Home Habari za Simba Leo JOSHUA MUTALE ATABIRIWA MAKUBWA…FADLU DAVIDS ATOA USHUHUDA.

JOSHUA MUTALE ATABIRIWA MAKUBWA…FADLU DAVIDS ATOA USHUHUDA.

HABARI ZA SIMBA- mUTALE

Kocha Mkuu wa Simba SC Fadlu Davids, amemtabiria makubwa Joshua Mutale, kuwa mmoja wa wachezaji watakaong’ara sana ndani ya kikosi chake msimu ujao.

Akizungumza akiwa Ismailia nchini Misri ambako kikosi hicho kinajiandaa na msimu mpya wa mashindano, Fadlu alisema katika mazoezi ya timu hiyo, moja ya kitu anachoshuhudia ni kipaji na uwezo mkubwa wa Mutale katika kutafuta nafasi yeye mwenyewe, kuwatengeneza wenzake, lakini akiwa hatari zaidi anapobaki na beki mmoja.

Kocha huyo mpya raia wa Afrika Kusini, alikuwa akizungumzia maendeleo ya maandalizi ya kikosi chake, huku akisema yanaelekea ukingoni.

“Hapa tuna Mutale, yeye ana uwezo mkubwa mno na kukimbia kwenye nafasi, kutengeneza nafasi kwa wenzake, ni hatari anapobaki na beki mmoja, nadhani anaweza kung’ara sana kwenye kikosi chetu.

“kingine tunachoangalia ni kutengeneza safu ngumu ya ulinzi na jinsi ya kucheza wakati hatuna mpira, na hapa naangalia kipaji cha mchezaji mmoja mmoja, nini anafanya wakati ana mpira na anachotoa wakati timu haina mpira mguuni. Kikosi cha Simba lazima kicheze kwa staili ya kuvutia,” alisema kocha huyo.

Alikuwa akizungumzia aina yake na staili anayopenda kucheza na anataka kikosi chake kicheze kwa kasi sana, hivyo anahitaji wawe na pumzi ya kutosha.

“Nadhani ‘pre season’ inakaribia kumalizika, wiki iliyopita tulicheza mechi ya wenyewe kwa wenyewe, yaani wachezaji wangu niliwagawanya na kukipiga, nimeona jinsi wanavyopambana, ushindani ulikuwa mkubwa sana.

“ila tunataka kubalansi baadhi ya maeneo machache tu, lakini kikubwa ni kwamba zaidi ya asilimia 90 kila kitu kiko sawa, eneo la ufiti wa wachezaji tumelifanyia kazi kwa kiasi kikubwa kwa sababu soka langu nataka wachezaji wacheze kwa spidi sana, hivyo ni lazima wawe na pumzi ya kutosha na utimamu wa mwili, kilichopo sasa ni kutafuta muunganiko, sasa ni wajibu wao uwanja kukimbia kwenye maeneo ya kutengeneza nafasi,” alisema.

Alisema anadhani kuna vitu vichache tu vilivyobaki ikiwamo kuwatengeneza wachezaji hasa wapya waweze kujiweka sawa kisaikolojia kucheza mechi ya Simba Day mbele ya mashabiki zaidi ya 60,000, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

“Nawatengeneza wachezaji hasa wapya kwa ajili ya kucheza kwenye uwanja mkubwa kama wa Mkapa, ukiwa na watazamaji 60,000 ili kuweza kuzuia presha pamoja na hisia zao, pamoja na zile watakazozipata kutoka kwa mashabiki,” alisema.

Simba inateremka dimbani leo kucheza na timu ya Daraja la Pili nchini Misri, El-Qanah, itakayopigwa saa 11:30 jioni kwa za Tanzania, huku kocha Fadlu, akisema baada ya hiyo kutakuwa na mechi zingine mbili za kujipima nguvu.

SOMA NA HII  KIUNGO HUYU YANGA NDIO BASI TENA...AFANYIWA UPASUAJI WA GOTI....KUIKOSA MECHI NA SIMBA