sare ya 1-1.”

Simba inahitaji ushindi wa mabao 2-0 mbele ya Al Ahly inayoshikilia taji la 11 la michuano hiyo kwa sasa katika mechi ya marudiano itakayopigwa Ijumaa jijini Cairo ili kwenda nusu fainali na kukutana ama na TP Mazembe ya DR Congo au Petro de Luanda ya Angola zilizotoka suluhu jijini Lubumbashi.

Kwa misimu minne kati ya mitano iliyopita ambayo Simba imeshiriki michuano ya kimataifa ya CAF kuanzia 2018-2019, timu hiyo imejikuta ikishindwa kuvuka robo fainali ikiwamo mara tatu za Ligi ya Mabingwa Afrika na moja ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Hii ni mara ya tano kwa timu hiyo kufika hatua hiyo na sasa inasubiri mechi ya marudiano kuona kama itavunja mwiko na kufuzu nusu fainali kurejea tukio la mwaka 1974 wakati Ligi ya Mabingwa Afrika ikifahamika kwa jina la Klabu Bingwa Afrika ilipoing’oa Hearts of Oak ya Ghana kwa mabao 2-1.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza nyumbani Simba ilitoka suluhu na Waghana na ilipoenda ugenini ikashinda 2-1 na kukutana na Mehalla El Kubra iliyoing’oa kwa penalti 3-0 baada ya kila moja kushinda nyumbani kwa bao 1-0.

Pia iliwahi kufika nusu fainali ya michuano ya Kombe la CAF mwaka 1993 kwa kuing’oa USM El Harrach ya Algeria kwa ushindi wa jumla wa mabao 3-1 na katika fainali iliitoa Atletico Sport Aviacao ya Angola kwa mabao 3-1 kabla kuvuka hadi fainali na kupoteza mbele ya Stella Abidjan ya Ivory Coast.

SOMA NA HII  KUELEKEA MECHI DHIDI YA AZAM..NABI FUNGUKA MAMBO KUWA MAGUMU KWA YANGA..ATOA TAHADHARI..