Klabu ya Yanga imefanikwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu ikiwa ni mara ya tatu mfululizo kuanzia msimu wa mwaka 2021/22 na imebakiwa na mechi tatu mkononi.
Ubingwa huo ni wa 30 kwa Yanga, katika historia yake, tangu ilipoanza kufanya hivyo kwa mara ya kwanza mwaka 1968.
Dalili za kutwaa ubingwa msimu huu kwa timu hiyo zilianza kuonekana mapema, kwa baadhi ya mechi zake ilizocheza na hata matokeo ya timu nyingine yalionekana kuwarahisishia kazi mabingwa hao.
Makocha wakubwa duniani, wanasema ili kutwaa ubingwa, kwanza inabidi timu inayousaka izifunge timu ambazo zinaonekana kugombea moja kwa moja taji hilo, au kupata pointi nyingi kutoka kwao.
Yanga ilionekana itakuwa mabingwa wa msimu huu mapema kuanzia Oktoba 23, mwaka jana ilipoichapa Azam FC mabao 3-2, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam licha ya kufungwa katika mechi ya marudiano iliyofanyika Machi 17, mwaka huu.
Baada ya Yanga kugawana pointi tatu na Azam, ikachukua pointi zote sita kutoka kwa watani zao Simba, hivyo ikawa imekusanya pointi tisa kati ya 12, kutoka kwa wapinzani wake wanaoonekana kutaka ubingwa huo.
Novemba 5, mwaka jana ilitoa kipigo cha mabao 5-1 dhidi ya Simba, kabla ya kushinda mechi ya mzunguko wa pili kwa mabao 2-1 mechi iliyochezwa Aprili 20, mwaka huu, katika michezo hiyo miwili ambayo ilionekana kuamua ubingwa kwa Yanga.
Mechi zingine ambazo zilionekana kuamua ubingwa kwa Yanga msimu huu ni dhidi ya Dodoma Jiji iliyochezwa Februari 5, mwaka huu ambapo ilipata ushindi kwa mbinde bao 1-0 na siku tatu baadaye ilipoichapa Mashujaa FC magoli 2-1, mechi zote zikichezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Februari 11, mwaka huu iliwachapa Prisons mabao 2-1, mechi iliyochezwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.
Kwa kiasi kikubwa hizi ndizo mechi zilizoamua ubingwa, na zilizofuata ilionekana kama ni kukamilisha ratiba, ambapo mashabiki wengi walichokuwa wakisubiria timu hiyo itatwaa ubingwa lini na kabla ya mechi gani kwa sababu tayari ilikuwa imeziacha Simba na Azam kwa tofauti kubwa ya pointi.
Hata hivyo, mechi hizo za Yanga zilirahisishwa zaidi na mechi ambazo Simba na Azam zilishindwa kasi ya kukimbizana na mabingwa hao.
Simba ilionekana kuisaidia Yanga kutwaa ubingwa ilipotoa sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo Novemba 9, mwaka jana na sare ya mabao 2-2 dhidi ya timu hiyo hiyo waliporudiana Aprili 30, mwaka huu kwenye Uwanja wa Majaliwa ulioko Ruangwa mkoani, Lindi.
Sare ya mabao 2-2 dhidi ya KMC, Desemba 23, mwaka jana pia iliipoteza Simba katika mbizo na kuibeba Yanga, sare ya bao 1-1 dhidi ya Ihefu na kipigo cha mabao 2-1 kutoka kwa Prisons lakini pia suluhu dhidi ya Kagera Sugar pia iliwarahisishia kazi kwa mabingwa hao.
Azam nayo ambayo ilijinasibu msimu huu kutwaa ubingwa, iliathiriwa na suluhu dhidi ya Dodoma Jiji, kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya Yanga, kipigo kingine cha nyumbani cha mabao 3-1 dhidi ya Namungo, sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba, Februari 9, mwaka huu, zikifuatia zingine dhidi ya Coastal Union, Prisons, kabla ya kipigo cha mabao 3-0 dhidi ya Simba, Mei 9, mwaka huu, Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, kilizima ndoto za kutwaa taji hilo na Yanga ikachukua ubingwa kabla ya mechi tatu Ligi Kuu msimu huu kumalizika.
Yanga imetwaa ubingwa mara ya tatu mfululizo, ikiwa ni mara ya nne katika historia ya soka nchini kufanya hivyo.
Ilifanya hivyo mwaka 1991, hadi 1993, ikatwaa tena mara tatu mfululizo mwaka 1996 hadi 1998, ikarudi tena msimu wa 2014/15, hadi 2016/7, na hii ni mara ya nne, kuanzia 2021/22.
Timu hiyo pia ina rekodi ya kutwaa mara tano mfululizo kuanzia mwaka 1968 hadi 1972, kama ilivyokuwa na watani zao wa jadi, Simba ambao walifanya hivyo mara tano pia kuanzia mwaka 1976 hadi 1980.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe, aliliambia gazeti hili timu hiyo itakabidhiwa Kombe la Ubingwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa baada ya kuwakaribisha Tabora United, ambapo wachezaji wa timu pinzani watasimama kwa ajili ya ‘paredi’ maalumu kabla ya mechi hiyo kuanza.
Hiyo itakuwa kabla ya mechi yao ya kumaliza msimu ambayo itachezwa Mei 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Complex dhidi ya Prisons.