Home Habari za Simba Leo KWA MARA YA KWANZA STEVE MUKWALA NA MUTALE WAFUNGUKA

KWA MARA YA KWANZA STEVE MUKWALA NA MUTALE WAFUNGUKA

HABARI ZA SIMBA- MUKWALA

KIKOSI cha Simba kinaendelea kujifua kambini jijini Ismailia, Misri kujiandaa na msimu mpya wa mashindano, huku mastaa wawili wapya wa timu hiyo, Joshua Mutale na Steven Mukwala wakivunja ukimya na kufunguka kwa mara ya kwanza walivyotua Msimbazi na walivyojiandaa kuwapa raha mashabiki.

Nyota hao wawili ni kati ya wachezaji wapya saba waliotua katika kikosi cha Simba wakiunga na wengine watano waliokuwapo msimu uliopita na wote ni kati ya wachezaji wa kwanza kutimba mapema kambini Misri kujifua, Mutale akitokea Power Dyanamos ya Zambia na Mukwala akitua kutoka Asante Kotoko yas Ghana.

Wakizungumza na mtandao wa klabu hiyo ya Simba, Mukwala ambaye ni Mghana, alisema baada ya kupokea simu ya mabosi wa Wekundu kuhitaji huduma yake alijiona anakwenda kutimiza ndoto ya muda mrefu, aliyokuwa ya kuichezea klabu kubwa Afrika.

Mukwala alisema rekodi tamu za Simba katika michuano ya CAF ni moja ya sababu kubwa iliyomvuta kujiunga na klabu hiyo, kwani alikuwa akitamani siku moja aje kuitumikia na kama utani msimu ujao atavaa uzi Mwekunud na Mweupe wa Mnyama.

Mshambuliaji huyo alisema kabla ya kufanya uamuzi alilazimika kuwasiliana na Emmanuel Okwi, nyota aliyewahi kuwika na Simba kwa vipindi tofauti na kumhakikisha anaenda klabu sahihi.

“Kabla ya kusaini nilimfuata Emmanuel Okwi, ambaye kwangu ni baba katika karia yangu ya soka, nikamuuliza asilia ya Simba ipoje, presha ya mashabiki, japo hili kwangu hainiogopeshi kwani nimetoka timu ambayo ina mashabiki wengi wenye presha kubwa, naye alinikihakikisha kila kitu,” alisema Mukwala.

“Japo sio mpenzi wa kusoma kila ujumbe ambao natumiwa na mashabiki wanaokuja katika mitandao yangu ya kijamii, huwa naambiwa na watu wangu wa karibu jinsi ambavyo mashabiki wa Simba wananizungumzia kwa uzuri na kunikaribisha kufanya kazi ya kuisaidia klabu.” Pia alifunguka juu ya kupenda kutumia a.k.a ya M9 kwa kufafanua kuwa; “Nimefupisha jina langu la Mukwala, hiyo 9 ni kwa sababu nacheza namba 9 asilia kabisa, ndio maana nikaitwa M9.”

Mbali na hilo, pia nyota huyo mpya alisema usajili uliofanywa na Simba, kwa kuleta vijana wengi ambao wapo tayari kujifunza na kuonyesha uwezo, anaamini jambo litakaloleta manufaa kwa klabu hiyo na kwamba kwa sasa anasubiri kuanza kwa Ligi Kuu na michuano mingine ili kuwapa mashabiki kitu wanachokisubiri.

Kwa upande wa Mutale, alisema walichokifanya Wazambia wenzake ndani ya Simba kwa maana ya Moses Phiri na Clatous Chama aliyejiunga Yanga, kimewapa imani Simba na kuwaamini wachezaji wanaotoka Zambia na kwamba hataki kuwaangusha wakati anaitumikia klabu hiyo.

“Nimejiunga Simba ili kuandika rekodi zangu na kuweka historia yangu, ambayo itakuwa inasimuliwa kama zinavyosimuliwa za kaka zangu hao (Chama na Phiri), hivyo nafahamu kwamba natakiwa kufanya kazi kwa bidii zaidi kufanikisha hilo,” alisema Mutale.

“Mashabiki wa Simba wamenipokea vizuri, nimeona nimepata wafuasi wengi katika mitandao ya kijamii, wengi wakinikaribisha, naamini msimu ujao utakuwa mzuri kwa upande wetu. Tusubiri tuone.”

Mutale (22) anamudu kucheza nafasi nyingi ikiwamo nyuma ya mshambuliaji na winga zote mbili, na akiwa na Dynamos msimu uliopita alifunga mabao matano na kuasisti matatu katika mechi 26.

Mbali na nyota hao wawili, wachezaji wengine wapya wa kigeni wa Simba ni mabeki, Valentin Nouma na Chamou Karabou, viungo Debora Mavambo, Augustine Okejepha na Charles Ahoua wanaoungana na Fabrice Ngoma, Ayoub Lakred, Che Fondoh Malone, Freddy Michael na Willy Onana.

SOMA NA HII  AISEE!! NABI AZINYAKA SIRI ZA INONGA...AWAKABIDHI MAYELE NA MUSONDA...ISHU NZIMA HII HAPA A-Z