KIKOSI cha Simba kipo jijini Arusha na leo jioni kimeshuka katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid kuikabili KMC na kushinda kwa goli 1-0 katika pambano la Ligi Kuu Bara, straika wa zamani wa Wekundu hao, Chris Mugalu amevunja ukimya na kufichua kitu kinachowatafuna kwa misimu mitatu mfululizo sasa.
Mugalu aliyeichezea Simba kwa misimu miwili kuanzia 2020-2022 na kutwaa mataji matatu tofauti likiwamo moja la Ligi Kuu Bara , Kombe la FA na Ngao ya Jamii kabla ya kutemwa na kwenda Al Quwa Al Jawiya ya Iraq akimpisha Jean Baleke, amesema kufeli kwa Simba kumetokana na kushindwa kudumu na washambuliaji.
Mugalu aliyemaliza nafsi ya pili ya wafungaji Bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2020-2021 nyuma ya John Bocco, ameliambia Mwanaspoti kwamba, timu yoyote inajengwa na safu imara ya ushambuliaji na mabeki, lakini hilo upande wa Simba hakuna kwani kila msimu inapangua safu hizo na hivyo kuyumba.
“Nimecheza Simba kwa mafanikio na nafurahia kwani nilikuwa na bahati niliweza kucheza na kupachika mabao mengi, silaumu kwa kuachwa kwani nilikuwa nimetoka majeruhi nilishindwa kuendeleza ubora lakini ukifuatilia mbali nami, kuna wachezaji wazuri waliachwa na Simba wakiwa bado wana ubora,” amesema Mugalu na kuongeza:
“Timu haiwezi kufanya usajili maeneo hayo muhimu kila msimu beki ni eneo ambalo linahitajika kujengwa na wachezaji ambao wanakaa pamoja zaidi ya misimu miwili hati minne sawa na eneo la ushambuliaji kulikuwa na sababu gani ya kuachana na Jeana Baleke aliyekuwa tayari alijenga maelewano na viungo?”
Mugalu amesema ni kweli wachezaji wanashuka viwango, ila Simba haikupaswa kuachana na wachezaji hao wote wanaocheza eneo moja na kusajili wachezaji wapya kati kati ya msimu huko sio kujenga timu imara.
“Mataifa mengi ambayo yamefanikiwa kimpira yana wachezaji wakongwe na wazoefu kwenye timu mfano nimecheza Simba nilimkuta John Bocco ni mchezaji ambaye alikuwa ananipa misingi na aina ya uchezaji wa timu hiyo,” amesema na kuongeza:
“Hiyo ilinisaidia kuingia haraka kwenye mfumo na kuweza kucheza kwa mafanikio hilo linatakiwa kuendelezwa kwa kuwa na wachezaji wazoefu kwenye kila nafasi ambao hata wasipokusaidia kiutendaji, kimbinu watasaidia kwa kutoa maelekezo kwa wachezaji ambao sasa wanasema damu changa.”
Mugalu amesema Simba ikijenga misingi imara kwa kuamini katika sajili wanazozifanya ndani ya misimu mitatu hadi minne itaweza kupiga hatua kama ilivyo kwa watani zao Yanga ambao amewataja kuwa wamekuwa bora baada ya kuwekeza misimu minne.
“Kipindi Simba inafanya vizuri, Yanga ilikuwa inasajili kila msimu wakiamini walikuwa wanakosea kumbe ni ubora wa wapinzani na hilo ndilo linawakuta Simba kwa sasa. Inasajili na kuacha hawapaswi kufanya hivyo wajenge imani na wachezaji wao kwa kuwajenga, watatoboa,” amesema Mugalu ambaye hana timu kwa sasa.