Coastal Union Yaanza Mipango ya Kumsajili Farid Mussa Kutoka Yanga
Uongozi wa Coastal Union umeanza hesabu kali za kuiwinda saini ya winga machachari wa Yanga, Farid Mussa, lengo likiwa ni kuongeza nguvu kikosini hapo kuelekea msimu mpya wa ligi.
Hatua hiyo inajiri baada ya nyota huyo kumaliza mkataba wake na mabingwa hao wa Ligi Kuu Bara, jambo linalomfanya kuwa mchezaji huru sokoni.
Taarifa za ndani kutoka Coastal Union zinaeleza kuwa Farid ni miongoni mwa wachezaji wa kipaumbele wanaotakiwa na benchi la fundi, na tayari mazungumzo ya awali kati ya pande zote mbili yameanza ingawa bado hayajafikia makubaliano ya mwisho.
“Ni kweli Farid yupo katika mipango yetu na ikiwa kila kitu kitaenda sawa tunaweza kukamilisha usajili wake. Kilichobaki kwa sasa ni kukubaliana maslahi yake binafsi,” kilisema chanzo kutoka ndani ya klabu hiyo.
Akizungumzia uvumi huo, Katibu Mkuu wa Coastal Union, Omary Ayoub, alisema klabu hiyo itamtambulisha rasmi mchezaji yeyote watakayefikia naye makubaliano kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii, huku akiepuka kuingia undani wa usajili wa Farid kwa sasa.
Kumalizika kwa mkataba wa Farid Mussa ndani ya Yanga bila uwepo wa mazungumzo mapya ya kuongeza mkataba kumefungua milango kwa klabu mbalimbali kuwania saini yake, huku Coastal Union ikionekana kuongoza mbio hizo.
Farid Mussa ana uzoefu mkubwa wa soka la ndani na kimataifa, akiwa miongoni mwa wachezaji wazawa waliocheza soka la kulipwa Ulaya katika klabu ya CD Tenerife B ya Hispania akitokea Azam FC, kabla ya kujiunga na Yanga mnamo Agosti 12, 2020.