Home Habari za Simba Leo BEKI SIMBA AFICHUA SIRI ZA JOSHUA MUTALE…JAMAA ANAJUA BALAA

BEKI SIMBA AFICHUA SIRI ZA JOSHUA MUTALE…JAMAA ANAJUA BALAA

HABARI ZA SIMBA- mUTALE

MNYAMA SIMBA amejichimbia huko Ismailia Misri kujinoa zaidi kabla ya kuanza kwa msimu mpya, itakumbukwa klabu hiyo imefanya sajili nyingi za kutisha moja ya sajili hizo ni Joshua Mutale winga mwenye kasi ya SGR.

Beki mmoja wa Simba bila kusita amemwaga sifa kwa mchezaji huyo wa Kizambia Mutale, hiyo ni baada ya kukutana nae uwanja wa mazoezi na kuoneshana uwezo.

Mutale ametua Simba hivi karibuni akitokea Power Dynamos akitajwa kumudu nafasi zaidi moja uwanjani, licha ya kucheza zaidi kama fowadi au winga, akiwa ni mmoja kati ya wachezaji 13 wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu mpya na unaambiwa huko kambini keshaanza mambo yake mapema na kuwa kivutio.

Beki mmoja wa kikosi hicho aliyekuwepo msimu uliopita, Hussein Kazi, amevujisha faili zima la nyota kutoka wa kimataifa wa Chipolopolo, tangu watue kambini huko Misri, akisema ukiacha ufanisi wake uwanja wa mazoezi, lakini ndiye komedi kutokana na ucheshi alionao na kumzoea kila mtu kwa haraka.

Kazi aliyekuwa katika kundi la pili la msafara sambamba na benchi zima la ufundi ukimuondoa Seleman Matola aliyetangulia mapema, aliliambia Mwanaspoti kuwa, tangu atue Misri, hakuna mchezaji anayechekesha wenzake kwa mastaa wapya kama Mutale na kumtaja ni mtu anayezoeana na kila mmoja bila kubagua.

“Sio kuchekesha wenzake na kuzoeana na kila mtu aliye kambini, lakini anapenda sana kujifunza kiswahili kwani kila neno analolisikia analiulizia ili kuielewa lugha hiyo, tofauti na wachezaji wengine wapya waliotua ndani ya timu,” alisema Kazi aliyesajiliwa msimu uliopita akitokea Geita Gold na kuongeza;

“Hadi sasaa namuona Mutale ndiye anayezoea watu kwa haraka, mcheshi anapokuwepo lazima utacheka, ukiachana na hilo namuona ana vitu vikubwa vya kuisaidia timu kwani ni mchezaji mwenye kipaji cha soka haswa na kila mmoja namfurahia hapa.

“Siku zote mchezaji fundi anaonekana katika mazoezi, jinsi anavyochezea mipira, jambo la msingi tunajipanga kuhakikisha msimu ujao unakuwa wa kicheko kwetu.”

Beki huyo wa kazi pia, alizungumzia kuhusiana na ongezeko la wachezaji wa kigeni, jinsi linavyoibua ushindani mkali katika mazoezi yao, kila mmoja akichangamkia fursa ya kupata namba kikosi cha kwanza.

“Kwanza waliosajiliwa ni vijana, kwa hiyo tumekutana wote vijana, ushindani ni mkubwa, makocha wanatujenga kimbinu na kiakili,” alisema Kazi aliyejikuta akimwaga machozi kmara baada ya mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara ya Dabi ya Kariakoo baada ya kusababisha penalti iliyozaa bao la kuongoza la Yanga lililowekwa kimiani na Stephane Aziz KI, kisha Joseph Guede kupiga chuma cha pili wakati Simba ikifa kwa mabao 2-1.

Kazi aliingia katika mchezo huo akitokea benchi baada ya Henock Inonga kuumia na dakika chache tu ndipo alipomkwatua Aziz KI aliyeipiga penalti na mwisho wa pambano Yanga ilihitimisha ushindi mwingine mbele ya Mnyama baada ya awali kuichapa mabao 5-1 mechi ya Novemba 5 mwaka jana.

Mara baada ya mchezo huo, Kazi alimwaga chozi na kuwapa kazi wachezaji wenzake wakiwamo wa Yanga waliongozwa na Khalid Aucho na Aziz KI pamoja na kocha Matola kushirikiana kumtuliza.

Simba na Yanga zinatarajiwa kukutana tena katika nusu fainali ya mechi za Ngao ya Jamii siku ya Wakulima, Nane Nane kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku Azam na Coastal zenyewe zitapepetana New Amaan Complex, mjini Unguja visiwani Zanzibar.

SOMA NA HII  BALEKE ATANGAZA VITA NA PRINCE DUBE...KAZI KAIANZA.