Habari za Simba Leo
JOSHUA MUTALE ATABIRIWA MAKUBWA…FADLU DAVIDS ATOA USHUHUDA.
Kocha Mkuu wa Simba SC Fadlu Davids, amemtabiria makubwa Joshua Mutale, kuwa mmoja wa wachezaji watakaong’ara sana ndani ya kikosi chake msimu ujao.
Akizungumza akiwa Ismailia nchini Misri ambako kikosi hicho kinajiandaa na msimu mpya wa mashindano, Fadlu alisema katika mazoezi ya timu hiyo, moja ya kitu anachoshuhudia ni kipaji na uwezo mkubwa wa Mutale katika kutafuta nafasi yeye mwenyewe, kuwatengeneza wenzake, lakini akiwa hatari zaidi anapobaki na beki mmoja.
Kocha huyo mpya raia wa Afrika Kusini, alikuwa akizungumzia maendeleo ya maandalizi ya kikosi chake, huku akisema yanaelekea ukingoni.
“Hapa tuna Mutale, yeye ana uwezo mkubwa mno na kukimbia kwenye nafasi, kutengeneza nafasi kwa wenzake, ni hatari anapobaki na beki mmoja, nadhani anaweza kung’ara sana kwenye kikosi chetu.
“kingine tunachoangalia ni kutengeneza safu ngumu ya ulinzi na jinsi ya kucheza wakati hatuna mpira, na hapa naangalia kipaji cha mchezaji mmoja mmoja, nini anafanya wakati ana mpira na anachotoa wakati timu haina mpira mguuni. Kikosi cha Simba lazima kicheze kwa staili ya kuvutia,” alisema kocha huyo.