Home Habari za michezo SIMBA BADO KUNAFUKUTA MOTO…ZIMBWE JR AWAACHIA MSALA HUU WAZAWA

SIMBA BADO KUNAFUKUTA MOTO…ZIMBWE JR AWAACHIA MSALA HUU WAZAWA

ZIMBWE JR AKUBALI KUPITIA NYAKATI NGUMU...KUMBE SIMBA WALICHUKUA MATAJI 5

Simba bado kunafukuta Timu hiyo inapitia kipindi kigumu cha mpito ambacho mambo mengi yametokea na yatatokea lakini wakijipanga vizuri yatapita na wakali hao wa Msimbazi watarejea kwenye ubora na uimara wao kama taasisi imara ya soka.
Wakati upepo huo ukiendelea kupita Simba, Mwanaspoti inakudokeza sababu nyingine ambayo imeifanya timu hiyo kukosa uimara. Si nyingine ni wachezaji wazawa

Simba kwa miaka ya hivi karibuni imekuwa eneo gumu sana kwa wachezaji wazawa wanaosajiliwa kupata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza na kuonyesha ubora.

Wengi husajiliwa kisha baadaye kuondoka baada ya kushindwa kupata nafasi kutokana na sababu mbalimbali.

Ukikiangalia kikosi cha Simba cha sasa mchezaji mzawa anayepata nafasi muda mwingi na amesajiliwa katika minne ya hivi karibuni ni Kibu Denis, wengine wote hali ni tete na wengi wamesepa zao.

Wazawa pekee unaoweza kusema wanatamba kikosini hapo ni beki wa kulia Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr.’, aliyetua kikosini miaka 10 iliyopita akitokea Kagera Sugar.

Shomari Kapombe na Aishi Manula waliosajiliwa mwaka 2017 kwa pamoja wakitokea Azam FC, na kwa mbali Mzamiru Yassin aliyesajiliwa mwaka 2016 akitokea Mtibwa Sugar labda na Kennedy Juma aliyetua msimbazi 2019 akitokea Singida United.

Msimu huu Simba iliwasajili wazawa kipa Hussein Abel, mabeki Hussein Kazi na David Kameta ‘Duchu’, viungo Abdallah Hamis, Edwin Balua, Ladack Chasambi na Salehe Karabaka lakini wote bado hawajafanya maajabu ndani ya kikosi hicho.

Chilunda tayari amejiondoa na kutimkia KMC lakini hata huko anaanzia benchi, Duchu, Hamis, Kazi, Abel, Chasambi na Salehe wao ni kama wasindikizaji tu, kuna muda benchi la ufundi linaamua kutoa nafasi kidogo kwao na wakati mwingi huishia benchi na kwenye majukwaa.

WASIKIE HAPA
Kocha wa zamani wa Simba, aliyekuwa akiwapa zaidi nafasi wazawa, Mbeligiji Patrick Aussems ‘Uchebe’, alisema wachezaji wengi wa Kitanzania (wazawa) wana vipaji vikubwa lakini Simba inakuwa changamoto kwao kutokana na ushindani wa namba na matarajio.

“Nilijaribu kutoa nafasi kwa kila mchezaji lakini ushindani wa namba ulikuwa mkubwa zaidi. Kuna muda nilikuwa naongea na mchezaji mmoja mmoja (mzawa) na kumueleza malengo ya timu na nini anatakiwa kufanya. Wakati mwingine niliwabadilisha hadi maeneo ya kucheza ili wapate nafasi na kuzoea ushindani lakini mwishowe baadhi yao waliniangusha na kushindwa kufikia malengo,” alisema Aussems anayeinoa AFC Leopards ya Kenya na kuongeza;

“Nadhani tatizo lao kubwa ni maisha ya Simba. Pale kuna presha kubwa hivyo mchezaji akishindwa kuhimili na kuimudu basi itakuwa ngumu kwake kuonyesha kiwango bora.”

Uchebe aliinoa Simba kuanzia Julai 2018 hadi Novemba 2019.
Kiungo Abdulswamad aliyesajiliwa Simba na baadaye kuondoka alisema kilichomkwamisha ni kukosa mwanga baada ya aliyemsajili (Zakaria Hans Pope) kufariki lakini pia kocha hakumwamini.

“Simba nilishindwa kwakuwa aliyenisajili alifariki halafu nikawa sina mwanga. Ujue yule mzee muda mwingi alikuwa akinipa nguvu kuwa naweza na nipambane yupo atanisimamia lakini alivyofariki kila kitu kikabadilika kwani nilikuwa sina msimamizi hivyo nilijawa na hofu na kushindwa kufanya vizuri kutokana na presha ya timu ile,” alisema Abdulswamad na kuongeza; “Jambo jingine sikupewa muda wa kutosha kucheza.

Hauwezi kuonyesha ubora wako bila kucheza hivyo hilo lilikuwa changamoto kutokana na eneo langu nililokuwa nacheza (kiungo), kuwa gumu lakini pia kuwepo na watu waliokuwa maalumu kucheza pale,” alisema Abdulswamad aliyetua Simba mwaka 2021 na kukaa miezi sita tu kisha kuondoka na kujiunga na Ruvu Shooting. Msimu huu Abdulswamad alianza na Coastal Union lakini aliachwa na sasa hana timu.

Nahodha msaidizi wa Simba aliyedumu kikosini hapo kwa miaka 10 na kumudu kupata nafasi katika kikosi cha kwanza licha ya ushindani uliopo, Mohamed Hussein Zimbwe Jr’ alisema siri ya kukaa muda mrefu kwenye timu hiyo ni nidhamu na kujitambua.

“Nidhamu ndio kitu cha msingi lakini pia kujitambua. Kufanya mazoezi sana na kufuata maelekezo ya makocha ndio siri ya mafanikio,” alisema Zimbwe Jr maarufu kama Tshabalala jina la kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini.

“Nidhamu ndio kitu cha msingi lakini pia kujitambua. Kufanya mazoezi sana na kufuata maelekezo ya makocha ndio siri ya mafanikio,” alisema Zimbwe Jr maarufu kama Tshabalala jina la kiungo wa zamani wa timu ya taifa ya Afrika Kusini.

Kocha Juma Mgunda alisema Simba ni sehemu ngumu kucheza kwa mchezaji ambaye hajajiandaa kisawa sawa kisaikolojia kwani kuna presha kubwa.

“Sio kwamba wachezaji wazawa hawana uwezo wa kucheza Simba lakini wanakumbana na changamoto nyingi ambazo wanashindwa kuzitatua. Simba ni timu kubwa, kuna presha ambayo mchezaji asipoihimili basi anakwenda na maji na hilo linawatokea sana wazawa. Kingine ni ushindani wa namba. Siku zote makocha hutoa nafasi kwa mchezaji aliyetayari na aliyefanya vizuri mazoezini,” alisema Mgunda ambaye kwa sasa ni kocha mkuu wa Simba Queens.

Mwanasaikolojia na Mshauri Nasihi, Godfrey Jumbe alisema tatizo kwa wachezaji wengi wazawa kushindwa kucheza soka kwenye klabu kubwa hususani Simba ni kutokana na mambo mengi yanayowazunguka ikiwemo kupata maisha mazuri.

“Hili jambo linasababishwa na mambo mengi. Sitazungumzia mambo ya kiufundi bali saikolojia zaidi.
Wachezaji wengi wazawa wana shida ya kupokea maisha mapya. Timu hizi kubwa zina utamaduni wa kuwapa mishahara na posho kubwa wachezaji tofauti na ilivyo kwa timu nyingine na hapa wengi wao wanajisahau na kusahau kilichowaleta kwenye hizo timu.

“Jambo jingine linalowakumba ni matokeo baada ya kupata hayo maisha makubwa, wengi hujiingiza kwenye matanuzi zaidi na tunajua matanuzi na soka haviendani na huo huwa mwanzo wao kushindwa,” alisema Jumbe aliyeshauri wachezaji wazawa wanaosajiliwa kwenye timu kubwa ikiwemo Simba na

Yanga kutafutiwa waangalizi na wasimamizi (mentors) wa ndani ya timu na maisha ya nje ya timu.

SOMA NA HII  DIARRA ANA UGOMVI GANI NA KIBU DENNS?...INSPECTOR HAROUN AFUNGUKA HAYA