Clatous Chama: Bao Langu Dhidi ya Yanga Linastahili Tuzo ya Puskas
KIUNGO mshambuliaji na nyota wa Simba SC, Clatous Chama, amesema bao la aina yake alilofunga dhidi ya Yanga katika mchezo wa Kariakoo Derby msimu uliopita lina sifa zote za kuwania Tuzo ya Puskas kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Chama alifunga bao hilo la ustadi wa hali ya juu katika mchezo uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, ambapo alimchungulia mlinda mlango wa Yanga, Djigui Diarra, na kupiga shuti lililochochea mjadala mkubwa ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Akizungumzia bao hilo, Chama amebainisha kuwa pamoja na kwamba matokeo ya sare yalimuumiza kwa sababu yalirudisha nyuma mbio zao za ubingwa, bado anakumbuka mchezo huo kwa hisia tofauti.
“Bao nililofunga dhidi ya Yanga bado nalikumbuka sana. Kinachoniuma zaidi ni kwamba tuliambulia sare, lakini kama tungepata ushindi, jambo hilo lingebadili mwelekeo wa mbio za ubingwa,” alisema Chama.
Nyota huyo aliongeza kuwa kuingia au kushinda Tuzo ya Puskas kwa bao hilo haitakuwa heshima kwake pekee, bali kwa soka la Tanzania kwa ujumla:
“Naamini kabisa lile ni bao linalostahili kuwania Puskas. Nilimsoma Diarra akiwa ametoka kwenye nafasi yake, nikafunga bila hata kuangalia golini. Likipata nafasi huko na hata kushinda, nitafurahi sana kwa sababu litatoa thamani na heshima kubwa kwa soka la Tanzania.”
Atangaza Rasmi Kustaafu Timu ya Taifa ya Zambia
Katika hatua nyingine, kiungo huyo wa kimataifa amethibitisha kustaafu rasmi kuitumikia timu yake ya taifa ya Zambia (Chipolopolo), ili kupisha kizazi kipya cha wachezaji chipukizi.
Chama alisema kuwa sasa hivi atabaki kuwa shabiki na mwombaji mkubwa wa timu hiyo ya taifa:
“Kwa sasa nimestaafu kuitumikia timu ya taifa. Nitaendelea kuiunga mkono na kuiombea mafanikio mema. Pamoja na yote, natamani kuiona Zambia ikifuzu na kufanya vizuri kwenye fainali za AFCON 2027.”
Kwa sasa, Clatous Chama yupo nchini Rwanda pamoja na kikosi cha Simba kinachoendelea na kambi ya maandalizi ya msimu mpya chini ya kocha mkuu Steve Barker, tayari kwa ajili ya michezo ya ndani na ile ya kimataifa.